Kanga moja kiunoni ------mbengembeng--21.soma zaid
Irene M. NDAUK
ILIPOISHIA IJUMAA WIKIENDA:
Hamadi! Sura ya baba Mei hii hapa! Mzee Hewa
akashtuka kwani wakati mlango unafunguliwa
alishaweka sura ya tabasamu akijua atamwona
mama Mei. Kwa hiyo alipokutana na sura ya
baba Mei ghafla, alikunja sura ghafla…
SASA TAMBAA NAYO MWENYEWE…
“HAA! Hujambo bwana mdogo?” mzee Hewa
alisalimia huku uso wake ukiwa haujakaa
sawasawa…
“Sijambo mzee, shikamoo…”
“Marhaba, za safari bwana?”
“Ni njema mzee wangu…vipi, nikusaidie nini?”
Mzee huyo alibabaika kwa mbali hali
iliyomshangaza sana baba Mei…
“Nilitaka kujua kama kuna gesi maana jiko langu
la gesi lime…aaah! Nataka kuazima kibiriti kwa
mama! Oooh! Nimepitiwa, kuna maji ya baridi ya
moto? Ha! Mimi naye kwa kusahausahau sijambo
kidogo…naulizia milango kama mmefunga.”
Baba Mei alibaki akimtumbulia macho tu huku
akijiuliza ni kitu gani kinamfanya mzee huyo
ababaike kusema kama kweli aligonga mlango
akiwa na shida ndani kwake…
“Mzee wangu kwani kuna nini, sikuelewi…”
“Haa! Nilikosea kijana kugonga kwako, nilikusudia
mlango ule,” alisema mzee Hewa huku akiondoka
kurudi kwake.
Ile baba Mei anageuka tu, mama Mei anatoka
chumbani…
“Vipi, ni nani?” alimuuliza mume wake…
“Ah! Mimi sijamwelewa mzee wako…nadhani
kuna kitu zaidi ya ujio wake,” alijibu baba Mei
huku akiingia chumbani moja kwa moja.
Mama Mei naye alifuata na kumkuta mume wake
akiwa amelala akiangalia juu kwa mawazo…
“Yule mzee asitake kuleta longolongo, kwa
vyovyote vile alimfuata mke wangu. Inaonekana
hakujua kama mimi nimerudi,” alisema moyoni
baba Mei…
“Baba Mei kwani kasemaje?”
“Nani?”
“Mzee mwenye nyumba?”
“Ah! Mimi sijamwelewa hata kidogo. Kwanza
nahisi shida yake kubwa ni wewe ila mimi
niliingilia kwa bahati mbaya tu…”
“Kwani amesemaje?”
“Hakuna kilichoeleweka… alipokutana macho na
mimi, kwanza akashtuka sana. baada ya salamu
akaniuliza habari za safari nikamwambia nzuri,
akasema nilitaka kujua kama kuna gesi maana
jiko langu la gesi lime…akasita, kisha akasema
nataka kuazima kibiriti kwa mama! Akaacha,
akasema oooh! Nimepitiwa, kuna maji ya baridi
ya moto? Pia akaacha akasema naulizia milango
kama mmefunga…”
“Khaa! Ndiyo nini sasa?” aliuliza mama Mei huku
akionesha kushangaa. Lakini moyoni alijua moja
kwa moja kwamba, mzee huyo alikuwa na shida
na yeye ila hakujua kama mume wake
alisharejea…
“Mimi sijui ndiyo nini!” alisema kwa mkato baba
Mei na kugeukia kwingine hali iliyompa ishara
mkewe kwamba, kuna jambo mumewe
amejifunza kuhusu ujio wa mzee mwenye
nyumba.
Mama Mei alibaki kimya. Alitamani sana
kumsemesha mume wake lakini angemsemesha
nini wakati mumewe amehisi jambo?
Kumsemesha kungemfanya ajulikane kwa undani
zaidi.
Usiku wa manane, baba Mei alishtuka na kujikuta
akimuwaza mzee Hewa, lakini pia akapata na
mawazo kuhusu ule ukaribu aliouona kati ya
mkewe na mpangaji mwenzao, Mfaume…
“Inaonekana kuna kitu kilikuwa kikiendelea wakati
mimi sipo. Mbona huyu mke wangu kama
amekuwa mwenyeji sana na hawa watu?”
alijiuliza.
Kitabia, baba Mei si mtu wa kukurupuka! Mambo
yake mengi hupenda kuyafanya kwa polepole na
utaratibu huku akihakikisha kama ni jambo
analipata kwa ukamilifu akitumia mahesabu ya
mwaka!
Alijichanga akili, akaamua kuweka mtego wa
makusudi ili kujua kama kweli mke wake ana
jambo la ziada au la, ni mawazo yake tu!
***
Kulipokucha, mama Mei alitoka kitandani na
kuendelea na kazi nyingine za kila siku za
nyumbani kwake.
Asubuhi hiyo, alikuwa amekunja sura vibaya
sana. hakumchangamkia mtu yeyote ndani ya
nyumba ile maana alijua wanataka kumweka
pabaya!
Baba Mei alipoamka, alikwenda kuoga na kurudi
ndani. Alivaa, akaenda sebuleni kunywa chai!
Hapo alimwita mkewe…
“Abee…”
“Njoo mara moja.”
Mama Mei alipofika alikaa akimwangalia mume
wake kwa macho yaliyojaa wasiwasi…
“Mimi jioni leo nasafiri tena, nakwenda Tanga
halafu Arusha,” alisema baba Mei kisha
akamwangalia mkewe ambaye aliachia sura ya
tabasamu kutoka ile ya wasiwasi…
“He! Yaani unaunga mume wangu?”
“Ndiyo kazi sasa mke wangu, nitafanyaje?”
“Kweli lakini,” alisema mama Mei huku akiachia
tabasamu pana…
“Kwa hiyo nilitaka ulijue hilo tu mke wangu
maana nikiondoka nikirudi jioni ni safari,” alisema
baba Mei na kuendelea kunywa chai…
“Sawa mume wangu, safari njema,” alisema
mama Mei naye huku akiondoka.
Baba Mei alimwangalia mkewe akatingisha
kichwa huku moyoni akisema…
Je, nini kilitokea hapo? Usikose kusoma Gazeti
la Ijumaa, Ijumaa ijayo. Pia soma chombezo
langu lingine kwenye Gazeti la Uwazi,
0 comments :
Post a Comment