Breaking News
Loading...

Advert

Wednesday, June 8, 2016

Kutoka bungeni# hii hapa bajeti ya 2016/2017 imesilishwa bungeni.soma zaid.

Dodoma. Sauti ya Rais John
Magufuli inasikika redioni kila mara ikiwasisitizia
wananchi kudai risiti kwa kila bidhaa
wanayonunua ili Serikali ipate kodi yake ya
kuwezesha kutoa huduma kwa wananchi.
Kauli hiyo ndiyo inategemea kuakisiwa kwenye
maeneo mengi ya Hotuba ya Makadirio na
Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2016/17
itakayosomwa leo na Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk Phillip Mpango bungeni mjini
Dodoma.
Kwa mujibu wa hotuba ya kiwango na ukomo wa
bajeti ya mwaka 2016/16 iliyowasilishwa awali na
Dk Mpango miezi miwili iliyopita, Serikali
inatarajia kukusanya na kutumia Sh29.5 trilioni,
ikiwa ni ongezeko la takribani Sh7 trilioni
kulinganisha na bajeti ya mwaka 2016/17.
Katika hotuba hiyo, Dk Mpango alisema fedha
zinazotarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo vya
ndani ni Sh18.5 trilioni ikijumuisha mapato kutoka
serikali za mitaa, kiwango ambacho ni takriban
asilimia 62.5 ya bajeti yote.
Kwa maana nyingine, nakisi ya bajeti ni takriban
Sh9 trilioni ambayo itajazwa kwa kutumia fedha
za mikopo ya ndani na nje na misaada.
Ni dhahiri kuwa kwa kiwango hicho cha Sh18.5
trilioni kinachotegemea kutoka katika mapato ya
ndani, Serikali ya Magufuli itashika kila
inapoweza kuhakikisha fedha za Serikali
zinalipwa kadri inavyotakiwa.
Na hii itamaanisha kuwa kila mtu ataguswa
kuanzia mwananchi wa kawaida anayetegemea
nyumba kuendesha maisha, biashara ndogo,
mpangaji hadi mfanyabiashara mkubwa ataguswa
na mkono wa Serikali ambayo inataka kuipeleka
nchi kwenye uchumi wa kati unaotegemea
viwanda.
Kwenye mpango wake wa bajeti kwa mwaka
2016/2017, Serikali imesema itapanua wigo wa
kodi ili kutunisha mfuko wake utakaogharamia
miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida.
Fedha hizo zitakusanywa ili zielekezwe
kuimarisha maeneo ya vipaumbele ambayo ni
pamoja na kufufua na kuanzisha viwanda
vitakavyotumia malighafi zinazopatikana nchini
kwenye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na
maliasili nyinginezo pamoja na vile vinavyozalisha
bidhaa zinazotumiwa na watu wengi nchini kama
nguo, viatu na mafuta ya kupikia.
Vingine ni vile vinavyotumia teknolojia ya kati na
kuajiri watu wengi. Baada ya kuzalisha bidhaa za
kutosha kutoka kwenye viwanda hivyo.
Kazi ya Serikali kuhakikisha lengo hilo linafikiwa
ni kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji kwenye
viwanda, kama ujenzi wa miundombinu ya usafiri
kama Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa,
barabara, bandari na viwanja vya ndege,
kuimarisha sekta ya nishati na kuandaa rasilimali
watu.
Kwenye miundombinu ya usafiri, sehemu
zinazotarajiwa kuimarisha ni usafiri wa abiria na
mizigo katika maziwa makuu (Victoria,
Tanganyika na Nyasa), ikiwa ni pamoja na
ununuzi wa meli mpya, na kununua ndege mpya
ili kuijengea uwezo Kampuni ya Ndege (ATCL).
Haya yakifanyika, wakazi wa Dar es Salaam,
Arusha na Dodoma watakuwa na uhakika wa kula
samaki wabichi kutoka Ziwa Nyasa au sato wa
Mwanza ama migebuka ya Kigoma ndani ya saa
24.
Wakazi wa mikoa kama ya Kanda ya Magharibi
hawatatumia tena siku tatu njiani kutoka Dar es
Salaam mpaka Kigoma. Bajeti hiyo pia itajenga
mtambo wa kusindika gesi kimiminika (LNG)
ambao utaenda sambamba na kusomesha vijana
katika fani za mafuta na gesi, uhandisi, kemikali,
tiba na afya.
Asilimia 40 ya bajeti nzima ya Sh29.5 trilioni,
imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Miradi mipya itakayosimamiwa na Serikali
yenyewe imetengewa Sh6.2 trilioni.
Lakini haya yote yatawezekana baada ya kodi ya
kutosha kukusanywa.
Mbunge wa Mafinga Mjini kwa tiketi ya CCM,
Cosato Chumi alisema uamuzi wa kutenga
asilimia 40 ya bajeti kwa ajili ya miradi ya
maendeleo unaleta matumaini kwa wananchi.
Alisema kwa miaka kadhaa miradi ya maendeleo
ilikuwa inatengewa fedha, lakini hazifiki hivyo
kutokana na msimamo wa Serikali iliyopo wa
kubana matumizi yasiyokuwa ya msingi fedha za
miradi ya maendeleo zitapatikana kwa asilimia
100 tofauti na ilivyokuwa awali.
“Mimi naona itakuwa ni bajeti ya ahueni kubwa
sana lakini sambamba na ahueni hiyo, pamoja na
kwamba hatujaiona bado, ninatarajia kutakuwa
kuna upanuzi wa wigo wa mapato,” alisema
Chumi.
“Kwa jinsi Serikali hii ilivyoanza, tunaweza
tukaondokana na utamaduni ule wa kuongeza
kodi sijui kwenye kiberiti, soda na bia. Imani
yangu inaniambia kutakuwa na wigo mpana wa
ukusanyaji wa mapato.”
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara,
Johnson Minja alisema endapo mazingira ya
kufanya biashara yatarahisishwa, Serikali
itakusanya zaidi ya malengo hayo.
“Kuna mtu anao mtaji wa kuagiza shehena za
vijiti vya meno au karatasi za chooni. Huyu
anahitaji kukalishwa na kuambiwa ajenge
kiwanda ili asiagize kutoka nje. Uwezo wa
kuanzisha viwanda vidogo tunao,” alisema Minja.
Alipendekeza lianzishwe dirisha la huduma za
pamoja za vibali na leseni za biashara.
Malengo ya Serikali ni kukusanya mapato ya kodi
ya Sh14.11 trilioni ambayo ni sawa na asilimia
13.2 ya pato la taifa kwa muda huo wa bajeti.
Kiwango hicho kitaongezeka mpaka asilimia 13.5
mwaka 2017/2018 na 14.4 mwaka 2019/2020.
Ili kufanikiwa hayo yote, Serikali itakusanya kodi
ya moja kwa moja. Hapa kutakuwa na kodi ya
mshahara (Paye) na mapato ya watu binafsi,
kampuni, zuio na michezo ya kubahatisha. Tozo
ya kuendeleza ujuzi pia itahusika. Kila mmoja
amsimamie mwenzake mpaka Serikali ipate
Sh5.3 trilioni ilizokusudia.
Dk Mpango pia anatarajiwa kueleza jinsi Serikali
itakavyokusanya fedha kutoka kwenye kodi zisizo
za moja kwa moja ambazo zitatoka kwenye
ushuru wa bidhaa za ndani kama vile vinywaji,
sigara na muda wa matumizi kwa simu za
viganjani.
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) nayo
itazingatiwa kwa kwa umuhimu wake mapka
Sh3.92 trilioni zipatikane.
Edmund Mariki, katibu mtendaji wa Chama cha
Wasindikaji wa Maziwa Tanzania (Tampa)
alisema ipo haja kwa Serikali kuona namna
njema ya kupunguza kodi za wazalishaji wa
sekta ya kilimo.
“Viwanda vinategemea malighafi za kilimo, uvuvi
na ufugaji. Inapaswa kumpa mwekezaji sababu
za kuchangamkia fursa zilizopo huko,” alisema
Mariki.
Asanterabi Barakaeli, aliyebobea katika masuala
ya mikopo ya miradi, alisema itakuwa ni fursa
kwa sekta ya benki na huduma za fedha nchini
endapo Serikali itawatumia wataalamu au taasisi
za ndani kutekeleza miradi yake.
“Kodi zipunguzwe ili wafanyabiashara wapate
faida. Hiyo itawapa ari ya kukopa kutoka benki
na kuwekeza kizalendo,” alisema Asanterabi.
Baadhi ya wadau wameonyesha wasiwasi
kutokana na Serikali kutofikisha fedha za miradi
ya maendeleo.
Akizungumzia sekta ya afya, mkurugenzi wa
taasisi ya Sikika, Irenei Kiwia alisema hakuna
matumaini kwa sababu tayari bajeti ya Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto imeonyesha kuwa pungufu kuliko mahitaji
yaliyopo.
“Bajeti yenyewe bado haitoshi kwa sababu
matatizo yaliyopo kwenye sekta ya afya ni
makubwa mno. Wamesema wameongeza bajeti
ya dawa, lakini kwa kuwa kuna deni la Bohari ya
Dawa (MSD) la Sh131 bilioni, huenda fedha yote
ikaelekezwa kulipa deni, maana yake hakuna kitu
kilichoongezwa hapo,” alisema Kiwia.
Mbunge wa Iringa Mjini(Chadema), Mchungaji
Peter Msigwa alisema hategemei jipya kwenye
bajeti ya leo kwa kuwa kwa mara ya kwanza
mawaziri wote hela walizotengewa katika idara
mbalimbali zimekuwa hazitoshi, lakini wanaogopa
kusema.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top