CHADEMA inavyopangua kete za ccm.soma zaid
Dar es Salaam. Wakati Serikali ya CCM
imekuwa ikijenga mazingira ya kuzuia
uwezekano wa vyama vya upinzani kufurukuta,
Chadema imekuwa ikichanga karata zake na
kuendelea kujiimarisha na kushindana kisiasa na
chama tawala.
Kwa mujibu wa baadhi ya wasomi na wanasiasa
nchini, matukio makubwa ya kisiasa
yanayoandaliwa na Chadema na kuibua mijadala
imekuwa ikifanywa kimkakati sambamba na ya
chama tawala, CCM.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Richard Mbunda aliliambia Mwananchi
kwamba aonavyo yeye matukio mbalimbali ya
Chadema ni mikakati ya kisiasa. “Inabidi
wafanye matukio ili chama kiendelee kubaki
katika ramani ya siasa,”alisema Mbunda.
Mwenyeki wa Chadema, Freeman Mbowe
amesema tofauti na mawazo ya baadhi ya watu,
matukio hayo zikiwamo operesheni mbalimbali
za chama si mikakati ya kudumu bali ni za
muda maalumu kwa malengo maalumu ambayo
ikikamilika wanabuni mbinu nyingine.
Chadema wamekuwa wakibuni mikakati
mbalimbali ya kuwafikia wananchi tangu
mikutano na maandamano ya vyama vya siasa
ilipopigwa marufuku na Rais John Magufuli hadi
mwaka 2020. Mikutano iliyoruhusiwa ni ya
wabunge tu tena katika majimbo yao, lakini si ya
wanasiasa.
Katika Bunge la Bajeti, wabunge wa Chadema
wakishirikiana na wenzao kutoka vyama vya
siasa vinavyounda Ukawa walikuwa wakisusa
vikao kwa staili tofauti. Kuna siku walitoka nje
wakiwa wamevaa mavazi meusi, siku nyingine
walibandika vitambaa mdomoni na kuna siku
walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Julai mwaka huu, CCM ilipoandaa mkutano
maalumu uliopangwa kwa ajili ya kumkabidhi
Rais Magufuli kijiti cha uenyekiti wa chama
hicho, Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha)
lilizua hofu lilipotangaza kwamba litakwenda pia
Dodoma kulisaidia Jeshi la Polisi kuzuia
mkutano huo kwa kuwa Serikali ilipiga marufuku
mikutano ya ndani na nje.
Hatua hiyo ya Bavicha ilisababisha Jeshi la
Polisi kuweka ulinzi mkali kila kona mjini
Dodoma kuzuia uwezekano wa Bavicha
kuvuruga mkutano huo wa CCM. Hata hivyo,
Bavicha walipiga chenga, walikutana Dar es
Salaam ambako walifanya mkutano wao.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM
walipokuwa katika shangwe na nderemo baada
ya kukamilisha ajenda yao ya kumchagua kwa
asilimia 100 Rais Magufuli, Kamati Kuu ya
Chadema iliketi Dar es Salaam na kutoka na
mkakati wa kupinga uvunjaji wa Katiba na
sheria waliouita operesheni Ukuta ambao
unasumbua vyombo vya usalama hadi sasa.
Matukio hayo ambayo yametokea kwa kufuatana
yamekuwa yakigonga vichwa vya habari huku
baadhi wakidai ni dalili za vurugu na uchochezi,
lakini pia yanakiweka chama hicho kwenye
mjadala kuliko vingine.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa
waliotafutwa na gazeti hili jana kuzungumzia
namna Chadema inavyocheza karata zake
kuhakikisha inasikika sawa au hata kuifunika
CCM, wamesema huo ni mkakati wa upinzani
kuendelea kutamba kwenye ‘ulingo wa siasa.’
Baadhi ya operesheni zilizoijengea umaarufu ni
kama Sangara na Movement For Change (M4C).
Akizungumzia mfuatano wa matukio hayo,
Mbunda amesema aonavyo yeye matukio hayo ni
mikakati ya kisiasa akibainisha kuwa kila chama
kina wapangaji mikakati ambao hupanga na
kutathmini mikakati hiyo. “…Siyo mikakati yote
inayofaulu. Wakiona huu haufai wanaweza
kubadili.”
Mhadhiri huyo alitoa mfano wa Operesheni
Ukuta ya Chadema iliyopangwa kufanyika
Septemba Mosi mwaka huu kwamba huenda
wakati ukifika chama hicho kikabadili uamuzi
wake baada ya kufanya tathmini ya operesheni
hiyo.
Mbunda amesema kwamba hizo ni amsha
amsha ambazo husaidia vyama hasa vya
upinzani kuendelea kuonekana katika uso wa
siasa na kwamba vyama mbalimbali duniani
hutumia mbinu hizo hivyo siyo jambo la
kushangaza. “Wasipofanya hivyo hata watu
watahoji kwa sababu hayo ndiyo maisha ya
siasa,”alisema Mbunda.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Dk Benson Bana
ambaye alisema kinachofanywa sasa na
Chadema ni mkakati wa kuendelea kubaki na
kusikika kwenye uwanja wa siasa.
Dk Bana, ambaye ni mhadhiri wa UDSM
amesema chama hicho kinafanya hivyo ili
kisipotee kwenye ramani ya siasa hadi Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2020.
Mchambuzi huyo wa masuala ya siasa
alibainisha kuwa chama hicho kikuu cha
upinzani kinafanya hivyo kwa sababu kilikuwa
hakijajipanga kuona Serikali ya awamu ya tano
inatekeleza baadhi ya ajenda zao.
“Hawajajipanga kuwa na mikakati endelevu…
wanaona wamenyang’anywa tonge mdomoni.
Mikakati yao ni ya kuziba ombwe hilo,” alisema.
Pia, Dk Bana amesema jambo hilo siyo baya
kwenye ulimwengu wa siasa tatizo ni aina ya
mikakati kwamba Chadema inapaswa kuja na
mikakati ambayo inakidhi haja ya Watanzania
siyo mikakati ya kumwita Rais John Magufuli
dikteta. “Watathmini mikakati yao. Waje na
mikakati yenye mashiko,”amesema Dk Bana.chanzo muungwana.com
0 comments :
Post a Comment