Habari kutoka ikulu jumaa bwando asimamishwa kazi.soma zaid.
RAIS Dk. John Magufuli, amefanya mabadiliko
mengine Ikulu jijini Dar es Salaam kwa
kumwondoa aliyekuwa Mnikulu, Jumaa Bwando.
Vyanzo vya habari kutoka Ofisi ya Rais
vimesema Bwando, aliondolewa katika wadhifa
huo Machi 14, 2015, ambapo kwa sasa nafasi
hiyo inakaimiwa na mmoja wa maofisa wa juu
wa Ikulu.
Julai 10 mwaka jana, Bwando aliteuliwa kushika
wadhifa huo na Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete,
kuchukua nafasi ya Shaban Gurumo,
aliyeng’olewa baada ya kukiuka sheria ya maadili
ya viongozi wa umma inayokataza kiongozi wa
serikali kupokea zawadi zaidi ya zawadi
ndogondogo na ukarimu wa kawaida.
Kazi ya Mnikulu ni kusimamia majengo yote ya
Ikulu kwa maana ya shughuli za utawala. Yeye
ndiye anayehusika na usafi, samani na mapambo
yote katika ofisi hiyo kuu ya nchi.
Ni mtu anayeweza kuamua mwonekano wa Ikulu
uonekanaje, hata kupanga na kuamua aina ya
nguo, mashuka, mapazia yanayopaswa kutumiwa
na Rais. Kwa majukumu husika anapaswa amjue
vizuri Rais.
Hatua hiyo ya Rais Magufuli ni mwendelezo wa
mabadiliko aliyoanza kuyafanya Ikulu siku chache
baada ya kuingia madarakani.
Tayari amezifumua na kuziunda upya baadhi ya
ofisi za Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam
pamoja na kuwaondoa baadhi ya watumishi
ambao hawana ulazima katika mfumo wa
utumishi wa Ikulu.
Rais Magufuli alianza kufanya ukaguzi wa ofisi
moja baada ya nyingine zilizopo Ikulu, huku
akitaka maelezo ya kina kuhusu shughuli zake na
aina ya watendaji waliopo.
Katika ukaguzi huo, Rais Magufuli aliamuru
kufungwa mara moja kwa baadhi ya ofisi
alizobaini kuwa hazina tija na kwamba zina
watumishi ambao ni mizigo.
Baadhi ya ofisi zinazodaiwa kufungwa ni pamoja
na iliyokuwa ikishughulikia chakula cha Rais na
ile iliyokuwa ikijihusisha na kupokea wageni
binafsi wa Rais.
Wakati akifanya mabadiliko hayo, Ofisa mmoja
wa Ikulu alinukuliwa na gazeti hili akisema. “Rais
Magufuli alipoingia tu Ikulu alifanya ziara ya
kukagua ofisi zote zilizopo Ikulu, alitaka kujua
utendaji kazi wa ofisi hizo, lakini alipofika kwenye
kitengo maalumu cha lishe ya Rais, alisema
haoni umuhimu wa kuwepo kwa ofisi hiyo kwa
sababu suala la lishe yake siku zote
linasimamiwa na mkewe Janeth.
“Akaamuru ifungwe na watumishi wake
warejeshwe walikotoka. Ofisi nyingine aliyoamuru
ifungwe ni kupokea wageni binafsi wa Rais.
Alisema haoni tija ya kuwepo kwa ofisi hiyo kwa
sababu mgeni anatakiwa kufika Ikulu baada ya
kutoa taarifa, nayo aliamuru ifungwe,” alisema
ofisa huyo.
Taarifa zilisema aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha
Lishe Ikulu alirudishwa katika ajira yake ya awali
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, huku
watumishi wengine wakipelekwa Wizara ya Nchi,
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
MTANZANIA ilipomtafuta Kaimu Mkurugenzi wa
Mawasiliano Ikulu Gerson Msigwa, ili kupata
ufafanuzi wa suala hilo, alijibu kwa kifupi kuwa
“Nalifanyika kazi swali lako kisha nitakupatia
ufafanuzi baada ya muda,” alisema Msigwa,
ambapo baada ya muda alipopigiwa simu.
0 comments :
Post a Comment