Breaking News
Loading...

Advert

Wednesday, January 11, 2017

Ndani ya kanisa la Anglikana hapa nchini hapatoshi hali bado sio nzuri.soma zaid

Hali ya amani ndani ya Kanisa la Anglikana
nchini, bado si nzuri baada ya Askofu wa
Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa
aliyevuliwa uaskofu kutoa msimamo wake na
kudai kuwa yeye ni msafi, na ndio Askofu wa Dar
es Salaam, hang’oki hata kwa dawa, na
amewasamehe wanaompinga.
Askofu Mokiwa aliyasema hayo kwenye Kanisa la
Anglikana Ilala jana, alipozungumza na waandishi
wa habari. Alisema licha ya kusemwa mambo
magumu, lakini yeye kama Askofu, kazi yake ni
kuwaombea waliomkosea na hana matatizo nao,
kwani amekwisha wasamehe.
Askofu Mokiwa pia alienda mbali zaidi kwa kudai
kuwa Dayosisi ya Anglikana Dar es Salaam haina
mgogoro, bali viongozi watano wa dayosisi hiyo
ndio wanatengeneza mgogoro huo kwa maslahi
binafsi, wakitumia Kanisa la Anglikana la
Mtakatifu Andrea la Magomeni kama njia ya
kupitishia migogoro yao.
“Siogopi kusema baba askofu kapotoka katika
hili, ameshauriwa vibaya na washauri wake wa
kisheria,”alisema Askofu Dk Mokiwa ambaye
alimtaja Profesa Palamagamba Kabudi kuwa
mshauri wa kisheria wa askofu mkuu.
Kauli hiyo ya Mokiwa imekuja siku chache baada
ya kuvuliwa uaskofu, kwa kile kilichoelezwa
mashtaka 10 yaliyofunguliwa na walei 32 wa
Kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam, yakiwemo
ya ufisadi wa mali za kanisa, ndio sababu ya
Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Jacob
Chimeledya kumvua uaskofu.
Hata hivyo, Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo,
kwa maelezo kuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar
es Saalam, ambayo ndiyo yenye uamuzi wa
kumfuta kazi na si askofu mkuu; au askofu
mwingine yeyote wa kanisa hilo Tanzania.
Uamuzi wa kumvua uaskofu, ulichukuliwa
mwishoni mwa wiki iliyopita na Askofu
Chimeledya baada ya Askofu Mokiwa kugoma
kujiuzulu, kama ilivyoshauriwa na Nyumba ya
Maaskofu, ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja
mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya
kichungaji, ambayo yalibainishwa kwenye ripoti
ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa
kanisa hilo nchini.
Akizungumzia suala hilo, Mokiwa alisema, “Alikuja
na maaskari zaidi ya 12 ambao wamevaa sare, na
wengine ambao hawakuvaa sare sijawajui idadi
yake, askofu mkuu alidai amekuja kuleta mrejesho
wa halmashauri kuu, na matokeo yake akaishia
kusema ameniondoa kwenye huduma ya uaskofu.
"Nimesema siondoki, na nimeona wanasema
wataweka kila kitu hadharani, nawambia hivi, mimi
ni msafi na sina uchafu sehemu yoyote ile, wawe
huru na amani kuanika madudu yangu kama yapo,
waweke tu hadharani wala siogopi.
“Ninavyo vyombo halali kwenye Dayosisi hii
ambayo hakutaka kukutana navyo ambavyo ni
Halmashauri ya Kudumu, hakuwahi kutaka
kuwasiliana na sisi, sisi tulitaka kuwasiliana na
yeye, angejibu mawasiliano yetu ya kujenga
mahusiano na kutekeleza yaliyoamuliwa, hukutaka
kutekeleza leo unakuja na hoja ya kuniaondoa.
“Halmashauri ya Kudumu inamwambia hatujawahi
kumpelekea mgogoro sisi kama Dayosisi ya Dar es
Salaam, waswahili wanasema ‘jipu linamsumbua
mwenye mwili wake’, hujawahi kupelekewa neno
lolote la machafuko, ni nani aliyekwambia Dayosisi
ya Dar es Salaam ina migogoro?
“Askofu anafanya kazi na sisi, askofu ana vyombo
vya kutawala, hana mamlaka ya kujiamulia mambo
yake mwenyewe, ukisema Dar es Salaam kuna
machafuko wewe Askofu Mkuu tunajua unasimama
na watu na makundi katika Dayosisi hii.
“ Yeye ni askofu kama mimi, yeye yupo Mpwapwa,
tuna taratibu zetu kama za bendera ukiingia mahali
unashusha bendera kidogo, kwa nini Askofu Mkuu
afanye kazi na watu ambao sio sehemu ya
mamlaka ya Dayosisi ya Dar es Salaam.
“Halmashauri Kuu inamwambia kwa kuwa amekuja
na tamko lake bila ya kuwashirikisha,
wamemwambia Dar es Salama kuna askofu mmoja
tu ni Mokiwa.
“Yeye kama Askofu Mkuu hakupaswa kucheza nje
ya Nyumba ya Maaskofu, mimi pia naingia kwenye
Nyumba ya Maaskofu, kuchomoka na kufanya kazi
nje ya taratibu, hii sio sawa.
"Askofu Mkuu ana timu yake ya maofisa ambao
wamemshauri vibaya, na yote yaliyonukuliwa yote
yamekosewa katika kusimamia taasisi, kila taasisi
ina uhuru wa kurekebisha pale palipoharibika
pasipo kuingiliwa.
“Dayosisi ya Dar es Salaam haina mgogoro na mimi
ndio Askofu wake, mgogoro uliopo ni wa
kutengeneza, katika timu yake kuna watu wenye
‘interest maalum’ ambao ni Profesa Palamagamba
Kabudi, yeye ndio mshauri mkuu wa askofu lakini
amekuwa akimpotosha, askofu akikosea na yule ni
mwanasheria aliyebobea na ndiye anayeingiza
kanisa kwenye migogoro iliyobobea.
“Tumewahi kuandikiwa barua na serikali Kanisa letu
ndio vinara wa migogoro, wamekuwa
wakitengeneza mgogoro kati ya waumini na
maaskofu wasielewane, wakubwa waingie kushika
hatamu za uongozi hapa.
“Nina kibali cha kuzungumzia Dayosisi ya Victoria
Nyanza Mwanza, uongozi wa kanisa umeingia pia
na kufanya kazi na makundi, kando ya taratibu,
kugombanisha askofu na watu wanaowangoza na
kusababisha maumivu makubwa, lakini nasema bila
kufuata taratibu yeye akiwa kiongozi mkuu, ni hatari
sana kiongozi anayeacha kuongoza kwa taratibu na
kufuata matakwa yake mwenyewe. "
Ataja majipu 5 ndani ya Kanisa
Askofu Mokiwa alisema kuwa ndani ya Kanisa
hilo, kuna majipu ambayo yamekuwa kiini cha
migogoro kila kukicha na kuchafua taswira nzima
ya kanisa hilo.
“Askofu Mkuu anashauriwa na Mwanasheria
(Profesa Kabudi) anayeheshimiwa na watu wengi,
aliyezalisha wanasheria wengi zaidi katika nchi hii
lakini halitendei haki kanisa, halisaiidi kusimama
sawa sawa, kuliokoa kanisa na mvurugiko,
haonekani mara zote kwa kuwa amejificha nyuma
ya taratibu hizo.
“Mwingine ni askofu Oscar Mnung’a, Makamu
Askofu Mkuu, huyu anakuja kufanya kazi na
makundi Dar ili aje kuwa askofu mkuu, alikuwa
padri wangu na ni askofu wa Newala, naamini watu
wa Mpwapwa na Newala wanawafahamu, kuwa
ndio viongozi wao ndio chanzo cha maumivu
kwenye kanisa hili.
“Mwingine ni Johnson Chinyong’ole ni Katibu
Mkuu, Padri wa Dayosisi ya Morogoro, moyoni
mwake anaamini mimi ndiye niliyebana asiwe
askofu mkuu, nataka kusema Kanisa Anglikana ni
Kanisa kubwa nchi hii, alipaswi kuonekana na dalili
yoyote ya migogoro, lina uwezo wa kufanya mambo
yake ndani bila ya kuvuana nguo kama ilivyo sasa
tena bila ya sababu za msingi.
“Askofu mkuu anafanya kazi na Kanisa la Andrea
Mtakatifu Magomeni, kule kuna mtu anaitwa John
Mhina, yule alikuwa Padri katika dayosisi yangu na
tulimuondolea haki za sakramenti na huduma za
kichungaji mikononi mwake, tulifanya hivyo kwa
sababu ya kukiuka jambo moja tu la utii.
“Tulifanya uhamisho katika Dayosisi ya Dar
akagoma, akatengeneza tuhuma kwa taasisi moja
kubwa ambayo naiheshimu, na sitaki kukosea
ikavurugikiwa kwa sababu ya maneno ya kinywa
changu, taasisi hiyo sina uchafu nao, na sina
uchafu popote.
“Sababu ya Mhina kumuondoa ni kwamba haifai,
mtu ni kuhani wa Mungu halafu anaenda kukopa
benki na kukimbia vielelezo ninavyo, benki
alizokopa ni BOA, Akiba Commercial Bank na
Tanzania Investment ambayo iliwahi kumtoa mpaka
picha zake.
“Mwingine ni Paul Mtweve alikuwa mkuu wa idara
ya Uinjilisti, naye nilimuondoa kwa sababu za
kiuaminifu, kulikuwa na Saccos ambayo
alijikopesha na sasa imefungwa, wamechafua
taswira nzima ya Dar es Salaam na ndio wamekuwa
wakitumika na askofu mkuu, ndio wamekuwa
vinara wa kutengeneza mashaka. Kuthibitisha kuwa
wanafanya kazi na Askofu mkuu, uhamisho wa
Mhina, alipopinga kuhama, askofu Mkuu ‘alisapoti’,
kwangu mimi kwa Dar es Salama sio tena Askofu,
mwaka jana sikukuu ya Matende alisema
amehamina Mpwapwa sasa sijui amebaki huko au
vipi maana hapa sijamuona.
“Nilisali Ubungo siku ya Krismasi, e-mail zilinaswa
ambazo zilikuwa zikisambazwa kwa wanangu wa
Magomeni ambao hawakusali Krismasi kwa sababu
walipewa taarifa kupinduliwa kwangu, hivyo walijua
kutakuwa na mapinduzi.
“Taasisi za dini hazipaswi kufanya kama hivi ni
aibu, waumini wakimbilie wapi wakati wanaamini
Kanisa ndio mahali salama.
“Waumini watulie, kwa jimbo la Dar es Salaam
hawatatusikia katika migogoro yoyote, bado nina
imani na waumini wa Dayosisi hii, tushikane
pamoja, kuifanya kazi ya Mungu.
“Tuna shule, vituo vya watoto yatima, nataka
ninaofanya nao kazi bila njaa, na wale wanaocheza
nje ya zizi, warudi kundini nitawakaribisha,”
alisema.
Mokiwa alifunguliwa mashtaka 10 Machi 2015
ambayo ni kuizuia dayosisi ya Dar es Salaam,
kupeleka michango pasipo maelekezo ya Sinodi
ya Dayosisi ya Dar es Salaam, kuhamasisha
dayosisi kujitoa katika udhamini wa Kanisa la
Anglikana Tanzania (KAT) kwa lengo la
kuifarakanisha dayosisi na Jimbo, kinyume na
katiba ya dayosisi.
Mashitaka mengine ni kufuja mali za kanisa na
kuingia mikataba kiholela yenye viashiria vya
rushwa katika eneo la kanisa la Mtoni Buza na
miradi mingine, kushindwa kutatua migogoro
inayohusu uwekezaji na maadili baina ya dayosisi
na mitaa ya Magomeni ambao kuna mgogoro na
Benki ya DCB, kanisa la Kurasini na mengine.
Askofu huyo pia anadaiwa kushindwa kutatua
migogoro baina ya mapadiri na waumini na
kutunza mali za kanisa katika mtaa wa
Watakatifu wote Temeke na kutelekeza nyumba
ya askofu iliyopo Oysterbay ambako imegeuzwa
kuwa yadi ya kuuza magari.
Pia alilalamikiwa kushitakiwa mahakamani na
Marehemu Christopher Mtikila na watu wengine
watatu kwa kosa la kuwatishia silaha ya moto na
kuwapapasa maungoni mwao bila ridhaa yao
kinyume na maadili ya kikanisa.
Askofu Mokiwa pia analalamikiwa kuanzisha
taasisi ya MEA Foundation iliyomwezesha
kupokea fedha nyingi za wafadhili kwa ajili ya
maendeleo ya dayosisi, lakini fedha zimefujwa na
hesabu za chombo hazikuwahi kukaguliwa.
Tuhuma zingine ni kurejea kwa mchakato wa
mapitio ya katiba mpya na kuvuruga mchakato
wa awali wa maandalizi ya katiba mpya ya
dayosisi kwa kutumia fedha za dayosisi na
kutekelezwa askofu msaidizi dayososi ya
Katanga Kalemi .
Hata hivyo akijibu tuhuma hizo Mokiwa alisema;
Nyumba ya Maskofu Oysterbay
“Ile nyumba haijatekelezwa bali vigae vilikuwa
vinaanguka, nina kijana wangu ambae ana matatizo
mpaka sasa ni mkubwa lakini hasemi vizuri kuna
siku nilimkuta anacheza na nyoka, paa linavuja
mvua zikinyesha, ndio niliamua kuhama na sasa
naishi nyumbani kwangu Mbezi Luisi.
“Kuna fedha Sh milioni 60 ambazo zimetengwa kwa
ajili ya ukarabati wa nyumba hiyo ikikamilika
nitarudi kukaa.
“Silverhok iliyopo Upanga, nyumba haikuwa kwenye
hali nzuri jengo halikua salama, ndio maana
tuliwahamisha na jengo halijatekelezwa kwani
tunataka kulifanya la kisasa kama majengo
mengine yanayozunguka eneo lile la Mindu.
"Fedha za DCB Kuna watu wanaeneza nimekuwa
nikilipwa Shilingi bilioni 6 na DCB, huku ndani mimi
nimewahi kuunda chombo ambacho kinahusisha
DCB Magomeni, wa wawakilishi wa dayosisi, lakini
Magomeni wenyewe ndio wanakimbia vikao, DCB
ndio waliojenga na ndio wanaolipa Kanisa Dayosisi
ya Anglikana.
“Kama ni vita yenye maslahi, fanyeni uchunguzi
mjue anayepokea fedha kutoka DCB ni nani, mtapa
ukweli kuwa ni Magomeni wenyewe, inashangaza
wao ndio wanakula na kushiba lakini ndio
wamekuwa wakipiga kelele na kupotosha watu.
“Kwa mikono yangu niliwaidhinishia Sh milioni 200
za ujenzi wa Kanisa lakini mpaka leo halijajengwa,
mabati yapo pale yamesimama kama kaburi,
hakuna kilichofanyika na hela zimeliwa, waseme
yote kwa ukweli na sio kuweka siasa.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top