Watumishi wengine 100,000 wanaofanya kazi serikali kuu wenye vyeti feki kuanikwa hadharani. Soma zaid
SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli
kupokea ripoti ya awamu ya kwanza na pili ya
uhakiki wa vyeti vya kitaaluma vya watumishi wa
umma ambayo imebaini watumishi 9,932 wana
vyeti vya kughushi, watumishi wengine
wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 100,000 nao hatima
yao itajulikana ndani ya siku tano zijazo.
Watumishi hao ni wale wanaofanya kazi Serikali
Kuu, kwa maana ya wafanyakazi wa wizara 18
isipokuwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, ambayo tayari ripoti yake
imekwishawasilishwa juzi.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella
Kairuki, alisema ripoti ya tatu ya uhakiki
itawasilishwa Ijumaa ijayo na imegusa wizara
zote.
Alifafanua kwamba ripoti aliyoiwasilisha juzi kwa
Rais Magufuli, ilikuwa ya awamu mbili ambazo
ziligusa mamlaka za Serikali za mitaa na
sekretarieti za mikoa, taasisi za Serikali,
mashirika ya umma, tume na wakala za Serikali.
Kwa mujibu wa Kairuki, ripoti iliyowasilishwa juzi
iligusa asilimia 75 ya watumishi wote wa
Serikali.
Kwa msingi wa maelezo hayo, MTANZANIA
Jumapili lilifanya makadirio ya kimahesabu kwa
kuangalia kama asilimia 75 ya watumishi
waliohakikiwa ni 400,035, basi asilimia 25
iliyobaki huenda ikawa ni watumishi 133,345.
Kwa mantiki hiyo, hatima ya watumishi hao
itajulikana Ijumaa ijayo wakati ripoti yao
itakapowasilishwa kwa Rais Magufuli.
Awali gazeti hili lilitaka kufahamu idadi ya
watumishi wote wa umma, lakini ilishindikana
baada ya Kairuki kusema kuwa anayefahamu hilo
ni Katibu Mkuu Kiongozi, huku Ikulu nayo ilidai
kuwa suala hilo lipo chini ya waziri huyo.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Kairuki
alisema katika mazingira aliyokuwapo ni vigumu
kupata idadi moja kwa moja, hivyo akamshauri
mwandishi amtafute Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi John Kijazi.
“Sasa unaniulizia hapa nitakujibu kweli? Mpaka
na mimi niwasiliane na watu wangu au mpigie
Katibu Mkuu labda yeye anaweza akawa na hizo
takwimu karibu kwa sababu si unajua leo
wanafutwa, mara wameondolewa wengine. Basi
wewe mpigie Katibu Mkuu, usipompata nitumie
ujumbe mfupi wa maneno nimtafute,” alisema
Waziri Kairuki.
Juhudi za kumpata Kijazi ziligonga mwamba
baada ya simu yake kutokuwa hewani.
MTANZANIA Jumapili lilipowasiliana na
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais
Ikulu, Gerson Msigwa, alisema mwenye dhamana
ya kuzungumzia jambo hilo ni Waziri Kairuki.
Alipotafutwa kwa mara nyingine Waziri Kairuki,
simu yake haikupokewa kila ilipopigwa na hata
alipotumiwa ujumbe mfupi wa mawasiliano kwa
mujibu wa agizo lake, hakujibu chochote hadi
gazeti hili linakwenda mtamboni.
Juzi wakati akiwasilisha ripoti ya awamu ya
kwanza na ya pili, Kairuki alikaririwa akisema;
“Ukiangalia watumishi wengi wako ngazi za
halmashauri ambako wanafikia kati ya asilimia 75
hadi 80 na sisi ndio tumeanza hao, Ijumaa
tunapata ripoti ya mawizara.”
ILIVYOKUWA JUZI
Waziri Kairuki akiwasilisha ripoti ya awamu ya
kwanza na pili ya uhakiki wa watumishi wa
umma mbele ya Rais Magufuli, alisema mpango
wa uhakiki kwa watumishi wa umma
haukuwagusa mawaziri, wakuu wa mikoa na
wakuu wa wilaya, kwa sababu sifa wanazotakiwa
kuwa nazo ni kujua kusoma na kuandika pekee.
“Uhakiki uliwahusu watumishi wa umma pekee,
wakiwamo makatibu wakuu wote na viongozi
mbalimbali katika ngazi ya utumishi wa umma.
“Hatua hii inatokana na ukweli kwamba kwa
mujibu wa sheria, pamoja na miundo ya
maendeleo ya utumishi serikalini, wanatakiwa
kuwa na sifa za msingi za kuingilia na kutumikia
nafasi zao ikiwa ni pamoja na vigezo vya elimu
na vigezo vya kitaaluma, hivyo uhakiki
haukuwahusisha viongozi wa kisiasa.
“Mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wakuu
wa wilaya na madiwani kwa mujibu wa sheria na
taratibu za nchi, wote mnafahamu uteuzi na
uchaguzi unafanyika kwa misingi ya wahusika
kuwa na sifa ya kujua kusoma na kuandika.
“Na hii ni kwa mujibu wa Ibara 61(1) ya Katiba,
isije ikaonekana ni maneno ya Kairuki,” alisema.
Alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa
kuimarisha usimamizi na mifumo maalumu,
hususani ya upokeaji wa taarifa za watumishi ili
kubaini wanaotumia vyeti vinavyofanana.
Kairuki alisema kwa kuzingatia maelezo ya Rais
Magufuli, ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara
ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, ilielekeza Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta) kufanya uhakiki wa vyeti vya kidato cha
nne, sita na ualimu.
Alitoa mfano wa nchi zilizowahi kufanya ukaguzi
kama huo kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, lakini
haikuweza kuwafikia watumishi wote kwa wakati
mmoja.
Akifafanua kilichogundulika kwenye ukaguzi,
alisema kati ya watumishi 400,035 waliokaguliwa,
376,969 wamebainika kuwa vyeti vyao ni halali
ambao ni sawa na asilimia 94.23, wengine 9,932
sawa na asilimia 2.4 wameghushi.
“Alama za siri pamoja na mhuri uliopo katika
vyeti hivyo haufanani na vyeti husika
vilivyotolewa na baraza hilo, kundi la tatu ni
wenye vyeti vyenye utata ambao ni 1,538 sawa
na asilimia 0.3 na vyeti hivyo vinatumiwa na
watumishi 3,076. Hii inamaanisha kuwa cheti
kimoja kinatumika na watumishi zaidi ya mmoja
na vingine watumishi wawili hadi watatu.
“Kundi la mwisho waliowasilisha vyeti pungufu ni
11,596 sawa na asilimia 2.8. Waliwasilisha vyeti
vya kitaaluma. Inatutia shaka kwa sababu
haiwezekani ukaenda kupata sifa ya kujiunga na
vyuo vya kitaaluma haukuwa na cheti cha kidato
cha nne na sita, baraza limewataka waajiri
kuwasilisha vyeti hivyo ili wafanye uhakiki,”
alikaririwa Kairuki juzi wakati akikabidhi ripoti ya
awamu ya kwanza na pili.
Alisema kughushi cheti ni kosa la jinai na hatua
za kisheria zitachukuliwa si kwa waliogushi tu,
bali pia kwa mawakala wanaotengeneza na kuuza
vyeti.
Kwa mujibu wa Kairuki, kanuni za kudumu za
utumishi wa umma, zinasema mwombaji wa ajira
serikalini akitoa taarifa za uongo na zikathibitika
baada ya kuajiriwa, atachukuliwa hatua za
kinidhamu na jinai.chanzo mtanzania digital
0 comments :
Post a Comment