Soma simulizi ya kusisimua ya ERICK SHIGONGO.soma zaid
Kuna jamaa alikuwa masikini sana mkoani
Kigoma. Alikuwa akiishi na mke wake huku
wakiwa na mtoto wao mdogo. Kutokana na
maisha kuwa magumu, akaamua kuwa mkulima.
Akalima na kulima lakini hakufanikiwa. Akakata
tamaa hivyo kuamua kujiingiza kwenye uuzaji wa
mafuta ya mawese.
Alihisi kwamba mambo yangebadilika lakini baada
ya yeye kuanza biashara hiyo, soko la mafuta ya
mawese likashuka kwa kasi ya ajabu hivyo
hakufanikiwa. Maisha yaliendelea kumtesa,
umasikini ulimtafuna yeye na familia yake.
Kikafika kipindi akachoka, hakutaka kuona
akiteseka na familia yake hivyo kumwambia
kwamba ni lazima aondoke na kwenda nchini
Kongo kuchimba dhahabu, labda bahati yake
ilikuwa huko. Mkewe alipinga lakini akamshawishi
kwa kipindi kirefu na hatimaye akakubaliana
naye.
Baada ya kutafuta fedha za kuungaunga,
akaelekea huko. Alipofika, alikaa kwa miaka saba
ndipo akafanikiwa kupata dhahabu kubwa, nzito
ambayo aliamua kuibeba katika begi lake na
kurudi Kigoma kwa meli.
Ndani ya meli kulikuwa na watu wengi, hasa
Wazungu ambao walikwenda huko kufanya utalii.
Wakati meli ikiwa imefika katikati ya ziwa
Tanganyika, ikaanza kuzama. Watu walipiga
kelele sana, kwa jamaa hakukuwa na tatizo
kwani alijua sana kuogelea, hivyo akawa anapiga
mbizi na wakati mwingine kuelea juu ya maji.
Wakati watu wengi wamekufa, akasikia sauti ya
msichana mmoja mdogo akilia, alikuwa mtoto wa
Kizungu, wa kike aliyekuwa akiomba msaada.
Jamaa alimuona mtoto yule wa miaka kumi na
tano, akaamua kumfuata na kumbeba, kitu cha
ajabu kabisa ambacho hakujua ilikuwaje, akaanza
kuzama kutokana na uzito.
Kulikuwa na mambo mawili makubwa, alitakiwa
kufanya moja ili anusurike. La kwanza lilikuwa ni
kumuacha mtoto yule afe na yeye aondoke zake,
au kuiacha dhahabu ile ili amnusuru yule mtoto.
Ulikuwa mtihani mkubwa mno kwake. Aliondoka
nyumbani miaka saba iliyopita, alimwambia
mkewe kwamba anakwenda kutafuta utajiri nchini
Kongo.
Alifanikiwa kwa kupata dhahabu kubwa ambayo
aliamini ingemfanya kuwa bilionea. Sasa iweje
aiache dhahabu kwa ajili ya mtoto asiyemjua
ambaye wazazi wake walikufa? Moyo wake
ukagawanyika, upande mmoja ukamwambia
aachane na mtoto kwani hata angemuokoa,
angeishi naye wapi?
Angemsaidia nini na wakati hawakujuana?
Ukamkumbusha maisha aliyokuwa amepitia,
maisha ya kimasikini, yaliyomuumiza, yakamletea
picha ya mkewe na mtoto wake walivyokuwa
wakiteseka kwa kupigwa na umasikini.
Upande mwingine ukamwambia lilikuwa jambo
jema kumsaidia mtoto yule. Utajiri hauna kitu
mbele ya utu. Ilikuwa ni lazima amsaidie mtoto
yule kwani hata kama angepata fedha, bado
angekufa baadaye, ni wangapi walikuwa na fedha
ila wamekufa na kuziacha fedha hizo?
Moyo wake ukawa mgumu kufanya maamuzi
lakini mwisho wa siku akaitupa dhahabu kubwa
majini. Moyo ulimuuma sana lakini hakuwa na
jinsi. Akambeba msichana yule wa Kizungu na
kuanza kuogelea naye, saa moja mbele,
wakaokolewa na meli nyingine.
Mtoto yule akasaidiwa na Umoja wa Mataifa
kurudishwa Marekani alipokuwa akiishi huku
nyuma jamaa alipofika nyumbani na
kumuhadithia mkewe kilichotokea, alimtukana
sana na kumuona mjinga, iweje atupe dhahabu
na wakati alipoteza miaka saba kuitafuta?
Majirani wakamcheka, wakamdharau na mkewe
akaamua kuondoka kurudi kwao kwani
asingeweza kukaa na mwanaume mpumbavu
kama yeye.
Jamaa akaanza upya, maisha yakaanza kumpiga
tena. Alilia sana, alichekwa kila kona. Alitamani
kurudi Kongo kutafuta tena dhahabu lakini
hakuwa na fedha. Akawa ombaomba, kila kona
mkoani Kigoma alikuwa akipita kuomba, kuanzia
Ujiji, Mwanga, Mwembetogwa, Mji Mwema,
Bangwe na kila sehemu alikuwa akiombaomba.
Baada ya miaka mitano, wakati akiwa amepigwa
sana na maisha, ghafla akamuona msichana wa
Kizungu akija mbele yake. Hakumjua, msichana
yule alipiga hatua mpaka kule nyumbani kwake
alipokuwa. Alipofika, akamsalimia huku akiwa na
Mkalimani wake. Akamuuliza kama alimkumbuka,
jamaa akasema hamkumbuki ndipo yule
msichana akasema kwamba yeye ndiye yule binti
wa miaka kumi na tano aliyekuwa amemuokoa
kipindi cha nyuma.
Jamaa alifurahi kumuona, akamkumbatia.
Msichana yule akamwambia kwamba alikuwa
akimkumbuka kila siku kwa wema
aliomuonyeshea. Kipindi hicho, msichana huyo
alifanikiwa sana, alikuwa mfanyabiashara
mkubwa Marekani, mwenye kampuni nyingi kwani
wazazi wake walimuachia utajiri mkubwa.
Jamaa akamwambia kila kitu kilichotokea katika
miaka mitano ya mateso. Msichana yule
akahuzunika sana, alichokifanya ni kumwambia
jamaa kwamba alikuja Kigoma kwa ajili ya
kumchukua yeye na familia yake kwenda kuishi
nchini Marekani kama fadhila kwake. Ila kwa
sababu mkewe aliondoka na mtoto na hakujua
walipokuwa, basi aondoke naye tu.
Jamaa akafurahi. Huo ndiyo ukawa mwisho wa
kuishi Tanzania. Akaondoka na kuelekea
Marekani, kama alivyokuwa msichana yule, naye
akawa mfanyabiashara mkubwa. Ameoa huko na
maisha yake yanaendelea kama kawaida.
FUNZO: Unapotakiwa kutenda wema, wewe tena
pasipo kujali itakugharimu kiasi gani.
Inawezekana jamaa angeona dhahabu ni mali,
angekufa njiani au ingepotea. Kwa kumsaidia
msichana yule, Mungu akaileta meli. Kwa
kumuokoa msichana yule, leo hii yupo nchini
Marekani akila maisha.
Alisubiri kwa miaka mitano, kama kukata tamaa
angekata mapema sana. Msichana hakumsahau,
aliendelea kumkumbuka, aliukumbuka wema
wake na kurudi Tanzania kutoa fadhila.
E.J SHIGONGO.
0 comments :
Post a Comment