IMF yafurahishwa na utendaji wa serikali ya Magufuri.
UJUMBE wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
umeridhishwa na juhudi zinazofanywa na Serikali
ya Rais John Magufuli katika kuongeza juhudi za
kupambana na rushwa. Hali hiyo itabadili
mtazamo wa awali kwamba utawala bora
ulishapotea nchini, kama ilivyoonekana katika
tafiti nyingi zilizofanyika.
Aidha, ujumbe huo unaunga mkono malengo ya
uchumi yaliyomo katika mwongozo wa Bajeti ya
mwaka 2016/2017 uliochapishwa, ambayo
yamezingatia uhalisia katika ukadiriaji wa
mapato.
Hayo yalielezwa katika taarifa ya shirika hilo,
iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana Dar es
Salaam baada ya kumalizika kwa ziara ya
ujumbe huo ulioongozwa na Mkurugenzi Msaidizi
na Mkuu wa IMF nchini, Herve Joly. Ujumbe huo
pia ulifanya tathmini ya nne ya Mpango wa
Ushauri wa Sera za Uchumi (PSI), ulioidhinishwa
na Bodi Tendaji ya IMF mwaka huu.
Ilieleza taarifa hiyo kuwa “ujumbe umeridhishwa
na juhudi zinazofanywa na serikali katika
kuongeza juhudi zaidi za kupambana na rushwa,
hali ambayo itabadili mtizamo wa awali kwamba
utawala bora ulikwishapotea nchini kama
ilivyoonekana kwenye tafiti nyingi zilizofanyika.”
Tangu aingie madarakani Novemba mwaka jana,
Rais John Magufuli na serikali yake
imejipambanua kwa kupambana na rushwa na
ufisadi kwa kuwachukulia hatua wakwepa kodi na
watendaji wa serikali ambao ni wala rushwa,
kuwapeleka mahakamani na kuwasimamisha kazi
kupisha uchunguzi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mwongozo wa bajeti
ya Tanzania kwa mwaka 2016/17 umezingatia
kupunguza kwa kiasi kikubwa nakisi ya bajeti na
matumizi ya kawaida ili kutoa fursa ya kuongeza
matumizi ya maendeleo. “Changamoto kubwa
katika kukamilisha bajeti ni kuhakikisha kuwa
matumizi yanaendana na mapato halisi.
Majadiliano yataendelea katika wiki chache zijazo
ili kufikia muafaka juu ya mfumo mzima wa sera
za uchumi ambazo zitapelekwa kukamilisha
mapitio ya nne ya mpango wa PSI,” ilieleza
taarifa hiyo.
Mapitio hayo ya mpango wa PSI na majadiliano
chini ya kanuni ya nne ya mkataba ulioanzisha
IMF, yanatarajiwa kujadiliwa na Bodi Tendaji ya
IMF mwaka huu. Majadiliano chini ya mpango wa
PSI pia yamelenga kwenye utekelezaji wa bajeti
ya mwaka 2015/2016 na mipango ya bajeti ya
mwaka 2016/2017.
Katika taarifa hiyo, Joly alisema mwenendo wa
uchumi umeendelea kuimarika kwani makadirio
yanaonesha kuwa Pato la Taifa kwa mwaka jana
lilikua kwa asilimia saba, huku shughuli zilizokua
kwa kasi ni ujenzi, mawasiliano, huduma za
kifedha na uchukuzi. “Mfumuko wa bei
umeendelea kubakia kwenye kiwango cha
tarakimu moja muda wote wa mwaka 2015 na
kufikia wastani wa asilimia 5.6, japokuwa
thamani ya Shilingi ilishuka kwa kiasi kikubwa
katika nusu ya mwaka,” alisema Joly.
Alisema majadiliano na serikali chini ya kanuni ya
nne ya mkataba wa IMF yalijikita kwenye namna
ya kuendeleza ukuaji wa uchumi kwa kiwango
cha juu unaozingatia utekelezaji wa vipaumbele
vya serikali bila kusababisha athari za kiuchumi.
Hata hivyo, mabadiliko makubwa ya kimfumo
yanahitajika ili kuboresha mfumo mzima wa
kiuchumi na kuongeza tija katika uzalishaji na
uwekezaji.
“Kumekuwa na mtazamo sawa wa maoni kwenye
maeneo ya vipaumbele vya maboresho ya
kiuchumi na jinsi serikali itakavyochangia katika
kuwezesha uchumi endelevu na unaoongozwa na
sekta binafsi,” aliongeza Joly. Alisema uboreshaji
wa sekta ya kilimo inayoajiri idadi kubwa ya watu
utasaidia kuongeza kipato cha watu wa vijijini na
hiyo kuchangia kupunguza umasikini.
Aidha, utatoa fursa ya ajira kwa sekta nyingine
za uchumi na kukuza viwanda mbalimbali
ikiwemo vya kusindika vyakula. Kipaumbele
kingine ni kuboresha mazingira ya kufanya
biashara, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa
nishati na miundombinu bora ya usafirishaji na
upatikanaji wa ardhi na mitaji.
Aidha, kuendelea kuimarisha hali ya kifedha ya
Shirika la Umeme (Tanesco) na kulipa
malimbikizo ya madeni ya huduma za gesi na
umeme ni muhimu katika kuwawezesha
wawekezaji binafsi kuendelea kuwekeza kwenye
sekta ya nishati. “Tanzania inaweza kunufaika
kwa kiasi kikubwa na kukamilika kwa soko la
pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo
litasaidia kuvutia mitaji na kukuza ushinda na
kuongeza ufanisi,” alisema.
Wakati huo huo, mapato ya serikali kwa mwezi
huu yamefikia Sh trilioni 1.4, kwa mujibu wa
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana, Dk Mpango alieleza mchanganuo
wa fedha hizo kuwa ni mapato ya kodi (Mamlaka
ya Mapato Tanzania -TRA) ni Sh
1,283,274,000,000, mapato yasiyo ya kodi Sh
77,504,000,000 na mapato yatokanayo na vyanzo
vya Halmashauri Sh 43,490,000,000, kufanya
jumla ya Sh 1,404,268,000,000.
“Tunatarajia pia kupata mikopo na misaada ya
mifuko ya ‘Basket’ na miradi ya maendeleo
kutoka kwa washirika wa maendeleo shilingi
71,200,000,000,” alieleza Dk Mpango. Akieleza
mchanganuo wa matumizi, Dk Mpango alisema
yametumika katika kulipa mishahara ya
watumishi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa,
watumishi wa Taasisi na Wakala za Serikali
pamoja na malimbikizo ya Sh 518,822,320 kwa
Taasisi na Wakala 24 na hasa sehemu kubwa
Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo jumla ya
mishahara ni Sh 582,043,000,000.
Alitaja matumizi mengine ni kulipia posho ya
chakula kwa ajili ya vyombo vya ulinzi na
usalama, ruzuku ya vyama vya siasa, posho ya
madaktari wanafunzi 1,608, Wizara ya Afya
ununuzi wa dawa na vifaa tiba, mikopo ya
wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa semista ya tatu,
kutekeleza mpango wa Elimu bure na mapato ya
ndani kwa Halmashauri kwa ajili ya miradi na
uendeshaji wa ofisi.
Mengine ni madeni ya watumishi wasio walimu
katika Halmashauri, miradi ya umeme, Wakala wa
Umeme Vijijini, Mradi wa Umeme Kinyerezi I,
Mradi wa Kufua Umeme Makambako – Songea,
malimbikizo ya madeni ya makandarasi wa
barabara, miradi ya maji, Mfuko wa Reli, fidia
kwa wananchi kupisha mradi wa Kurasini Trade
and Logistic Hub, Mradi wa Ununuzi wa Dawa na
Vifaa Tiba (ORIO) na Mfuko wa Kuchochea
Maendeleo ya Jimbo.
0 comments :
Post a Comment