Rais john magufuli awapa somo wawekezaji.soma zaid.
RAIS John Magufuli amesema Serikali ya Awamu
ya Tano, imejipanga kuwasaidia na kuwaunga
mkono wawekezaji wote wa ndani,
watakaoanzisha viwanda nchini ikiwa ni pamoja
na kuwahakikishia ulinzi wa viwanda vyao.
Pia amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha
anatengeneza mazingira yatakayowapunguzia
kwa kiasi kikubwa kodi wawekezaji wa ndani na
kupandisha kodi zaidi kwa bidhaa zinazoingia
kutoka nje ya nchi.
Dk Magufuli aliyasema hayo Dar es Salaam jana
katika mkutano wa mwaka ulioandaliwa na
Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kwa ajili ya
utoaji wa Tuzo za Rais kwa wazalishaji bora
nchini.
Alisema Tanzania ni nchi yenye utajiri wa
rasilimali, fursa ya masoko, nguvukazi na
mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo kipaumbele
kikubwa kitakuwa ni kuhakikisha wazalendo
wanapata fursa ya kufungua viwanda kwa wingi
na kutumia ipasavyo fursa hiyo.
“Mchango wetu Afrika kiuchumi duniani uko chini
ya asilimia tano, sasa ili tuweze kufikia malengo
ya kukua zaidi kiuchumi, Afrika hatuna budi
kufanya mageuzi ya sekta ya viwanda,”
alisisitiza.
Alisema endapo wafanyabiashara wa Tanzania
watawekeza na kuanzisha viwanda nchini,
watapata faida kubwa, wataongezea nchi
mapato, kuingiza zaidi fedha za nje na
kutengeneza ajira kwa wingi.
Alisema kuendelea kutegemea na kutoa
kipaumbele kwa bidhaa za nje hakuna faida zaidi
ya hasara kwa Watanzania kwani pamoja na
bidhaa hizo wakati mwingine kuingizwa kwa njia
za panya na kuwa feki au bandia, pia
watengenezaji wake wako nje ya nchi.
Alisema kwa kuwa watengenezaji wake wako nje
ya nchi, Tanzania haipati mapato zaidi ya ushuru
wa kuingiza bidhaa hizo lakini pia ajira
zinazotengenezwa zaidi ni kwa nchi ambazo
bidhaa hizo zinatengenezwa.
Aliwataka Watanzania hasa watendaji
kuondokana na tabia ya wivu kwa kuwanyima
fursa wawekezaji wa ndani pindi wanapotaka
kuwekeza na badala yake kupendelea na
kuwaamini zaidi wawekezaji kutoka nje.
“Matokeo yake, tunakuwa na rasilimali nyingi
lakini tunashindwa kuziboresha, wanakuja watu
wa nje wanachukua mahindi yetu wanasaga na
kuuza Sudan Kusini kwa bei ya juu, tuacheni hii
dhambi ya wivu ya kunyima fursa pindi mmoja
wetu akitaka kuwekeza sehemu…”
“…nimeshamwambia Waziri wangu Serikali hii ya
Awamu ya Tano inatoa fursa mtu kuwekeza
popote hata kama ni mzalendo, ukitaka kuwekeza
kwenye mbolea, gesi, saruji, kilimo au mafuta
ruksa,” alisisitiza.
Alisema kwa sasa Tanzania ni nchi ya pili au ya
tatu Afrika kwa ufugaji wa ng’ombe lakini cha
kushangaza hakuna kiwanda cha kutengeneza
viatu, mabegi wala mikanda. “Ng’ombe wetu
hawa wanachukuliwa watu wanaenda
kutengeneza bidhaa hizi wanazirudisha na
kutuuzia kwa bei ya juu.”
Alisema uwekezaji katika sekta ya viwanda
ukikua nchini hata wakulima wa pamba, korosho,
kahawa na mazao mengine ya biashara
watazalisha kwa wingi na kupata faida kwa kuwa
watakuwa na soko la uhakika lakini pia viwanda
hivyo vitatengeneza ajira na kuuza bidhaa hiyo
kwa bei ambayo Watanzania wataimudu.
Alisema serikali yake imejipanga kuwaunga
mkono wawekezaji wa kizalendo watakaoanzisha
viwanda na nguvu kubwa imeelekezwa katika
uwekezaji wa viwanda vya uzalishaji utakaotumia
kwa wingi malighafi zinazozalishwa nchini.
Dk Magufuli alisema lengo la Serikali ya Awamu
ya Tano ni kuhakikisha kupitia sekta hiyo ya
viwanda ifikapo 2020 ichangie katika Pato la
Taifa kwa asilimia 40 lakini pia ajira
zitakazozalishwa kupitia viwanda pia zifikie
asilimia 40.
“Naamini jambo hili linawezekana kwa sababu
nchi yetu imebarikiwa kuwa na rasilimali
zinazowezesha kujenga uchumi wa viwanda,
tunayo ardhi ya kutosha, nguvu kazi, misitu,
samaki kupitia uvuvi, soko la uhakika kwa kuwa
tumezungukwa na nchi zisizo na maji,” alisema.
Aidha, alisema Tanzania ina fursa nzuri za
uwekezaji kwa kuwa iko katika ushirikiano wa
Afrika Mashariki na Jumuiya ya Nchi za Kusini
mwa Afrika (SADC) hivyo kuwa na uwezekano
wa soko la watu zaidi ya milioni 390.
Alisema nchi zote duniani zilizokuwa na hali
mbaya ya uchumi ziliweza kuendelea baada ya
kuwekeza zaidi nguvu zake katika sekta ya
viwanda na sasa nchi hizo ndio zinazoongoza
duniani kwa kuwa na uchumi mkubwa.
Alitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni China, Korea
Kusini, Thailand, Malaysia, Vietnam iliyochukua
mbegu za korosho nchini na sasa ndio
inayoongoza kwa uzalishaji wa zao hilo na
Mauritius inayoongoza duniani kwa uzalishaji
sukari.
Rais aliwaahidi wawekezaji wa ndani kuwa
serikali italinda viwanda vyote vya ndani kwa
kuhakikisha inaondoa mazingira yote yanayoweza
kusababisha vikose soko, vishindwe kuzalisha na
kufa.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili sekta ya
viwanda nchini, alisema kubwa ya miundombinu
tayari serikali inaifanyia kazi, na mwaka ujao wa
fedha imetenga Sh trilioni moja kwa ajili ya
kuanza ujenzi wa reli ya kisasa.
Aidha, alisema Tanzania iko katika mazungumzo
ya mwisho na Zambia kwa ajili ya kuifanyia
ukarabati reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na
Zambia (Tazara) pamoja na kujipanga kuondoa
kabisa kero ya umeme kupitia miradi mbalimbali
ya umeme inayoendelezwa nchini.
Kuhusu suala la utitiri wa tozo kwa wawekezaji
wa viwandani, Dk Magufuli alieleza kuwa serikali
imeshaunda kamati ya kitaifa kwa ajili ya
kuangalia mazingira ya tozo na endapo kutakuwa
na tozo zisizo na tija zilizolenga kuwanufaisha
wachache zitaondolewa.
“Ni kweli nchi yetu ina vikodi vingi hasa kwenye
mazao kama vile kahawa, pamba na korosho, na
ninafahamu kuna kodi nyingine ni kwa ajili ya
kuliwa na baadhi ya watu, hizi nitaziondoa. Ndio
maana wengine wananiita mkorofi lakini
ninasimamia haki na si lingine,” alisema.
Waziri Mwijage alisema serikali imeanza
kuonesha kwa vitendo dhima yake ya kuijenga
Tanzania ya viwanda kupitia Mpango wake wa
Maendeleo wa miaka mitano 2016/17 hadi
2020/25.
Mwenyekiti wa CTI, Dk Samuel Nyantahe
alimpongeza na kumshukuru Rais kwa kutambua
umuhimu wa sekta ya viwanda katika kujenga
uchumi na kutaja changamoto kadhaa ikiwemo
miundombinu, utitiri wa kodi, uingizwaji wa
bidhaa bandia na utitiri wa mamlaka za udhibiti.
0 comments :
Post a Comment