Japani kuwekaza katika nishati ya umeme.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KOYO ya
Japan, Bw. Norio Shoji
Hayo yamesemwa jana jioni na Mwenyekiti na
Mtendaji Mkuu wa shirika la Koyo, Bw. Norio
Shoji wakati alipokutana na kufanya mazungumzo
na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ofisini kwake,
Magogoni, jijini Dar es Salaam.
“Tumepanga kuwekeza kwenye maeneo matano
ambayo mojawapo ni kujenga mtambo wa
kuchakata gesi kwa kutumia gesi asilia
inayozalishwa hapa nchini. Mtambo huu utakuwa
na uwezo wa kuzalisha megawati 1,000 za
umeme,” alisema.
"Pia tunao mpango wa kujenga mitambo ya
umemejua inayoweza kujiunganisha kwenye gridi
(on-grid/off grid solar power plants) kwa ajili ya
maeneo vijijini na yale yasiyofikika kwa urahisi
zaidi ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa
usambazaji umeme kwenye gridi ya Taifa ili
Tanzania iweze kuzalisha zaidi nishati hiyo na
kuiuza nchi jirani," aliongeza.
Bw. Shoji alimweleza Waziri Mkuu kwamba wana
nia ya kuwekeza pia katika sekta nyingine kama
kilimo, sayansi ya tiba (medical science),
usafishaji na uyeyushaji madini (refinery-
smelting), uzalishaji wa bidhaa za viwandani na
teknohama.
Akifafanua zaidi Bw. Shoji alisema shirika lake
kwa kushirikiana na makampuni mengine
makubwa ya Japan pamoja na Serikali ya nchi
hiyo wamedhamiria kuwekeza kwenye
miundombinu hiyo kwa sababu wanataka
Tanzania iwe ni kitovu (hub) cha uzalishaji na
iweze kulisha nchi jirani katika SADC na EAC.
Akitolea mfano, Bw. Shoji alisema mbali na
miradi mingine wanayotaka kuwekeza, gharama
za kuweka mtambo wa kuzalisha megawati 1,000
za umeme hazitapungua kiasi cha dola za
marekani bilioni moja (sawa na sh. trilioni 2.2).
Waziri Mkuu alimshukuru Bw. Shoji kwa nia yake
aliyoionyesha na akamtaka achangue eneo
mahsusi kwa sababu Tanzania inahitaji umeme
wa kutosha katika kutekeleza azma yake ya
kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kujenga
uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa
umaskini miongoni mwa wananchi wake.
Tunahitaji uwekezaji mkubwa kwenye nishati ya
umeme katika mikoa ya Kusini, ya Kaskazini, ya
Magharibi na hata mikoa ya kati,” alisema Waziri
Mkuu.
Kwa upande wake, Bw. Suleiman M. Nassor
alisema shirika la Koyo litafanya uwekezaji huo
kwa kushirikiana na kampuni ya SSF Limited
ambayo inajihusisha na masuala ya nishati.
“Tunashirikiana na shirika la Koyo pamoja na
Serikali ya Japan ili kuleta unafuu wa maisha
kwa Watanzania wenzetu,” alisema Bw. Nassor.
Tags: waziri mkuu
▪ Kassim Majaliwa
▪ Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KOYO ya Japan
▪ Bw. Norio Shoji
▪ SADC
▪ EAC
0 comments :
Post a Comment