Watu 3 wa wanaosadikiwa kutengeneza vyeti bandia wakamatwa.soma zaid
Watu watatu wanaosadikiwa kuwa vinara
wa kutengeneza vyeti bandia pamoja na
nyaraka mbalimbali za Serikali
wamekamatwa eneo la Buguruni wakiwa
na mitambo yao.
Kukamatwa kwao kulitokana na msako
mkali uliofanywa na Jeshi la Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam hivi karibuni
na hatimaye watuhumiwa walinaswa
wakiwa nyumbani wanakoishi eneo la
Buguruni Ghana wakitengeneza nyaraka
bandia.
Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro
aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa
ni Ashraff Maumba (37) mkazi wa
Buguruni Ghana, Mwamba Seif (38) mkazi
wa Mnyamani, na Mahmudu Zuber (24)
mkazi wa Buguruni.
Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana
kwamba Julai 8, saa 4.00 usiku walifanya
upekuzi katika nyumba wanayoishi na
kukuta nyaraka mbalimbali vikiwamo vyeti
bandia vya kidato cha nne 50 na vyeti vya
vyuo vya uuguzi.
Kamanda huyo alisema nyaraka nyingine
bandia zilizokamatwa ni stika 20 za
Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi
Kavu (Sumatra), vyeti vya kuzaliwa 10 na
vya Chuo cha Ufundi (Veta).
Nyaraka nyingine zilizokamatwa, kwa
mujibu wa Sirro ni leseni za biashara,
stika 100 za bima za magari, mitambo na
vivuli 10 bandia vya vyeti vya Chuo cha
Biashara (CBE).
Katika upekuzi huo pia walikamata mihuri
mbalimbali ya ofisi za Serikali na binafsi
ukiwemo muhuri wa Bibi na Bwana.
“Tulifanikiwa kukamata vifaa mbalimbali
vya kutengenezea nyaraka zikiwamo
karatasi maalumu zilizo na nembo ya
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa
ajili ya kutengeneza zaidi ya kadi 500 za
vyombo vya moto, kompyuta nne na
mashine moja ya kuchapisha,” alisema
Sirro.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi huku
upelelezi ukiendelea na ukikamilika
watafikishwa mahakamani ili kujibu
mashtaka yanayowakabili.
Katika hatua nyingine, Mpiga Chapa Mkuu
wa Serikali, Cassian Chibogoyo alisema
Serikali haitakubali kuhujumiwa na watu
wachache hivyo itachukua hatua kali kwa
wote wanaojihusisha na utengenezaji
vyeti bandia vya Serikali.
“Tunashukuru jeshi la polisi kuibua shina
ambalo lilikuwa linatusumbua sana
kutambua ni wapi wanatengeneza vyeti
hivi vya bandia na tumepata taarifa za
mawakala wanaofanya ujanja huo,”
alisema Chibogoyo.
0 comments :
Post a Comment