Madawati yawakosesha usingizi ma' DC na RC.soma zaid.
VIONGOZI wa serikali hususan wakuu wa mikoa
na wilaya, wako katika heka heka za kutekeleza
kutengeneza madawati. Lengo ni kuhakikisha
hakuna mwanafunzi atakayekaa sakafuni, kabla
ya muda wa ukomo, waliopewa Rais John
Magufuli .
Wakati zikiwa zimebaki siku 39 kabla ya muda
huo wa ukomo ambao ni Juni 30 mwaka huu,
miongoni mwa maeneo ambayo gazeti hili
limefanya ufuatiliaji, imeshuhudiwa mikakati
mbalimbali ikitumika kwa ajili ya kupata fedha za
utekelezaji wa agizo ikiwamo kuangukia
wahisani.
Baadhi ya wakuu wa mikoa wameelekeza
halmashauri zao, kuhakikisha mapato ya vyanzo
vya ndani yanaelekezwa kwenye utengenezaji wa
madawati huku wengine wakishawishi wananchi
kuchangia kwa hiari kutekeleza agizo.
Hata hivyo, katika mchakato huo wa kutekeleza
matakwa ya agizo, baadhi ya maeneo
yamebainika kufanya uchakachuaji kwa
kutengeneza madawati kwa kutumia mabanzi
badala ya mbao ambao hata hivyo, umeshtukiwa
na viongozi wa serikali wa maeneo husika.
Uchakachuaji Vitendo vya matumizi ya mabanzi
badala ya mbao kutengeneza madawati,
vimebainika mkoani Tabora, ambako Mkuu wa
Mkoa, Aggrey Mwanri amebaini hilo na kuagiza
halmashauri zote zenye kufanya hivyo kuacha
mara moja.
Mwanri alibaini hayo hivi karibuni, alipofanya
ziara katika wilaya za Igunga na Nzega, ambako
aliagiza viongozi kufuatilia na kuhakikisha fundi
yeyote atakayebainika kutengeneza madawati
kwa kutumia mabanzi, asilipwe fedha.
Mwanri alisema ni jambo la aibu, kuona madawati
yakitengenezwa kwa mabanzi wakati mbao zipo.
Aliahidi kurudi wilayani Igunga na Nzega, kupiga
kambi kuhakikisha utengenezaji madawati
unakamilika muda uliopangwa.
Aidha aliagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri
ya wilaya ya Igunga, Alois Kaziyaleli kuhakikisha
fedha zote zitokanazo na makusanyo ya vyanzo
vya halmashauri, zinapelekwa katika utengenezaji
wa madawati. Mkuu wa Wilaya ya Igunga,
Zipporah Pangani, Mwenyekiti wa Halmashauri,
Peter Onesmo na Mkuu wa Wilaya ya Nzega,
Jackilin Liana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Mji Mdogo wa Igunga, Jeremia Jomanga kwa
nyakati tofauti, walimhakikishia Mwanri kuwa
ifikapo Mei 30, watakuwa wamekamilisha
utengenezaji madawati katika shule zote za
wilaya ya Igunga.
Kulingana na taarifa ya Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Nzega iliyotolewa
kwenye kikao cha Baraza la Madiwani,
Halmashauri imeidhinisha Sh milioni 100 kwa ajili
ya kutengeneza madawati kabla ya muda wa
ukomo. Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri
hiyo ya Nzega, Emanueli Kitundu, alisema
Januari mwaku huu kulikuwa na upungufu wa
madawati 40,000, lakini mwezi huu upungufu ni
madawati 10,000.
Wahisani waokoa jahazi Miongoni mwa maeneo
ambayo wahisani mbalimbali wamejitolea kuokoa
jahazi la upatikanaji madawati ni mkoani
Manyara, ambao ni moja ya mikoa 19
inayopakana na hifadhi 16 za taifa, iliyopokea
fedha kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa)
. Tanapa ilitoa madawati 16,500 yenye thamani
ya Sh bilioni moja kuunga mkono mkakati wa
serikali. Hundi za fedha hizo zilitolewa kwa
wakuu wa mikoa 19 mkoani Arusha mbele ya
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Madawati hayo yatasambazwa katika shule za
msingi za wilaya 55 zinazopakana na hifadhi
hizo. Vile vile hivi karibuni, kampuni za Tanzania
Bundu Safaris na Rungwa Game Safaris,
zilikabidhi madawati 90 kwa shule ya msingi
Loiborsiret wilayani Simanjiro. Akipokea
madawati hayo juzi, Mkuu wa Wilaya ya
Simanjiro, Mahmoud Kambona, alishukuru
kampuni hizo na kusema huu ni wakati wa jamii
ya wafugaji kupata elimu.
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro pia
imepata wahisani wakiwemo Ubalozi wa Japan,
ambao wamewatengenezea madawati 212 .
Akitoa taarifa hivi karibuni kwa Mkuu wa Mkoa
wa Morogoro, Dk Kebwe Steven, Mkurugenzi wa
Manispaa hiyo, Theresia Mahongo alisema
wamejipanga kukamilisha utengenezaji wa
madawati 6,672 kabla ya Juni 30, mwaka huu.
Alisema mahitaji ya madawati katika shule za
msingi ni 16,244, yaliyopo ni 12, 572 na upungufu
ni madawati 6,672 sawa na asilimia 34. “
Tumepata wahisani wa kututengenezea madawati
212 kutoka Ubalozi wa Japan na wengine ili
kukamilisha madawati,” alisema Mahongo. Vile
vile manispaa imepata kibali cha kuvuna miti
sita, itakayowezesha kupasua mbao 9,000
zitakazotengeneza madawati 300.
Aidha alisema pia imetengwa bajeti ya fedha kwa
ajili ya madawati. Manispaa ya Moshi Mkurugenzi
wa Manispaa ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro,
Jeshi Lupembe alisema halmashauri imetenga Sh
milioni 20 zitakazotengeneza madawati 500 na
kufanya madawati yaliyotengenezwa na
halmashauri kuwa 750 na yaliyobaki 600
yatatolewa na wadau mbalimbali.
Alisema wadau mbalimbali waliojitokeza kusaidia
kuchangia madawati na idadi kwenye mabano ni
Kampuni ya vinywaji baridi ya Bonite, walioahidi
kutoa madawati 100, Benki ya Ushirika Mkoa wa
Kilimanjaro-KCBL (100), Chama cha Walimu na
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa
madawati 20 na wadau wengine.
Alisema halmashauri imeshatoa Sh milioni 10 na
kuomba kibali cha kukata miti mitano kwa ajili ya
utengenezaji wa madawati 250 na vitanda 150
katika shule ya Moshi ufundi ambayo ndiyo
ilikuwa na upungufu mkubwa.
Dar yaandaa uchangishaji
Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ofisa
Elimu wa Mkoa , Raymond Mapunda alisema
mkoa huo umejitahidi kupunguza uhaba wa
madawati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,
ingawa bado upo upungufu.
Alisema ili kumaliza tatizo hilo, wako kwenye
maandalizi ya mwisho ya kualika wadau kwenye
chakula cha jioni, hafla iliyopangwa kuzinduliwa
kati ya Juni 2 na 3 mwaka huu ili kuwashirikisha
wadau na wahisani mbalimbali.
“Kama mkoa tuna mambo makubwa matatu
tunayafanya ili kuhakikisha tunamaliza tatizo la
miundombinu ya elimu hasa kwa upande wa
madawati na vyumba vya madarasa, na jambo
mojawapo ni hilo la kuzindua uchangiaji wa vitu
hivyo kupitia chakula cha jioni tunachoandaa”,
alisema Mapunda.
Alisema mkoa una upungufu wa madawati 94,030
kwa shule za msingi na sekondari. Kwa upande
wa vyumba vya madarasa, kuna upungufu wa
vyumba 8,317. Akichanganua, Mapunda alisema
katika shule za msingi, madawati yaliyopo ni
102,175 na upungufu ni 66,301 huku upande wa
sekondari kuna viti na meza 99,189 na upungufu
ni viti na meza 27,729.
Hata hivyo alisema mwitikio wa wadau kuchangia
miundombinu hiyo ni mkubwa. Hivi karibuni
Umoja wa watoa huduma ya usafiri wa daladala
jijini hapo, wameahidi kuchangia madawati 100.
Mgawanyo huo ni kama ifuatavyo, wilaya ya Ilala
wamepata Sh milioni 323, Temeke, 391 na
Kinondoni 391. Halmashauri zenyewe zimetakiwa
kujitengea fedha kutoka vyanzo vyao kwa ajili ya
kununua madawati.
Wananchi wachangishana Mkoani Simiyu, wakazi
wa kijiji cha Luguru wilayani Itilima, katika
kuunga mkono mkakati huo, wameamua
kuchangishana Sh 10,000 kila kaya kwa ajili ya
kutengeneza madawati 380 ya shule ya msingi
kijijini hapo.
Mwenyekiti wa kijiji, Dolnad Aloyce alisema
waliwahamasisha wananchi kupitia mkutano wa
hadhara kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo. Kwa
upande wa Wilaya ya Bariadi, Katibu Tawala wa
Wilaya ya Bariadi, Albert Rutahiwa, alisema
“Tumebakiza siku 42 (sasa 39) kukabidhi
madawati , hivyo wote kwa ujumla wetu jukumu
letu ni moja tuhakikishe upatikanaji wa mawadati
ifikapo Juni 30’’.
Taarifa kutoka mkoa wa Pwani, zinasema wilaya
ya Mkuranga hadi sasa, imefanikiwa kutengeneza
madawati 5,043 kwa ajili ya shule za msingi na
sekondari. Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Abdalla
Kihato alitoa taarifa hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa
Pwani, Evarist Ndikilo aliyekuwa ziarani humo.
Kihato alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba
hadi Juni 30, hawana wasiwasi tatizo la
wanafunzi kukaa chini litakuwa limekwisha kwani
wanashirikiana na wadau mbalimbali kutengeneza
madawati. Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huo
wa Pwani, Ndikilo mkoa huo ulikuwa una
upungufu wa madawati 43,047 kwa shule za
msingi lakini kwa jitihada zilizopo, tatizo
limepungua kwa kiwango kikubwa.
Vile vile, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku
Galawa ameuhakikishia umma kuwa tatizo la
uhaba wa dawati kwenye halmashauri zilizopo
mkoani kwake litamalizika kabla ya Juni 30.
Alisema kwa mkoa mzima wa Songwe mahitaji
ya madawati ni 63,537 ambapo yaliyopo ni 49,692
hivyo pungufu ni madawati 11,804.
Imeandikwa na Lucas Raphael, Igunga, John
Gagarini, Kibaha, Joachim Nyambo, Mbozi,
Kareny Masasy, Itilima, John Nditi, Morogoro,
Ikunda Erick, Dar es Salaam na Arnold Swai.chanzo habar leo.
Moshi
0 comments :
Post a Comment