Kasi ya Rais magufuri
WAFANYABIASHARA wa Rwanda
wamepongeza hatua zinazochukuliwa na
Rais John Magufuli katika Bandari ya Dar
es Salaam, kwa kuimarisha ufanisi wa
bandari, kukuza biashara baina ya
Tanzania na nchi jirani.
Aidha wamesema tangu Rais Magufuli
aanze kuchukua hatua hizo, mizigo yao
imekuwa salama zaidi na wamefanikiwa
kuipata kwa urahisi tofauti na zamani
ambapo mingi ilikuwa ikipotea.
Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Mambo
ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine
Mahiga wakati akizungumza na waandishi
wa habari katika Ukumbi wa Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA).
Akizungumza baada ya kutua nchini
akitokea Kigali, Rwanda, Balozi Mahiga
alisema pia Rais wa nchi hiyo, Paul
Kagame amemhakikishia kuwa ataendelea
kushawishi wafanyabiashara wake
kutumia Bandari ya Dar es Salaam, ili
kukuza uhusiano wa kibiashara uliopo.
“Nilipata bahati ya kuzungumza na
wafanyabiashara wa kule... wamepongeza
sana hatua zinazochukuliwa na Rais
Magufuli pale bandarini kwa sababu
wanasema sasa hivi itawasaidia sana
kuhakikisha usalama wa mizigo yao,”
alisema Blozi Mahiga.
Alisema wafanyabiashara hao pia
wameomba mkutano wa pamoja na
wenzao wa Tanzania, ili kujadili masuala
mbalimbali, ikiwemo fursa za uwekezaji
ndani ya Rwanda na Tanzania.
Alisema Rais Kagame anaunga mkono
ujenzi wa reli itakayotumika kusafarisha
mizigo kwa kuwa ni njia mojawapo ya
kukuza uchumi wa nchi hizo mbili rafiki.
Akizungumzia safari yake hiyo, Balozi
Mahiga alisema, alienda nchini humo
kujadiliana masuala mbalimbali
aliyoagizwa na Rais Magufuli kwa Rais wa
nchi hiyo, ambapo walijadili masuala
matatu, ikiwemo machafuko
yanayoendelea Burundi.
Alisema kuhusu machafuko ya Burundi,
Rais Kagame alikanusha tuhuma
zinazotolewa na nchi hiyo pamoja na
jumuiya za kimataifa kuwa anahusika
katika kuchochea machafuko hayo.
Kwa mujibu wa Balozi Mahiga,
maandamano ya nchi nzima yaliyofanyika
wiki iliyopita nchini Burundi ya
kuishutumu Rwanda kuhusika na
machafuko nchini mwao, yalishitua nchi
za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
kutokana na baadhi ya maneno ya chuki
yaliyokuwa yakitolewa na wananchi hao
dhidi ya nchi hiyo.
Alisema hali hiyo, ilihofiwa kwamba
ingeweza kuvunja mazungumzo ya
kutafuta suluhu yanayoendelea.
“Nilimuuliza Rais Kagame kuhusu hili
suala, akasema hatachukua hatua yoyote
licha ya kwamba wananchi wake
wamemlazimisha kufanya kitu. Lakini
alisema atashiriki katika majadiliano ya
kutafuta suluhu ya Burundi. “Sisi tulikuwa
tunahofia kuwa huenda akachukua hatua
ambazo zingeweza kuleta matatizo na
hata mazungumzo yanayoendelea
kuvunjika, lakini ameniambia hatachukua
hatua yoyote inayoweza kusababisha
kuvunjika kwa uhusiano,” alisema Balozi
Mahiga.
Hata hivyo, alisema Rais Kagame
alilalamikia nchi yake kushutumiwa kwa
kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wakimbizi
wa Burundi, ili kuipindua Serikali ya nchi
hiyo na kutaka Jumuiya za Kimataifa,
kuwaondoa wakimbizi zaidi ya 70,000 na
kuwahamishia nchi nyingine za jirani.
“Aliniambia kuwa kuendelea kuwa na
hawa wakimbizi katika nchi yake,
kunaweza kumletea matatizo makubwa,
kwa sababu amekuwa akilaumiwa sana.
Hivyo kuliko lawama, ni bora hizi Jumuiya
za Kimataifa zikawaondoa wakimbizi,”
alisema.
Alisema kwa mujibu wa Rais Kagame,
Rwanda itaendelea kushiriki katika
mijadala mbalimbali ya kutafuta suluhu ya
Burundi na itahakikisha Burundi inakuwa
salama.
Jambo lingine walilozungumza na Rais
Kagame ni mkutano wa marais wa Nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotarajiwa
kufanyika mwisho wa mwezi nchini
Tanzania, ambapo pia alikuwa katika
hatua ya mwisho katika kukamilisha
ajenda na watakaoshiriki mkutano huo.
0 comments :
Post a Comment