Breaking News
Loading...

Advert

Tuesday, January 24, 2017

Mtendaji wa kijiji anusurika kifo kwa kutetea wazi wa mifugo.soma zaid

Mtendaji wa Kijiji cha Iponyanholo, Kata ya
Sabasabini wilayani Kahama, Shinyanga, Elias
Mpigamamoni.
Kwa ufupi
“Kwanza sikuweza kuelewa kilichokuwa
kinaendelea, taratibu nilianza kukumbuka
kwamba nilikuwa kwenye mkusanyiko wa
walinzi wa jadi muda mfupi uliopita lakini
kumbukumbu ziliniijia kwamba nilipigwa fimbo
kichwani.”
By Shija Felician, Mwananchi
“Kama ni kuonja kifo basi mimi nilikionja ingawa
ninachokumbuka ni mtu mmoja aliyenirukia na
kuanza kunipiga fimbo kichwani... Taratibu
nilianza kuona nyota nyota zikitanda usoni na
baadaye nilishtuka nikiwa kwenye gari huku nguo
zangu zote zikiwa zimelowa damu.
“Kwanza sikuweza kuelewa kilichokuwa
kinaendelea, taratibu nilianza kukumbuka
kwamba nilikuwa kwenye mkusanyiko wa walinzi
wa jadi muda mfupi uliopita lakini kumbukumbu
ziliniijia kwamba nilipigwa fimbo kichwani.”
Ndivyo anavyoanza kueleza Elias Mpigamamoni
mwenye umri wa miaka 49 kufutia kisa cha yeye
kupigwa na wananchi wenzake kwa kile
kilichodaiwa kuwa alikuwa akiwatetea wezi wa
mifugo.
Kwa mujibu wa Mpigamamoni, baada ya kupata
fahamu aliwatambua watu wote waliokuwa ndani
ya gari hiyo na haraka akagundua kuwa kumbe
safari hiyo ni yake alikuwa akipelekwa hospitalini
baada ya kupata majeraha kichwani na usoni
kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa
wananchi.
Jinsi ilivyokuwa
Mpigamamoni ambaye ni Mtendaji wa Kijiji cha
Iponyanholo kata ya Sabasabini wilayani
Kahama, Shinyanga anasema kuwa alipata kipigo
hicho wakati akiwazuia walinzi wa jadi
sungusungu kuwaua watuhumiwa wawili wa wizi
wa ng’ombe waliokuwa wamewakamata.
Anasema mara baada ya walinzi hao kuwatia
nguvuni watuhumiwa hao walianza kuwapiga kwa
lengo la kuwaua ndipo alipotokea yeye na
kupinga kitendo hicho ambapo alitaka wafikishwe
katika vyombo vya sheria.
“Nilikuwa nikitekeleza agizo la Serikali kwa
viongozi wake kusimamia amani hasa maeneo ya
vijijini ambako ukiukwaji wa sheria umekithiri
kwani kwa mujibu wa taarifa Wilaya ya Kahama
inaongoza kwa mauaji ya watu wasio na hatia
ambao huuawa kwa kuchomwa moto au kukatwa
mapanga.
Mpigamanoni anasema kuwa alipigiwa simu na
diwani wa kata hiyo Emmanuel Makasi aende
kwenye tukio hilo ambalo sungusungu walikuwa
wamewazingira watuhumiwa wakitaka kuwaua
kwa kuwachoma moto.
Kutokana na hali hiyo mtendaji huyo alitumia
nguvu kubwa kuzuia wananchi hao wasifanye
mauaji hayo waliyokusudia.
Anasema baada ya kuwazuia alishtukia ameanza
kushambuliwa kwa fimbo kichwani huku akisikia
sauti za watu zikidai mtendaji huyo pamoja na
watuhumiwa wa wizi wa ng’ombe wauwawe kwa
kuchomwa moto na kazi hiyo ilianza.
Anasema alisikia sauti zikisema
mnawachelewesha, watu hao wanapaswa
kuuawa wote na hapo kijana mmoja alichomoka
kwenye kundi na kuanza kumshambulia mmoja
wa watuhumiwa.
Pamoja na juhudi za kumuokoa kushindikana
kibao kilimrudia yeye na kushambuliwa kwa
kipigo na watu hao mpaka alipopoteza fahamu na
hajui ni nani aliyemuokoa.
Anasema baada ya shambulio hilo alipoteza
fahamu na kupelekwa hospitali ya Halmashauri
ya Mji wa Kahama ambako alipatiwa matibabu.
Mganga mfawidhi katika hospitali hiyo Dk Joseph
Ngowi anasema mtendaji huyo alifikishwa hapo
akiwa na majeraha kichwani ambayo yalionyesha
yalitokana na kupigwa na vitu vizito.
Ngowi anasema hivi sasa hali yake ni nzuri
ingawa ataendelea kufanyiwa uchunguzi
kutokana na majeraha hayo ya kupigwa yalikuwa
kichwani hali ambayo inaweza kuwa na madhara
kwa ndani.
Mtendaji wa kata ya Sabasabini Christopher
Lyogelo anasema mtendaji huyo alipigwa akiwa
kwenye majukumu yake ya kutekeleza agizo la
Mkuu wa Wilaya na mkakati mzima wa kata hiyo
kuzuia matukio ya wananchi kuua watu
wanaowatuhumu kwa wizi wa mifugo.
Diwani wa kata hiyo Emmanuel Makashi
anasema mtendaji huyo alipigwa baada ya
kutokea ugomvi kati yake na mtu mmoja
aliyejulikana kwa jina la Nkinga Nzinza ambaye
hata hivyo alikimbia kusikojulikana. Mpaka sasa
polisi mjini Kahama wanaendelea kumsaka kwa
RB Namba KAH/RB/7721/2016.
Makashi anasema baada ya mtendaji kupigwa na
yeye kufika kwenye tukio alituliza vurugu hizo na
watuhumiwa wote aliwatoza faini za jadi ambapo
kwa pamoja walilipa Sh150,000 na ng’ombe
mmoja ambaye alirejeshwa kwa mwenyewe na
fedha hizo ziligawanywa zote kwa
wanasungusungu.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya wadau wa
maendeleo wilayani Kahama akiwamo Jackson
Mpejiwa wameeleza kuwa Serikali inapaswa
kuangalia upya ulinzi wa sungusungu vijijini
kutokana na uamuzi wao kutozingatiwa.
Polisi wazungumza
Kamanda wa polisi Mkoa wa Shinyanga, Muliro
Jumanne amekiri kutokea kwa tukio hilo na
kusema kuwa uchunguzi unaendelea juu ya tukio
hilo.
“Ni kweli tumepokea taarifa juu ya kujeruhiwa
kwa mtendaji huyo wakati akijaribu kuzuia
sungusungu wasiwaue watu wanaotuhumiwa kwa
wizi wa mifugo.
“Nataka kutoa wito kwa wananchi waache
kujichukulia sheria mikononi kwani si jambo
jema. Endapo watakamata watuhumiwa ni vyema
wawafikishe katika kituo cha polisi kwa taratibu
za kisheria,” anasema Kamanda Jumanne.
Awali diwani Makashi alisema sungusungu hao
wamekubaliana kufanya kikao cha mazungumzo
ya kulimaliza tatizo hilo mezani.
Agizo la Mkuu wa Wilaya
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Basil
Nkurlu alifanya mkutano wa pamoja na watendaji
wa kata na vijiji na kuwaeleza kwamba yeyote
yule ambaye atabainika kwamba kwenye eneo
lake kuna mtu ameuawa na wananchi ataanza
kuwajibika nae kwanza.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top