Wabunge wampa mbinu waziri jinsi ya kuondoa migogoro ya ardhi nchini.soma zaid.
WABUNGE wameitaka serikali kuweka mkazo
katika kuhakikisha ardhi yote nchini inapimwa.
Pia, wametaka kuwepo na programu ya kupima
ardhi nchi nzima na kuwauzia wananchi, jambo
litakalosaidia kuondoa migogoro ya ardhi.
Wametaka suala la upimaji kutoachwa kwa sekta
binafsi, ambayo kwa mujibu wa wabunge, ina
gharama kubwa; badala yake, serikali ijiwekee
mkakati wa kupima angalau mikoa miwili kila
mwaka.
Aidha, wabunge wameyashukia mabaraza ya
ardhi huku wakikosoa kutumia watu wasio na
taaluma ya sheria katika kuamua kesi. Walitoa
maoni hayo jana wakati wakichangia mjadala wa
bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi.
Walisisitiza umuhimu wananchi kupimiwa ardhi
na kupatiwa hati. Walia upimaji ardhi Mbunge wa
Mbinga, Sixtus Mapunda (CCM), alisema kuwe na
programu maalumu ambayo serikali itakuwa na
vifaa vya upimaji nchi nzima na kupima ardhi
yote ; na pale mwananchi anaponunua ardhi
anakuta eneo limepangwa.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuondoa usumbufu
wa kupima kwa gharama kubwa na wakati huo
huo kukabili migogoro ya ardhi. Alitoa mfano wa
Jiji la Dar es Salaam, ambalo serikali inakabiliwa
na usumbufu wa kulipanga.
Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary
Mgumba (CCM) aliunga mkono umuhimu wa
kupima maeneo yote, kuondoa utata na kumaliza
migogoro ya ardhi. Mwingine aliyehimiza upimaji
wa maeneo yote ni Mbunge wa Viti Maalumu,
Cecilia Paresso (Chadema ) ambaye alishauri
wananchi wapimiwe maeneo kwa kuwakopesha
kisha walipe madeni hayo taratibu.
Alisema kwa kufanya hivyo serikali mbali na
kuondoa migogoro ya ardhi, pia itaingiza kipato
kutokana na wananchi kulipia hati. Wakosoa
mabaraza Wakati huo huo katika kuchangia,
baadhi ya wabunge wametaka kazi za kiutendaji
katika masuala ya ardhi zifanywe na wataalamu
wa ardhi ; na serikali iachane na utaratibu wa
sasa wa kuwapa kazi watu kiholela.
Walitaka mabaraza ya ardhi yasimamiwe na
wataalamu wa ardhi, badala ya kuchukua watu
wasio na taaluma. Mbunge wa Manyoni
Mashariki, Daniel Mtuka (CCM), alieleza
kushangazwa na kitendo cha serikali kukabidhi
jukumu kubwa la usuluhishi wa masuala ya ardhi
kwa watu ambao hawajasoma na hawajui sheria
za ardhi.
Alisema, wapo wataalamu wengi nchini ambao
wamekwenda kusomea masuala ya ardhi
wanaotakiwa kufanya kazi hiyo, lakini wamekuwa
wakitumiwa watu maarufu vijijini kufanya kazi
hiyo.
0 comments :
Post a Comment