Breaking News
Loading...

Advert

Tuesday, February 7, 2017

Simulizi ya ERIC SHIGONDO DIMBWI LADAMU sehemu ya 15.soma zaid


ERIC SHIGONGO
DIMBWI LA DAMU-15
Tayari Manjit alishaingia �mikononi mwa polisi
na �alikuwa ndani ya gari akipelekwa kituoni,
hiyo ilitokea baada ya kumweleza Patrick ukweli
kuwa asingeweza kumlipa pesa alizokuwa
akimdai,Victoria aliumia sana moyoni mwake
wakati Manjit akiondolewa ndani ya ofisi ya
Patrick huku akiliita jina lake, alishindwa
angemsaidia vipi Manjit mtu pekee aliyekuwa
akimtegemea kwa wakati huo.
Walitoka ofisini Patrick akiwa amemshika mkono
Victoria na kumuongoza hadi mahali lilipokuwa
gari lake la kifahari aina ya Potsche, na kuingia
ndani, Patrick alikaa kwenye usukani na Victoria
alikaa kushoto kwake, ilikuwa ni safari kwenda
nyumbani kwa tajiri Abdulwakil ambako Victoria
alikuwa akipelekwa kuongea na tajiri huyo
aliyemiliki visima vingi vya mafuta ili ajaribu
kumshawishi asimfunge Manjit kwani ndiye
alikuwa tegemeo lake maishani.
“Akiniona katika hali hii ya upofu ni lazima
atabadili nia yake ya kumfunga Manjit, Mungu
yupo pamoja na mimi ninaamini atanihurumia!”
Aliwaza Victoria wakati gari likipita kwenye mitaa
ya katikati ya jiji la Baghdad kuelekea nyumbani
kwa tajiri Abdulwakil kilometa kumi na tano nje
ya jiji.
“Hivi baba yangu atakubali kweli? Sina uhakika
anachotaka yeye ni pesa na kama hakuna pesa
lazima Manjit atafungwa tu!”
“Mwanangu niache nikaongee naye akikataa basi
lakini nitakuwa nimejaribu!”
“Sawa mama!”
Gari lilizidi kwenda kwa kasi na dakika kumi na
tano baadaye liliacha barabara na kukata kona
kuingia kulia likipita chini ya miti mirefu, mbele
zaidi kama nusu kilometa lilikata tena kushoto na
kuzidi kutokomea ndani! Hatua kama mia mbili
mbele Victoria alisikia honi ikipigwa na mlio wa
geti likifunguliwa ulisikika, akafahamu walikuwa
wamefika mahali walipokuwa wakienda.
“Asalam alekum!”
“Aleikum salam!”
Alisikia maneno hayo kila walivyozidi kusonga
mbele hatimaye gari likasimama kabisa na
Patrick alifungua mlango na kuzunguka hadi
upande wa pili ambako pia alifungua mlango na
kumsaidia Victoria kushuka.
“Tumefika!”
“Kumbe sio mbali?”
“Kwa kweli sio mbali sana!”
Patrick akiwa amemshika mkono Victoria
waliongozana na kuanza kupandisha ngazi
taratibu, aligundua walikuwa wakiingia ndani ya
nyumba, kila mahali walikopita salamu zilisikika
na milango ilifunguliwa na wakaingia hadi ndani
ambako Victoria alisaidiwa kuketi kitini.
“Karibu mama hapa ndio nyumbani kwetu!”
“Ahsante sana mwanangu, kikubwa naomba
unisaidie nikutane na baba yako!”
“Basi nisubiri hapa nikaongee naye” Alisema
Patrick, alionekana kumwonea huruma sana
Victoria lakini hakuwa na uwezo wa kumsaidia
kwa sababu mwenye amri alikuwa ni baba yake
mzazi.
“Haina matatizo!” Aliitikia Victoria na baadaye
akasikia mlio wa viatu ukiondoka mahali alipokaa.
Alisubiri kwa muda mrefu mno bila Patrick
kurejea, alishindwa kuelewa ni kitu gani
kilichokuwa kikiongelewa huko ndani! Hofu yake
kubwa ilikuwa ni tajiri Abdulwakil kukataa
kuonana naye alimwomba Mungu wake hilo
lisitokee. Mawazo yake yote wakati akisubiri
yalikuwa juu ya Manjit ambaye alikuwa polisi,
hakujua ni kitu gani wangekuwa wamemtenda!
Alizidi kumwomba Mungu amwepushe Manjit na
mabaya yote, hakuwa tayari kushuhudia Manjit
akipatwa na tatizo kwani maisha bila yeye
yasingewezekana, alikuwa tayari kufa pamoja
naye.
Baadaye akiwa sebuleni alianza kusikia
minong’ono kutoka upande wa pili, ilikuwa ni
sauti nzito ya kizee ikifoka! Hakuelewa ni nini
kilichokuwa kikiongelewa kwa sababu maongezi
yalifanyika katika lugha ya Kiarabu.
Kadri dakika zilivyozidi kwenda ndivyo sauti ya
mzee akifoka ilivyozidi kuongezeka na kukikaribia
chumba alichokuwa amekaa, hofu kubwa ilimpata
moyoni mwake akijua kitu kibaya kilikuwa
kikimfuata! Alianza kulia akimwomba Mungu
abadilishe mawazo ya wabaya wake.
“Ee Mungu wangu naomba unisai........!” Alisema
Victoria lakini kabla hajaimalizia sentensi yake
mlango ulifunguliwa na nyayo za watu wengi
zilisikika zikiingia, alikaa kimya akisubiri sauti ya
Patrick iongee lakini badala yake alisikia sauti
nzito ya mzee ikifoka.
“Yuko wapi huyo? Hawa watu wanafikiri sisi
tunafanya mchezo na biashara, ikibidi hata huyu
mama tutamfunga pamoja na Manjit!” Alifoka
mzee huyo, sauti yake pekee ilitosha kumtisha
Victoria.
Victoria aliposikia kauli hiyo aliinamisha kichwa
chake na kuuficha uso wake katikati ya miguu
yake miwili, kwa maneno yaliyosemwa na mzee
huyo alijua taabu kubwa ilikuwa inakuja! Aliumia
sana moyoni mwake, alifikiri shida zilikuwa
zimekwisha katika maisha yake kumbe haikuwa
hivyo alitakiwa kupambana na matatizo mengine
tena.
“Hebu mleteni hapa!” Aliamrisha mzee huyo na
Victoria alibebwa juujuu na kupelekwa moja kwa
moja hadi mahali mzee huyo alipokaa.
“Nisamehe sana mzee, naomba unisikilize
kwanza ninachotaka kusema!”
“Onyesha uso wako kwanini unaficha sura? Hebu
mnyanyueni sura yake niione ingawa ukitaka
kumuua nyani usimwangalie usoni!” Alisema tajiri
Abdulwakil na vijana kama watatu walimshika
Victoria shingoni na kuanza kukinyanyua kichwa
chake.
“Khaa! Victoria ni wewe?” Tajiri Abdulwakil
alisikika akipiga kelele.
Victoria alishangaa kusikia mtu aliyemhofia
akimwita kwa jina, hakuwa maarufu kiasi cha
kujulikana kwa tajiri Abdulwakil!
“Wewe ni nani unayeniita jina?”
Tajiri Abdulwakil hakujibu kitu kwa mshtuko
alioupata alilegea na kuanguka moja kwa moja
sakafuni! Ikawa hekaheka ndani ya chumba, watu
wote hawakuelewa ni nini kimempata ikabidi kwa
haraka haraka abebwe na kutolewa moja kwa
moja hadi nje ambako alipakiwa ndani ya gari na
kukimbizwa hospitali! Hakuna mtu aliyeelewa
kilichotokea, kilibaki ni kitendawili.
“Au yule bibi ni mchawi nini?” Aliuliza Patrick
wakiwa ndani ya gari kuelekea hospitali.
“Kwanini unafikiri hivyo Patrick?”
“Maana amening’ang’ania sana nimlete kwa baba
sasa baada tu ya baba kumwona ameanguka na
kupoteza fahamu. Kama baba akifa kwa hakika
nitamuua huyu bibi kizee! Hawezi kuniulia baba
yangu hivi hivi nikamwacha hai” Aliendelea
kusema Patrick huku machozi yakimtoka.
Walipofika hospitali walipokelewa na tajiri
Abdulwakil akiwa hajitambui alikimbizwa moja
kwa moja hadi chumba cha wagonjwa mahututi,
iligundulika baadaye kuwa mmoja wa mishipa
yake katika ubongo ulipasuka sababu ya mshtuko
mkubwa alioupata. Jambo hilo lilimfanya Patrick
aamini Victoria alikuwa na majini na alimpiga
baba yake na moja ya majini yake.
“Nitamuua! Hakyanani nitamuua! Nikirudi
nyumbani tu lazima afe na atafukiwa ardhini
hakuna mtu atakayejua”
**************
Kwa sababu ya kuchanganyikiwa na tukio
lililotokea Patrick alimsahau Victoria ndani ya
nyumba yao na kuondoka mbio kwenda hospitali,
alibaki sebuleni akiwa katika dimbwi la mawazo
na maswali yasiyokuwa na majibu, alishindwa
kuelewa ni nani aliyemwita kwa jina, aliamini
hapakuwa na mtu yeyote aliyemfahamu katika
nchi ya Iran.
Alivuta kumbukumbu zake kwa muda akijaribu
angalau kuikumbuka sauti aliyoisikia lakini
hakupata jibu na kilichomchanganya zaidi ni
kitendo cha kumsikia Patrick akimtupia lawama
juu ya matatizo yaliyompata baba yake! Aliogopa
na kuamini lazima Patrick angemfanyia kitu.
Ni wasiwasi huo ndio uliomfanya atoke taratibu
sebuleni na kutembea hadi nje akishika ukuta,
nyumba nzima ilikuwa kimya iliashiria watu wote
hawakuwepo, aliamini wote walimkimbiza tajiri
Abdulwakil hospitali.
Nyumba ya tajiri Abdulwakil ililindwa kila upande,
ilikuwa si rahisi kutoka wala kuingia ndani ya
nyumba hiyo bila kuonekana lakini kwa tukio
lililotokea siku hiyo, walinzi wote walikusanyika
sehemu moja na kuanza kujadili juu ya
kilichompata tajiri wao.
“Sijui kapatwa na nini?”
“Hata mimi sifahamu, nimeona tu akitolewa ndani
na kupakiwa ndani ya gari na kwa haraka gari
likaanza kuondoka!”
“Labda mama yumo ndani tumuulize?”
“Hata yeye hayupo amekwenda hospitali!”
“Atapona kweli mzee?”
“Kwa hali niliyomwona nayo kwa kweli nina
wasiwasi!”
Wakati maongezi hayo yakiendelea Victoria
alikuwa akiupapasa ukuta kwa kuuzunguka
akitafuta mahali pa kutokea, alikuwa ameamua
kutoroka kwenda mahali kusikojulikana, mwili
wake ulihisi mabaya! Alijua kama Patrick
angerudi kutoka hospitali na kumkuta ni lazima
angemdhuru na hata kumuua kabisa, Victoria
hakuwa tayari kwa hilo.
Alipapasa kwa dakika ishirini nzima ndipo
akafanikiwa kulifikia lango, kubwa lilikuwa
limefungwa lakini alipopapasa pembeni
alifanikiwa kugusa kitu kama komeo, alipokishika
na kujaribu kukifungua na kisha kuvuta
alishangaa kuona lango dogo likifunguka!
Akamshukuru Mungu na kwa taratibu pamoja na
uzee wake alinyata na kutoka nje bila kuonekana
na mtu yeyote.
Sababu ya upofu alisimama bila kujua aelekee
wapi, aliusikiliza moyo wake kwa muda na
akakumbuka maneno aliyoambiwa kanisani miaka
mingi akiwa mtoto mdogo kuwa Mkono wa kulia
ulikuwa mkono wa Kuume ambao uliaminika
kuwa na baraka! Bila hata kujadili mara mbili
Victoria alikata kulia akachuchuma na kuanza
kutambaa akielekea vichakani bila kujua mahali
alikokuwa akielekea.
Kwa saa nzima alitambaa ardhini akipita katikati
ya nyasi zilizomuwasha mwili mzima, hakujali
kwa sababu alishaamua kujiokoa, machozi
yaliendelea kumtoka sababu ya Manjit aliyekuwa
polisi! Kwa mara nyingine alikuwa
ametenganishwa na mtu aliyempenda na
aliyekuwa msaada pekee kwake!Kumbukumbu
zake zilimrejesha tena kwa kaka yake Nicholaus.
“Yaani kila mtu anayejitolea kunisaidia
anaondolewa kwangu! Wa kwanza alikuwa
Nicholaus, akaja Leah, baadaye Manjit lakini hata
yeye wameninyang’anya! Nitaishije mimi
Victoria? Ni heri kufa kuliko mateso haya!”
Aliwaza akizidi kutambaa kwenda mbele zaidi
katikati ya vichaka.
Mpaka masaa matatu baadaye alikuwa bado
akitambaa porini, alikuwa bado hajaonekana wala
kukutana na mtu yeyote! Alimshukuru Mungu
kwa hilo mbele zaidi alichoka na kuamua kulala
chali ardhini na kuamua kuifungua ncha moja ya
nguo aliyojifunga na kutoa kipande cha noti
walichogawana na kaka yake, alikuwa bado
akikitunza! Hakuwa tayari kukipoteza kwake
ilikuwa ni bora apotee yeye lakini si kipande
hicho cha noti alichokichukulia kama kaka yake.
“Hivi kweli ipo siku nitakutana na Nicholaus na
kuiunganisha noti yetu?” Aliwaza Victoria akiwa
amelala chali ardhini, alikuwa amechoka hoi bin
taaban na njaa ilimsumbua, si njaa tu kulikuwa
na mbu wengi waliomuuma kila sehemu ya mwili
wake, ingawa alikuwa kipofu hali ilimuonyesha
kuwa tayari usiku ulishaingia.
Hakuwa na matumaini ya kumwona Manjit tena!
*************
Taarifa za tajiri Abdulwakil kuanguka ghafla
nyumbani kwake baada ya kumwona mwanamke
mzee zilitapakaa kila sehemu ya mji wa
Baghdad! Watu wengi walifurika hospitali
kushuhudia kilichompata mtu waliyeamini alikuwa
tajiri kuliko wote nchini humo.
“Ni jini!”
“Kweli eh?”
“Hakuna kitu kingine! Si ajabu maadui zake
walimtuma bibi kizee nyumbani kwake wakiwa
wamemvalisha jini chinjachinja!”
“Lakini kweli inawezekana!”
Hayo ndiyo yalikuwa maneno ya kila mtu aliyefika
hospitali, hawakuruhusiwa kumwona mgonjwa
watu wote waliongea na Patrick na kumpa pole
na alivyowasimulia yaliyotokea wote waliamini
bibi alitumwa.
“Huyo bibi yuko wapi?” Aliuliza mmoja wa
wafanyakazi kwenye visima vilivyomilikiwa na
tajiri Abdulwakil.
“Tulimwacha nyumbani!”
“Kwa hiyo atakuwa bado yuko nyumbani kwenu?”
“Naamini hivyo!”
“Jamaniee!” Alipiga kelele mfanyakazi huyo na
wafanyakazi zaidi ya mia tatu waliokusanyika
walikaa kimya kumsikiliza yeye, alikuwa ni
kiongozi wao katika visima vya mafuta.
“Ni lazima huyu bibi tukamuue, hawezi
kumuumiza tajiri yetu na ushirikina au
mnasemaje?”
“Sawaaaaaaaaa!”Wafanyakazi wote waliitikia.
Kama walioamrishwa waliingia ndani ya magari
yaliyokuja nayo kutoka kwenye visima vya mafuta
na kwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa
tajiri Abdulwakil kwa lengo la kwenda kumkamata
Victoria na kumuulia mbali. Walipokelewa na
walinzi na walipomuulizia bibi walinzi hawakuwa
na jibu kwa sababu hawakutaarifiwa kuwa
kulikuwa na mtu aliyebaki ndani ya nyumba!
“Ingieni muangalie!”
Kiongozi wa wafanyakazi hao na wenzake wawili
waliingia hadi sebuleni na kuanza kumsaka
Victoria bila mafanikio, walinyanyua hadi viti na
meza na kumwangalia chini yake lakini bado
hakupatikana.
Walitoka nje na kuwataarifu wenzao juu ya
kutoonekana kwa mtu waliyekuwa wakimtafuta
ndani ya nyumba, waliamua kuacha ili wafanye
msako asubuhi iliyofuata, baadaye Patrick alirudi
kutoka hospitali na kuungana nao! Yeye ndiye
aliwajaza jazba zaidi wafanyakazi wake pale
alipowaeleza wazi kuwa mwanamke
aliyemsababisha baba yake matatizo alistahili
kufa.
Wafanyakazi walilala nje ya nyumba ya akina
Patrick na asubuhi ilipowadia, nyumba nzima kwa
msaada wa Patrick ilianza kupekuliwa lakini
mpaka hatua ya mwisho hawakuweza kumwona
ndipo ukatolewa uamuzi watafutwe nje ya
ngome.
“Hatakuwa mbali na hapa, si ajabu alifanikiwa
kutoka na yupo porini!” Patrick aliwaeleza
wafanyakazi wake, alikuwa amedhamiria kumuua
Victoria kabisa akiamini alimpiga baba yake na
jini! Hakuna mtu kati yao aliyeelewa kwanini
Abdulwakil alipoteza fahamu mara tu baada ya
kumwona mwanamke huyo na kilichowashangaza
zaidi ni kitendo cha Abdulwakil kumtaja
mwanamke huyo kwa jina kabla ya kupoteza
fahamu.
“Jamani hizi ni nyayo za nani? Lazima kuna kitu
kimepita hapa kikijivuta!” Alipiga kelele mmoja
wa wafanyakazi waliokuwa wakimsaka Victoria.
Mchana kabla Victoria hajapelekwa nyumbani
kwa tajiri Abdulwakil mvua kubwa sana ilinyesha
ni hiyo ndiyo iliyofanya nyayo na alama za
Victoria akitambaa ardhini zionekane.
“Ni yeye ndiye kapita hapa!”Patrick alisema na
kuwaongoza wafanyakazi wake kuzifuata nyayo
hizo porini,walitembea karibu masaa mawili
wakizifuata nyayo hizo porini, ghafla walimsikia
mtu aliyekuwa mbele yao akipiga kelele kwa
sauti.
“Huyu hapa! Huyu hapa!” Wafanyakazi wote
walikimbia kwenda mbele kila mtu na silaha
yake, mwenye rungu, mwenye jiwe, mwenye
panga, mwenye nondo tayari kwa kumuua
Victoria.
Alikuwa usingizini lakini kelele hizo zilimzindua
alishindwa kuelewa ni akina nani waliokuwa
wamemzunguka.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho hapahapa

0 comments :

Post a Comment

Back To Top