mashoga na machangodoa kunufaika elimu ya ukimwi shinyanga.
Wakati serikali ikiendelea na zoezi la
kamata kamata ya wanawake
wanaojihusisha na biashara ya ngono
“kuuza miili yao” Madiwani wa
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga
wameliruhusu Shirika lisilo la kiserikali la
Rafiki SDO kuendelea kutoa elimu ya
UKIMWI kwa wanawake wanaojihusisha
na biashara ya ngono “machangudoa” na
wanaume wanaofanya ngono na wanaume
wenzao “Mashoga”,anaripoti Kadama
Malunde.
Madiwani hao wamebariki mradi huo
uendelee kwa masharti ya shirika hilo,
kutumia wataalam wa afya kutoa elimu ya
Ukimwi, kutoruhusu ndoa ya jinsia moja
na kutowapatia mafuta ya vilainishi
vinavyosaidia kupunguza michubuko
wakati wa tendo la ndoa ili kuhamasisha
ngono kwao kama ilivyoripotiwa hapo
awali.
Madiwani waliazimia kuliruhusu shirika
hilo jana kwenye kikao cha dharura cha
baraza lao likiwa na ajenda moja ya
kupata ufafanuzi juu ya shughuli za Mradi
wa Shirika hilo la utoaji wa Elimu ya
UKIMWI kwa watu hao, baada kutoa
tamko la kusitisha shughuli zake kwenye
kikao kilichopita, kwamba Shirika la Rafiki
linatakiwa litoe ufafanuzi wa kina kuhusu
elimu hiyo ili kuepuka kukiuka tamaduni
za kiafrika.
Shirika hilo hapo awali lilizuiwa kufanya
kazi zake mwezi Machi mwaka huu na
Madiwani hao baada ya kupata taarifa ya
kufanya kazi zake kinyemelea kwenye kata
zao ”bila kushirikisha madiwani” huku
kukiwa na madai kuwa wanakusanya
Machangudoa na Mashoga na kisha
kuwahamasisha kuendelea kuuza miili yao
pamoja na kuwapatia mafuta ya vilainishi
wanaume wanaofanya ngono na wanaume
wenzao.
Akitoa ufafanuzi kuhusu namna shirika
hilo lisilo la kiserikali, mkurugenzi wa
Shirika la Rafiki Gerald Ng’ong’a, alisema
elimu wanayoitoa kwa machangudoa na
mashoga ni kuwazuia kuendelea na
biashara hiyo na kuwahamasisha
kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali
ili wajikwamue kiuchumi.
“Mimi ni mkristo kamwe siwezi kubadili
mila na desturi za kiafrika kwa sababu ya
mzungu, mradi huu unatekelezwa katika
mikoa 11 Tanzania, ndugu zangu siku
zote linapotokea jambo yanazungumzwa
mengi, kuna wengine wanakuwa
hawaelewi matokeo yake kupotosha
jamii”,alisema Ng’ong’a.
“Naomba radhi kwa taarifa zilizoenezwa
hapo awali kuwa tunafanya shughuli ya
kuchochea ngono, kutetea mashoga
pamoja na makahaba. Nakiri kuwa
tulifanya kosa kutotambulisha mradi wetu
kwa madiwani na kutoipatia taarifa ofisi
ya mkurugenzi, ninakiri hapo tulikosea
ndiyo maana zikaenea kwenu taarifa
ambazo ni za upotoshaji”, alieleza
Ng’ong’a.
Alisema lengo la mradi wa Sauti
uliozinduliwa mwezi Agosti mwaka 2015
na katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga
ni kuboresha afya za watu kupitia njia
endelevu na umekusudia kupunguza
kiwango cha maambukizi ya VVU mkoani
Shinyanga ambayo sasa ni asilimia 7.4
hivyo umelenga kutoa elimu kwa makundi
maalumu hususani ambayo ndiyo
yanasambaza kwa kasi VVU.
Ng’ong’a alibainisha kuwa shirika lake
linajihusisha na ushauri nasaha na
upimaji wa VVU na kutoka elimu ya
ujasiriamali kwa makundi hayo maalum ili
kupunguza idadi ya wanawake wanaouza
miili yao na wanaume wanaofanya ngono
na wanaume wenzao kwani ujasiriamali
huo utawafanya wasiwaze tena biashara
ya ngono.
Mkurugenzi huyo wa shirika la Rafiki
aliyataja makundi maalumu waliyoyalenga
kuwa ni vijana hususani mabinti walio
katika umri balehe, wanawake
wanaojihusisha na biashara ya ngono na
wanaume wanaofanya ngono na wanaume
wenzao.
Aliongeza kuwa wameamua kuhusika zaidi
na makundi hayo kwa sababu ndiyo yapo
hatarini zaidi kwa maambukizi ya VVU na
kwamba wateja wa watu hao wapo katika
jamii wakiwemo waume za watu na wake
za watu na kusisitiza kuwa vijana ndiyo
wahanga wakubwa.
Hata hivyo Ng’ong’a alikanusha kuwa
shirika lake linagawa vilainishi kwa
mashoga kwa ajili ya kupunguza
michubuko wakati wa tendo la ndoa na
kudai kuwa vilainishi hutolewa na
madaktari kwa sababu maalumu siyo
kugawiwa tu kama kondomu.
Akieleza zaidi juu ya namna wanavyofanya
kazi Ng’ong’a alisema wanaotoa elimu ya
UKIMWI na Ujasiriamali kupitia kwa vijana
waliowapatia mafunzo maalum na mpaka
sasa wana vijana 50 kutoka kata 15 za
manispaa ya Shinyanga.
Hata hivyo Madiwani hao baada ya kupata
ufafanuzi huo waliliruhusu Shirika hilo
kuendelea na shughuli zake, kwa masharti
ya kufuata taratibu za nchi na
kutokuvunja sheria za maadili ya kiafrika
pamoja na kutumia wataalamu wa afya
kutoa elimu hiyo, na wakienda kinyume
na maagizo yao yatasitishwa mara moja.
Akizungumza katika kikao hicho
mwenyekiti wa kikao hicho, ambaye ni
naibu meya wa manispaa ya Shinyanga
Agnes Machiya alisema mradi huo
utatekelezwa katika kata 15 kati ya kata
17 za manispaa ya Shinyanga huku
akisisitiza wahusika wa shirika hilo
kushirikiana na viongozi wa serikali
kuanzia ngazi ya mtaa hadi mkoa ili
kuondoa mkanganyiko katika jamii.
Mradi huo utatekelezwa katika kata za
Kolandoto,Ibinzamata,Ngokolo,Ibadakuli,
Shinyanga
mjini,Chamaguha,Kitangiri,Kizumbi,Ndala,
Kambarage,Chibe,Lubaga,Ndembezi,
Masekelo na Old Shinyanga.
Kata za manispaa ya Shinyanga ambazo
hazijapata bahati ya mradi huo ni
Mwawaza na Mwamalili.
Hata hivyo pamoja na mradi huo
kupitishwa na madiwani hao,baadhi ya
madiwani hawakuridhishwa na kupitishwa
kwa mradi huo wakidai kuwa shughuli
zake zinaenda kinyume na maadili ya
kiafrika hivyo shirika limekosa sifa ya
kufanya kazi katika manispaa hiyo.
Mmoja wa madiwani ambao
hawakuridhishwa na azimio hilo
Mchungaji Jilala Fumbuka kutoka kata ya
Lubaga (Chadema) aliyetoka nje ya kikao
aliiambia Malunde1 blog baada ya kikao
kufungwa kuwa mradi huo unaunganisha
Makahaba na Mashoga kuunda SACCOS
yao hali ambayo ni hatari kwa utamaduni
wa kitanzania na Afrika kwa ujumla na
kuongeza kuwa wanaounga mkono mradi
huo walaaniwe.
“Wanaokubali mradi huu ama kwa
kuhongwa ama kwa utashi wao, adhabu
ya mungu na iwe kwao, haiwezekani
Shinyanga igeuzwe kuwa sodoma na
gomora, hii ni laana kubwa”,alisema
mchungaji Jilala.
Naye mchungaji wa kanisa la Giligali la
mjini Shinyanga Shaneli Sessoa
aliyehudhuria kikao hicho aliiambia
Malunde1 blog kuwa kwa mujibu wa
utafiti alioufanya ni kwamba mradi huo
unatoka nchi ya Marekani inayounga
mkono ndoa za jinsia moja.
“Hili shirika halifai waende za mtu yeyote
anayetoa elimu ya ngono ya jinsia moja
hatakiwi katika jamii yetu kwa niaba ya
wakristo wote siungi mkono uwepo wa
shirika hili, hawa watu wakitoa taarifa
kwa viongozi wa serikali hawasemi kama
wanatoa elimu ya ushoga, lakini utafiti
wangu unaonesha kuwa wanafundishana,
hata hayo mafuta ya vilainishi
wanapeana”, aliongeza mchungaji Sessoa.
“Hata ujio wao una uwalakini,
haiewezekani waingie kwenye kata za
watu bila kuwataarifu viongozi wa maeneo
husika, badala ya kuwaambia waache
biashara ya ngono nyinyi
mnawaunganisha na kuwasaidia, hii ni
hatari sana”, alisema mchungaji huyo.
Mchungaji Sessoa alisema kama
manispaa ya Shinyanga imekubali
kupokea mradi huo ni vyema makahaba
waliokamatwa hivi karibuni wakaachiwa
mara moja ili wakaungane na vikundi vya
wenzao ili wakapate msaada na elimu
bora ya kuendeleza vitendo hivyo.
Katika hatua nyingine mchungaji huyo
aliitaka serikali kutumia rasilimali asili za
kiuchumi ambazo ni nyingi kuliko hata za
Marekani kwa ajili ya kuwasaidia
wananchi wake na kuwajengea uwezo wa
maisha kiuchumi badala ya kuendelea
kutegemea wahisani ambao hutumia
mwanya kuingiza mila na desturi zisizo za
kiafrika.
“Naomba serikali ikubali kutambua
mchango wa taasisi za kidini kuhusu vita
dhidi ya ushoga na Ukimwi,kanisa
linapaswa kushirikishwa katika shughuli
zote zinazohusus jamii kwani kwa asilimia
70 katika nchi hii shughuli za kijamaa
zinafanywa na taasisi za kidini,lakini kwa
maksudi serikali imekuwa haishirikishi
viongozi wa taasisi hizo”,aliongeza
mchungaji Sessoa.
Hata hivyo taarifa za kupokelewa kwa
mradi huo umepokelewa kwa hisia tofauti
na wakazi wa Shinyanga huku wengine
wakidai kuwa ni sahihi kuwakusanya
pamoja makahaba na mashoga ili kuwapa
elimu ya ujasiriamali na Ukimwi ili
kupunguza maambukizi ya VVU kwani hali
inatisha kutokana na biashara hiyo
kukitihiri katika manispaa ya Shinyanga.
Baadhi wananchi waliozungumza na
Malunde1 blog walisema kitendo cha
kukusanya mkahaba na mashoga ni hatari
kwani inachochea vitendo vya ngono na
badala yake ni bora serikali ikaweka
sheria kali kuzuia biashara ya ngono
kwani haiwezekani serikali iendelee
kukamata makahaba na wateja wao huku
watu wengine wakikusanya watu hao na
kuwapa elimu hiyo iliyoleta sintofahamu.
Mradi wa Sauti ni mradi ni wa miaka
mitano unaofadhiliwa na shirika la
maendeleo la misaada la Marekani(USAID)
,ulianza kutekelezwa na shirika la Jhpiego
mwezi Februari mwaka 2015,Jphiego
inashirikiana
naEngenderhealth,Pact,NIMR/Mwanza na
sasa imekabidhi mradi huo kusimamiwa
na shirika la Rafiki kuendeshwa katika chanzo jamii forum.
0 comments :
Post a Comment