DR. JOHN POMBE MAGUFULI NDIYE RAIS MTEULE WA AWAMU YA 5 TANZANIA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi -NEC imemtangaza Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi - CCM, Dokta JOHN POMBE MAGUFULI kuwa mshindi wa Urais kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi NEC Jaji mstaafu DAMIAN LUBUVA amemtangaza Dokta MAGUFULI kuwa amepata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 akifuatiwa na Mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo - CHADEMA aliyepata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97.
Mgombea ANNA ELISHA MGHWIRA wa Chama Cha ACT WAZALENDO amepata kura 98,763 sawa na asilimia 0.65, Mgombea wa ADC CHIEF LUTALOSA YEMBA amepata kura 66,049 sawa na asilimia 0.43, Mgombea HASHIM RUNGWE SPUNDA wa Chama Cha CHAUMMA amepata kura 49,256 sawa na asilimia0.32.
Mgombea KAMBALA JANKEN MALIK wa NRA amepata kura 8,028 sawa na asilimia 0.05, Mgombea LYMO MACMILLIAN wa TLP amepata kura 8,198 sawa na asilimia 0.05 ambapo Mgombea DOVUTWA FAHMI NASORO wa Chama Cha UPDP amepata kura 7,7785 sawa na asilimia 0.05.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu LUBUVA amesema wananchi 23,161,440 waliandikishwa kupiga kura ambapo wananchi 15,589,639 sawa na asilimia 67.31 wamepiga kura.
Jaji Mstaafu LUBUVA amesema kura halali zilikuwa 15,193,862 sawa na asilimia 97.46 huku kura 402248 sawa na asilimia 2.58 zikiwa batili.
Kutangazwa kwa Dokta MAGUFULI kumefuatia uhakiki na majumuisho ya kura zilizotangazwa kutoka majimbo ya uchaguzi 264 nchini kote kabla ya kumtangaza mshindi wa ngazi hiyo ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo mawakala wa vyama SABA vya siasa walisaini hati ya kukubali matokeo hayo ya urais.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuwa hafla ya kukabidhi vyeti vya ushindi kwa washindi itafanyika tar 30/10/2015 Saa NNE Asubuhi katika Ukumbi wa DIAMOND Jijini DSM.
0 comments :
Post a Comment