Mapato bandàri ya Dar es salaam yaongezeka.soma zaid.
Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata
amesema mapato katika Bandari ya Dar es
Salaam yameongezeka katika miezi miwili
iliyopita licha ya mizigo inayopitia hapo
kupungua.
Kidata alisema hayo jana baada ya hivi karibuni
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutoa
taarifa kuhusu kushuka kwa zaidi ya asilimia 50
mizigo inayosafirishwa kwenda nchi jirani za DR
Congo na Zambia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana Kidata alitaja sababu za kupungua
kwa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam
kuwa ni matatizo yaliyopo duniani kote
yakichagizwa na kuyumba kwa uchumi wa China
hivyo siyo Tanzania pekee iliyoathirika.
Kamishna huyo alisema utafiti walioufanya
umebainisha kwamba mizigo imepungua pia
katika Bandari za Mombasa, Beira na Durban ya
Afrika Kusini. Hata hivyo, alisisitiza kuwa licha ya
kupungua kwa mizigo, mapato ya bandarini
yameongezeka kwa sababu wameziba mianya ya
uingizaji mizigo kwa njia zisizo rasmi na
wamejipanga vema kuhakikisha mizigo yote
inapita bandarini na kulipiwa kodi stahiki.
“Ni kweli mizigo imepungua bandarini lakini siyo
nchini kwetu pekee, hata bandari nyingine. Hapa
kwetu limekuwa likizungumzwa sana. China ni
nchi kubwa na ya pili kiuchumi duniani, na ndiyo
inayoongoza kwa kusafirisha mizigo, wao
wameyumba kidogo, hivyo wakapunguza
kusafirisha. Lazima na sisi huku tutaathirika pia,”
alisema.
Kamishna huyo alisema walikuwa wakikusanya
Sh200 bilioni hadi Sh300 bilioni kwa mwezi
kutoka katika bandari hiyo lakini baada ya
kudhibiti mianya ya uingizaji mizigo, Aprili
walikusanya Sh458 bilioni na Juni walikusanya
Sh517 bilioni.
Na kuhusu makusanyo ya jumla ya TRA, Kidata
alisema kwa Juni makusanyo yameongezeka
kufikia Sh1.41 trilioni kutoka lengo la Sh1.31
trilioni. Vilevile, alisema makusanyo kwa mwaka
uliokwisha pia yameongezeka kwa wastani wa
asilimia 100.04 hadi kufikia Sh13.37 trilioni
badala ya Sh13.31 trilioni ya lengo.
Aprili 2, mwaka huu wakati akifunga warsha ya
Wahariri wa Habari, Kaimu Meneja wa Bandari ya
Dar es Salaam, Hebel Mhanga alisema kwamba
mizigo inayokwenda katika nchi hizo inapitia
Bandari ya Beira, Msumbiji.
Mhanga alionyesha hofu yake kwamba huenda
hali ikawa mbaya zaidi kwa Bandari ya Dar es
Salaam baada ya kukamilika kwa ujenzi wa reli
ya kisasa inayoanzia katika Bandari ya Mombasa
(Kenya) mpaka DR Congo, kwa kuwa itaongeza
unafuu wa usafirishaji wa mizigo katika bandari
hiyo shindani kwa Tanzania.
Aidha, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip
Mpango alilieleza Bunge Aprili kuwa kutoka
Oktoba 2015 hadi Machi mwaka huu mizigo
ilikuwa ikipungua bandarini huku makontena
kutoka nchini Congo yakishuka hadi kufikia
makontena 4,092 kutoka makontena 5, 529.
Dk Mpango alieleza kuwa mizigo ya kwenda
Malawi ilishuka kutoka makontena 337 hadi 265,
huku yale Zambia yakishuka kutoka makontena
6,859 hadi kufikia 4,448.
Akifafanua kuhusu kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) kwenye mizigo, Mtafiti Mwandamizi Mkuu
wa TRA, Beldon Chaula alisema Sheria ya VAT
hairuhusu mizigo ya kimataifa kutozwa kodi
isipokuwa kwa huduma nyingine zitakazofanyika
hapa nchini.
Alisema mizigo yote inayosafirishwa ndani ya
nchi na kutumiwa ndani, itatozwa kodi ya VAT
kama ilivyo kwa bidhaa nyingine. Alisisitiza
kwamba hiyo siyo sababu ya kupungua kwa
mizigo bandarini kwa sababu mizigo inayotoka
nje na inayokwenda nje hailipiwi kodi.
“Mizigo inayotoka nje kwenda bandarini hailipiwi
kodi isipokuwa huduma nyingine kama kupakia
mizigo, kushusha mizigo au kuhifadhi mizigo
ndizo zinatozwa kodi ya VAT,” alisema Chaula.
Kamishna wa Mapato ya Ndani, Elijah
Mwandumbya alisema wamejipanga kuhakikisha
kwamba wafanyabiashara wote wanatumia
mashine za kielektroniki za EFD na kwamba
watapita sehemu mbalimbali kuhakiki kama
wanatumia mashine hizo au la.
0 comments :
Post a Comment