Breaking News
Loading...

Advert

Monday, May 23, 2016

Haya ndio maamuzi ya CUF soma zaid.


Chama cha Wananchi (CUF) kimesema
kitawashtaki Mahakama ya Kimataifa (ICC)
viongozi wa Serikali ambao walitumia mamlaka
yao vibaya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka
jana, wakiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani na
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.
mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF)
kimesema kitawashtaki Mahakama ya Kimataifa
(ICC) viongozi wa Serikali ambao walitumia
mamlaka yao vibaya wakati wa Uchaguzi Mkuu
wa mwaka jana, wakiwamo Waziri wa Mambo ya
Ndani na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest
Mangu.
CUF, chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar
kinachodai kuwa mgombea wake wa urais
alishinda kwenye uchaguzi huo uliofanyika
Oktoba 25, 2015, kimesema kwa sasa kinatumia
kampuni mbili za kisheria, moja ya ndani na
nyingine ya nje, kuwasaidia katika kushughulikia
suala hilo.
Mbali na vigogo hao wawili wa Serikali, chama
hicho kimesema hatua hiyo pia itawahusisha
viongozi na watumishi wa umma ambao
hawakuchukua hatua kwa dhuluma iliyofanywa
kwa Wazanzibari wakati na baada ya uchaguzi.
CUF imesema hatua hiyo itachukuliwa baada ya
jana kuzindua ripoti yake ya uvunjwaji wa haki za
binadamu visiwani humo wakati wa uchaguzi
huo.
Mbali na kuwafikisha ICC, Mazrui alisema tayari
chama hicho kimeanza kuchukua hatua stahiki ili
kuwafikisha viongozi hao kwanza mbele ya
Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kutochukua
hatua dhidi ya uovu uliokuwa unafanywa Zanzibar
wakati wa kipindi hicho.
Iwapo CUF itatekeleza azima hiyo, itakuwa tukio
la kwanza kwa Tanzania kupeleka viongozi wake
kwenye mahakama hiyo inayopingwa na viongozi
wa Afrika wanaodai kuwa wana vyombo vyao vya
kushughulikia haki za binadamu. Tayari viongozi
wawili wa Kenya, Rais na makamu wake
wameshafikishwa kwenye mahakama hiyo, lakini
kesi dhidi yao ilikosa nguvu baada ya mashahidi
kukataa kwenda kutoa ushahidi.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, mwenyekiti wa
Tume ya Uchaguzi (ZEC), Salim Jecha Salim
alifuta matokeo ya urais, wawakilishi na
madiwani Oktoba 28, mwaka jana siku ambayo
alitakiwa atangaze mshindi wa mbio za urais.
Alifuta wakati matokeo ya majimbo 31 kati ya 40
yameshatangazwa na kubakia majimbo tisa
ambayo matokeo yalishabandikwa vituoni.
CUF ilidai kuwa ilishinda na Jecha alipotangaza
uchaguzi wa marudio, chama hicho kilijitoa na
hivyo CCM kushinda viti vyote.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa,
naibu katibu mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor
Ahmed Mazrui alisema chama chake
kinakamilisha ripoti ya ukiukwaji wa wa haki za
binadamu uliofanywa wakati wa mchakato huo
ambao chama hicho kina ushahidi wa kutosha.
Alisema ripoti hiyo ina matukio yote yaliyotokea
kuanzia uandikishaji, kampeni, kuahirishwa kwa
uchaguzi na hata kurudiwa.
“Hakuna mtu aliyechukuliwa hatua za kisheria ili
kutenda haki kwa waathirika,” alisema
akizungumzia vitendo vya wananchi kupigwa na
askari, kurushiwa risasi za moto, kubambikiwa
kesi, mashambulizi yaliyofanywa na mazombi na
uchomaji nyumba za wafuasi na ofisi za wafuasi
wa chama.
Shaweji Mketo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF
alifafanua kuwa licha ya viongozi hao wa wizara
na Jeshi la Polisi kuanza kushtakiwa kwenye
mahakama za ndani, ICC itawahusisha watu
wengi zaidi.
Alisema juhudi za makusudi zimechukuliwa na
chama hicho kuwatafuta washauri wa masuala
ya kisheria na uendeshaji wa ICC ili kukusanya
ushahidi wa kutosha utakaowatia hatiani
wahusika wote.
“Waziri, IGP na baadhi ya askari watahusika.
Tunayo majina yao na uchunguzi wetu
utakapokamilika tutawataja,” alisema Mketo.
Kuhusu waziri atakayehusika kwenye mashtaka
yatakayofunguliwa ICC endapo vigezo vitatosha
ni wale waliokuwa kwenye nafasi hiyo wakati
hayo yakitokea.
“Zipo kampuni mbili zinatushauri na kutusaidia
kukusanya ushahidi,” alisema bila kuzitaja, lakini
akafafanua kuwa moja ni ya nje na nyingine ya
ndani. Alisema hazitaji majina kwa kuwa Serikali
inaweza ikaingilia kati na kukwamisha mchakato
mzima.
Baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika jana,
Mazrui alisema wamepanga kumuandikia barua
Rais John Magufuli na kumkabidhi nakala kwa
kuwa ni Amiri Jeshi Mkuu, ajue kinachoendelea
ndani ya utawala wake.
Alisema ripoti hiyo pia itapelekwa kwenye
jumuiya, taasisi na mashirika ya kimataifa
yanayotetea haki za binadamu ulimwenguni.
Alisema CUF imebaini mipango ya Serikali ya
kutaka kuwakamata viongozi wake wa Zanzibar
na “kuwaweka kwenye magereza ya Bara ili
kuwanyamazisha Wazanzibar”.
Ili kuongeza uwazi kwa wanaharakati wa ndani,
alisema ripoti ya chama chake sambamba na
vielelezo vyote muhimu, itapelekwa Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora, Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu (LHRC), Kituo cha Huduma
za Sheria Zanzibar (ZLSC) na taasisi nyingine
zinazojishughulisha na masuala ya haki za
binadamu nchini.
Ili kuongeza uwajibikaji, alisema jopo la mawakili
wa chama chake linashirikiana na wanasheria
wabobezi wa kimataifa ili kukamilisha taratibu
zitakazowezesha kuchukuliwa hatua kwa watu
wote ambao walichochea au walitoa maagizo
yaliyosababisha makosa dhidi ya binadamu.
“Tumeshamuandikia barua IGP na waziri. Hiyo ni
moja ya hatua muhimu kabla hujawashtaki,”
alisema.
Waziri hakupatikana kuthibitisha kupokea barua
hiyo. IGP alisema hajaipata ripoti hiyo, hivyo
hawezi kusema chochote juu ya madai
yaliyosemwa na CUF. “Nikiipata nitaijibu,”
alisema kwa kifupi.
Naibu katibu mkuu wa CCM-Zanzibar, Vuai Ali
Vuai alisema hujuma ni sehemu ya siasa za kila
siku visiwani humo.
Alibainisha kuwa chama chake ambacho
kimekuwa kikitangazwa mshindi tangu siasa za
ushindani ziliporejeshwa mwaka 1992, kimekuwa
kikihujumiwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa
vyama vingi na kutoa rai kwa CUF kuchukua
hatua kama ina uthibitisho.
“Makosa yote ya jinai yanashughulikiwa na
vyombo vya dola. Kinachohitajika ni ushahidi wa
kutosha,” alisema Vuai.
Pia alitahadharisha dhidi ya siasa za chuki
ambazo alisema zinaenezwa visiwani humo licha
ya kuwa pazia la Uchaguzi Mkuu limeshafungwa.
“Wapo viongozi wanaenda misikitini kuhubiri
uongo… hii si sawa,” alisema.
Kuhusu hatua za zinazotarajiwa kuchukuliwa na
CUF alisema viongozi wa chama hicho wanajua
kuwa wamekosea, hivyo wanajaribu kutafuta
namna ya kuwatuliza wanachama wao hasa wale
waliopoteza nafasi zao za uwakilishi kwenye
Baraza la Wawakilishi.
“Viongozi wanahangaika. Jinamizi la kususia
uchaguzi bado linawaandama. Hawaeleweki na
ndiyo maana wanajaribu kote kote. Mahakamani
na misikitini. Huko ni kutapatapa,” alisisitiza Vuai.chanzo mwananch.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top