Katika mpango wa kuimarisha nishati na madini wizara imetengewa sh.trilioni 1.22 katika bajeti 2016-2017.soma zaid.
WIZARA ya Nishati na Madini imetengewa Sh
trilioni 1.22 katika bajeti ya mwaka wa fedha
2016/17 huku fedha za miradi ya maendeleo
zikiwa ni asilimia 94 ya fedha hizo.
Pia katika kuongeza kiwango kikubwa cha
uzalishaji wa nishati, kuongeza mchango wake
katika Pato la Taifa, asilimia 98 ya Bajeti ya
Maendeleo imetengwa kwa ajili ya sekta ya
nishati.
Aidha, serikali imeongeza bajeti ya maendeleo ya
fedha za ndani kwa Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) kufikia Sh bilioni 534.4, huku wateja wa
umeme wa REA na Tanesco wakifikia 220,128.
Mbali na hayo, kiwango cha upatikanaji wa
huduma ya umeme kimeongezeka kufikia asilimia
40.
Hayo yalisemwa bungeni jana mjini hapa na
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo wakati akiwasilisha Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka
2016/17.
Profesa Muhongo alisema bajeti ya wizara kwa
mwaka 2016/17 ni Sh trilioni 1,22,583,517,000, na
kati ya fedha hizo, Sh 1,056,354,669,000 ni fedha
za miradi ya maendeleo sawa na asilimia 94.
“Kwa kuzingatia Ibara ya 43(a) ya Ilani ya CCM
ya mwaka 2015-2020 inayoelekeza serikali
kuongeza kiwango kikubwa cha uzalishaji wa
nishati ili kuongeza mchango wake kwenye Pato
la Taifa, asilimia 98 ya Bajeti ya Maendeleo
imetengwa kwa ajili ya sekta ya nishati,” alisema
Profesa Muhongo.
Alisema katika mwaka wa fedha 2015/16,
waliidhinishiwa na Bunge Sh bilioni 642.12, na
kati ya fedha hizo, Sh bilioni 502.30 sawa na
asilimia 78 ya bajeti yote zilikuwa ni bajeti ya
maendeleo.
“Hata hivyo, Bajeti hiyo iliongezeka kutoka
shilingi bilioni 642.12 hadi shilingi bilioni 762.12.
lengo la ongezeko ni kutekeleza miradi mikubwa
ya kufua umeme ukiwemo Mradi wa Kinyerezi II
– MW 240 ili kuimarisha upatikanaji wa umeme
nchini,” alisema Profesa Muhongo.
Megawati zaongezeka
Akizungumzia sekta ndogo ya umeme, alisema
uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini
umeongezeka kutoka megawati 1,226.24 Aprili,
2015 hadi kufikia megawati 1,461.69 Aprili, 2016
sawa na ongezeko la asilimia 19.
“Ongezeko hilo limechangiwa na mitambo ya
kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia baada
ya kukamilika kwa bomba la kusafirisha gesi
asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es
Salaam,” alisema.
Aidha, alisema mahitaji ya juu ya umeme
yameongezeka kutoka megawati 988.27
Desemba, 2015 hadi kufikia megawati 1,026.02
Machi, 2016 sawa na ongezeko la asilimia nne.
Kuhusu upatikanaji wa umeme nchini, alisema
kiwango cha huduma ya upatikanaji wa umeme
kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka.
“Watanzania waliofikiwa na huduma hiyo
wameongezeka kutoka asilimia 36 mwezi Machi,
2015 hadi kufikia takribani asilimia 40 mwezi
Aprili, 2016. “Ongezeko hilo limetokana na juhudi
za serikali za kusambaza umeme nchini kupitia
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco),” alisema Profesa
Muhongo.
Alisema kuanzia Julai, 2015 hadi Aprili, 2016
idadi ya wateja waliounganishwa na umeme wa
REA pamoja na Tanesco ni 220,128 sawa na
asilimia 88 ya lengo la kuunganisha wateja
250,000 ifikapo Juni mwaka huu. Umeme bila
MCC “Katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa
umeme vijijini, serikali imeongeza Bajeti ya
Maendeleo ya fedha za ndani kwa REA kutoka
shilingi bilioni 357.12 kwa mwaka 2015/16 hadi
shilingi bilioni 534.4 kwa mwaka 2016/17.
Tumeongeza asilimia 50 na hakuna fedha za
MCC (Shirika la Changamoto za Milenia) hapa,”
alisema Muhongo. “
Ongezeko hilo ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020.
Aidha, fedha za nje zilizotengwa kwa ajili ya
mradi huo ni shilingi bilioni 53.21 sawa na
asilimia tisa na hivyo kufanya jumla ya bajeti
yote ya REA kwa mwaka 2016/17 kuwa shilingi
bilioni 537.61.”
Mitambo kuongezwa Akizungumzia miradi ya
kuzalisha na kusafirisha umeme, alisema serikali
itatekeleza miradi mingi ambayo baadhi
itakamilika katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Alisema katika juhudi za kuongeza uzalishaji
umeme, serikali imepanga kuongeza mitambo
mingine ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi – I
Extension wa megawati 185.
Alitaja mingine ni Kinyerezi II megawati 240, huku
akitaja miradi iliyo katika hatua za mwisho za
maandalizi ya miradi ambayo ni Kinyerezi III
(megawati –MW 300), Rusumo Falls MW 80),
Malagarasi MW 45 na Kanoko MW 87.
Kuhusu miradi ya usafirishaji umeme, alisema
ujenzi wa mradi wa Iringa hadi Shinyanga wa
kilovolti 400 umefikia wastani wa asilimia 89,
ambao gharama zake ni Sh bilioni 387.5 na
utakamilika Septemba mwaka huu.
Alisema serikali inaendelea kutekeleza miradi ya
ujenzi wa njia za kusafirisha umeme zenye
uwezo mkubwa hususan kilovolti 400. Miradi
ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika
ifikapo mwaka 2019/20 aliitaja kuwa ni Singida –
Arusha – Namanga kv 400, Bulyahulu – Geita kv
220, Geita – Nyakanazi kv 220, North East Grid
kv 400 na Somanga – Kinyerezi kv 400.
Aidha, alisema mradi wa ujenzi wa njia ya
kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400
kutoka Somanga Fungu hadi Kinyerezi, Tanesco
imeshakamilisha ulipaji wa fidia kwa wananchi
wanaopisha mradi huu. “Hadi kufikia mwezi Aprili,
2016 shilingi bilioni 26.06 tayari zimelipwa na
Tanesco kwa watu 947 katika wilaya za Ilala na
Temeke,” alieleza.
Katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji na
usambazaji wa umeme nchini, mwaka 2014
Tanesco ilianzisha Kampuni Tanzu ya Tanzania
Concrete Poles Manufacturing Company Limited
(TCPCO), kwa ajili ya kujenga viwanda vya
kutengeneza nguzo za zege nchini.
“Baada ya kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa
viwanda hivyo, TCPCO inatarajia kuanza
uzalishaji wa nguzo za zege mwaka 2016/17,”
alisema.
Kuhusu punguzo la viwango vya bei za umeme,
Profesa Muhongo aliliarifu Bunge kuhusu punguzo
hilo lililoanza Aprili mosi, mwaka huu.
Alisema serikali imepunguza bei ya umeme kwa
kati ya asilimia 1.5 na 2.4, na pia imeondoa tozo
ya kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa umeme
ya Sh 5,000 na tozo ya huduma ya mwezi ya Sh
5,520 kwa wateja wa umeme wa Daraja la TI na
DI, ambao wengi wao ni wa majumbani.
“Hatua hii itawasaidia watumiaji wadogo wa
umeme mijini na vijijini kumudu gharama hizo,
hivyo kuboresha shughuli za kijamii na kiuchumi,”
alisema Profesa Muhongo aliyerejea katika
wizara hiyo baada ya kuwahi kuiongoza katika
Serikali ya Awamu ya Nne.
Kuhusu gesi asilia, alisema kukamilika kwa ujenzi
wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara kupitia
Lindi hadi Dar es Salaam kumeongeza mchango
wa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa
kutumia gesi asilia kufikia asilimia 49.
Aidha, alisema uzalishaji wa umeme kwa kutumia
gesi asilia umewezesha gharama za uzalishaji
umeme nchini kupungua kutoka wastani wa Sh
262 hadi 229 kwa uniti moja ya umeme.
Profesa Muhongo alisema bomba hilo lenye urefu
wa kilometa 542 ni pamoja na mitambo ya
kusafisha gesi asilia katika maeneo ya Madimba
(Mtwara) na Songo Songo (Lindi). Mradi huo
ulizinduliwa rasmi Oktoba, 2015 na Rais wa
Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Akizungumzia shughuli za utafutaji gesi asilia,
alisema Kampuni ya Dodsal imekamilisha
tathmini ya kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa
katika kisima cha Mambakofi – I kwenye Kitalu
cha Ruvu Mkoa wa Pwani. Alisema tathmini hiyo
inaonesha uwepo wa gesi asilia kiasi cha futi za
ujazo trilioni (TFC) 2.17.
“Hivyo kufanya gesi asilia iliyogunduliwa nchini
hadi Mei, 2016 kufikia TCF 57.25 ikilinganishwa
na TCF 55.08 zilizokuwepo mwezi Aprili, 2015.
Kati ya kiasi hicho, TCF 47.13 zipo kwenye kina
kirefu baharini na TCF 10.12 zipo nchi kavu,”
alisema.
Akizungumzia usambazaji wa gesi asilia jijini Dar
es Salaam, alisema lengo la mradi huo ni kujenga
mtandao wa kusambaza gesi asilia kwa njia ya
mabomba na iliyoshindiliwa (CNG).
0 comments :
Post a Comment