Hii ndio mishahara ya vigogo wa mashirika ya umma.soma zaid.
Ni mashirika ya umma wanayolipana mishara
minono
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli,
kusema kwamba Serikali inafanya marekebisho
ya viwango vya mishahara kwa watendaji wa
mashirika ya umma, hatimaye
imebainika viwango mbalimbali vya mishahara
wanavyolipana vigogo katika mashirika hao.
Katika mashirika hayo, baadhi ya vigogo hulipana
viwango vikubwa vya mshahara, ambapo kigogo
mmoja hulipwa Sh Sh milioni 36 kwa mwezi na
wengine hufikia kiwango cha Sh milioni 40 kama
alivyoeleza Rais Magufuli juzi.
Akizungumza na wananchi wa Chato, Dk.
Magufuli alisema watu hao wanaolipwa kiwango
kikubwa cha mishahara wamekuwa wakiishi
kama malaika na sasa ni lazima washushwe ili
waishi kama shetani.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Serikali
kiliambia MTANZANIA kuwa, ulipwaji wa viwango
vikubwa kwa watendaji wa mashirika ya umma
umetengeneza tabaka kubwa la wenyenacho na
wasionacho.
Uamuzi huo wa Rais Magufuli, umetajwa kuwa
huwenda ukaleta heshima na utu kwa
Watanzania, kwani baadhi ya taasisi na mashirika
ya umma watendaji wake wa ngazi za juu
wameonekana kulipana mishahara ya kufuru.
“Kuna taasisi watendaji wa ngazi za juu
wamekuwa wakilipwa mishahara minono zaidi
ambapo kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
hulipana Shilingi milioni 24 kwa mwezi pamoja na
marupurupu,” kilisema chanzo chetu.
Taasisi nyingine zinazolipwa kiwango kikubwa
kwa watendaji wake ni Shirika la Taifa la Hifadhi
ya Jamii (NSSF), Sh milioni 36, Shirika la Umeme
nchini (Tanesco), Sh milioni 36.
Mashirika mengine ambayo yanaongoza kwa
kulipana kiwango kikubwa ni Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC), Sh milioni 36 na Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)
ambapo watendaji wa juu hulipwa Sh milioni 36.
Mbali na taasisi hizo pia timu ya waatalamu ya
Rais Magufuli inaangalia taasisi kama za Mpango
wa Matokeo Makubwa sasa (BRN), Mamlaka ya
Hifadhi za Taifa (Tanapa), Ngorongoro, Mamlaka
ya Bandari Tanzania (TPA), Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH).
Taasisi nyingine ni Benki ya Rasilimali Tanzania
(TIB), Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC),
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Bodi
ya Bima ya Amana, Shirika la Maendeleo la Taifa
(NDC) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
Hatua ya Rais Magufuli kupitisha panga na
kuweka uwiyano wa mishahara kwa watendaji wa
taasisi hizo unaelezwa kuwa utaisaidia uwajibikaji
na usawa kwa watendaji.
“Kwa mfano kwa sasa zipo taasisi nyingine
hupandishiana mishara kila wakati, unakuta
mfagiaji analipwa hadi Shilingi milioni Moja,
wakati katika sekta nyingine kama walimu
wanaambulia Shilingi 400,000 kabla ya makato.
“Hatuwezi kujenga Taifa la wenye nacho na
wasio nacho kwa mfumu huu na ikiwa Serikali
italitekeleza hili kama Rais Magufuli alivyoamua
ni wazi sasa tutapiga hatua mbele zaidi,” alisema
mtoa habari huyo.
Azivaa bodi
Kiongozi huyo wa nchi, alishangazwa na baadhi
ya bodi za wakurugenzi kushindwa kufanyakazi
zao kwa mujibu wa sheria na badala yake
wamekuwa na kazi ya kupandisha mishahara kwa
viongozi.
Alisema kutokana na hali hiyo anashangazwa na
bodi hizo kila kukicha zimekuwa zikifanya kazi ya
kupandisha mishahara pamoja na kufanya vikao
nje ya nchi.
Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli ameunda
timu ya wataalamu ambayo imeanza kufanya
kazi ya upunguzaji wa mishahara mikubwa kwa
watendaji wakuu wa mashirika ya umma.
“Tena hawa wakurugenzi ndio wanaongoza kwa
kulipwa fedha nyingi na hata kwenda kufanya
vikao ulaya, ninasema hapa kwamba suala hili
litaanza kushughulikiwa katika bajeti ya hivi
karibuni,” alisema Rais Magufuli.
Juzi akiwa wilayani Chato, Rais Magufuli, alisema
wapo watendaji wanalipwa Sh milioni 40 kwa
mwezi na wengine wanalipwa Sh 300,000.
Alisema tayari ameunda timu ya wataalamu
ambayo inafanya kazi ya kupunguza mishahara
hiyo na kufikia Sh milioni 15 kwa mwezi ili
asipatikane Mtanzania anayelipwa zaidi ya
kiwango hicho.
“Tunafanya hivi ili nyingine tuziteremshe kwa
watu wa chini na yule atakayeng’ang’ania
kwamba lazima alipwe Sh milioni 40 aache kazi
tuweke mtu mwingine,” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo Rais Magufuli, alishangazwa na watu
namna wanavyolipana kile alichokiita mishahara
ya ajabu kwa kushirikiana na bodi ambazo wakati
mwingine huzihonga fedha ili zipandishe
mishahara yao.
“Kuna watu wanaishi kuliko hata malaika lazima
tuwashushe waishi kama shetani,” alisema Rais
Magufuli.
Pamoja na hali hiyo kiongozi huyo wa nchi
alianika madudu aliyoyakuta ndani ya Serikali
ikiwemo mmoja wa mfanyakazi wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), kulipwa mishahara ya
watu 17 na kuagiza mfanyakazi huyo afikishwe
mahakamani.
Pamoja na hali hiyo alisema wapo watumishi
wanaolipwa mishahara mikubwa ambayo inafikia
hadi Sh milioni 40 kwa mwezi, ambayo sasa
itapunguzwa na kuweka kima cha juu cha
mshahara usiozidi Sh milioni 15.
Dk. Magufuli alisema Serikali yake imejiandaa
kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa
kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi
asilimia 10 au 9 (single digit) kuanzia bajeti
ijayo.
“Kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa, uhakiki
mdogo uliofanywa hivi karibuni, umebaini
wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa
shilingi bilioni 1 na milioni 800 na kwamba ni
matarajio kuwa uhakiki unaofanywa nchi nzima
utaisaidia Serikali kubaini wafanyakazi hewa
wengi zaidi na kunusuru fedha nyingi zaidi za
Watanzania.
Alisema anashangazwa na hatua ya baadhi ya
watu kuishi kama malaika huku wengine wakiishi
kama masheteni, jambo ambalo alisema halina
nafasi katika Serikali yake.
“Nyiye mliokuwa mnaishi kama malaika, sasa
zamu yenu kuishi kama mashetani,” alisema Dk.
Magufuli huku akishangiliwa na umati wa
wananchi waliohudhuria katika mkutano huo.chanzo mtanzania
0 comments :
Post a Comment