Bwawa la nyumba ya mungu mikoa ya kilimanjaro na manyara limefungwa kujihusisha na uvuvi.soma zaid.
Mwanga. Serikali imesitisha kwa mwaka mmoja
shughuli za uvuvi katika Bwawa la Nyumba ya
Mungu linalotegemewa na wavuvi wa mikoa
miwili ya Kilimanjaro na Manyara kutokana na
kukithiri kwa uvuvi haramu.
Kufungwa kwa bwawa hilo ambalo sasa samaki
wanaovuliwa ni wadogo, kutakuwa na athari za
kiuchumi si kwa wavuvi tu, bali pia
wafanyabiashara na walaji.
Uamuzi wa kufungwa kwa bwawa hilo
linalotegemewa na wananchi wa vijiji vya Wilaya
za Mwanga na Moshi mkoani Kilimanjaro na
Simanjiro mkoani Manyara ulitangazwa na
Serikali juzi.
Akitangaza maazimio 14 ya wadau wa bwawa
hilo waliokutana Mwanga, Katibu Tawala (Ras)
wa Mkoa wa Manyara, Eliakim Maswi alisema
bwana hilo litafungwa kuanzia Julai Mosi hadi
Juni 2017.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Mkuu wa
Mkoa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki na wa
Manyara, Joel Bendera, wadau walikiri hali ni
mbaya katika bwawa hilo kutokana na uvuvi
haramu.
Uvuvi huo haramu umesababisha samaki
wanaovuliwa kushuka kutoka tani 25,000 mwaka
1970 hadi tani 11 mwaka 2016. Taarifa zinasema
kiwango kimekuwa kikishuka taratibu kuanzia
mwaka 1973.
Maswi alisema katika maazimio hayo, viongozi
wa vijiji na kata wakishirikiana na vyombo vya
ulinzi na usalama, wametakiwa kuwabaini
wanaomiliki nyavu aina ya makokoro ifikapo Juni
30 mwaka huu.
Kadhalika, Serikali imetoa muda wa mwezi
mmoja hadi kufikia Juni 30 wamiliki wote wa
makokoro kuyasalimisha kwa hiyari kwa vyombo
vya dola na kwamba wasiofanya hivyo
watakamatwa.
Chini ya maazimio hayo, wavuvi wote
watakaosalimisha makokoro hayo kwa hiyari,
watasainishwa mkataba wa kutorudia tena kuvua
kwa kutumia nyavu hizo na wakirudia
watafikishwa kortini.
Akizungumza katika mkutano huo, Bendera
alisema katika kipindi hicho cha mwaka mmoja,
Serikali haitaruhusu aina yoyote ya uvuvi na
mvuvi atakayeonekana ndani ya bwawa hilo
atakamatwa.
“Mvuvi yeyote atakayeonekana ndani ya Bwawa
la Nyumba ya Mungu atakamatwa. Ni lazima
tukubali kunywa dawa chungu ya mwaka mmoja
lakini tupate samaki wakubwa baadaye,” alisema
Bendera.
Akisisitiza, Sadiki alivitaka vyombo vya ulinzi na
usalama kuhakikisha vinasajili mitumbwi yote
itakayoruhusiwa kuingia ndani ya bwawa baada
ya kufunguliwa Julai 2017.
Baadhi ya wananchi wanaotegemea uvuvi
kujikimu kimaisha, walisema hatua hiyo
itawaathiri kimaisha kwa kuwa bwawa hilo ndilo
shamba lao lakini wanaafiki uamuzi wa Serikali.
0 comments :
Post a Comment