Sura 4 za Raisi john magufuli kumtumbua kitwanga.soma zaid.
JAMII ya Watanzania imetakiwa kujifunza sura
za Rais John Magufuli, kutokana na hatua yake
ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.
Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu hatua
hiyo ya Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja,
alisema Rais ametuma salamu kwa sura nne
kupitia utenguzi huo.
Sura ya kwanza kwa mujibu wa Minja, alisema
Rais amewakumbusha watumishi wote wa umma
kwamba uadilifu ni jambo muhimu mahali pa kazi,
na wanapaswa kuheshimu na kutekeleza
majukumu yao kwa kuzingatia muda na sio
kutumia muda huo vibaya.
Pili, Minja alisema Rais ametuma salamu kwa
walio karibu yake, kwamba uswahiba wao
hauhusiani na kazi ya nchi, hivyo suala la
kufahamiana si kigezo cha kiongozi avunjaye
maadili kuachwa, bali wanapaswa kutambua nchi
inaongozwa kwa Sheria na Katiba.
Akizungumzia sura ya tatu ya uamuzi huo, Minja
alisema Rais amewakumbusha Watanzania kuwa
haangalii muda gani amemteua kiongozi au muda
gani ametumikia nafasi aliyopewa, bali
kinachoangaliwa ni utendaji kazi wake kwa Taifa.
Aidha sura ya nne, imeelezwa kwamba Rais
ameoneshwa kuwa haendeshwi kwa siasa za
vyama kwa kuangalia wanasiasa watasema nini,
hasa wakati huu wa uwepo wa Sakata la
Kampuni ya Lugumi, na kusema alichoangalia ni
kosa limetendeka muda gani.
“Kwa kweli Rais kaonesha ukomavu wake,
ameonesha ni Rais mwenye msimamo, bila kusita
amefanya uamuzi sahihi, hakuangalia vyama vya
siasa vinasema nini, bali aliangalia maadili ya
utumishi wa umma yanasema nini na kuchukua
hatua,” alisema Minja.
Watumishi wengine
Kwa upande wake Profesa wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam na mchambuzi wa habari, Kitila
Mkumbo, alisema uamuzi huo wa Rais ni hatua
muhimu, na amefanya jambo kubwa na sahihi
hivyo mawaziri wengine wanapaswa kuwa
makini.
“Ni hatua kubwa, Rais amefanikiwa kuvuka hili,
ameonesha uwezo wake wa kufanya uamuzi na
sio kuangalia sura kwa minajili ya urafiki, au
kufahamiana, ukiwa kiongozi unapaswa
kujitambua hadhi yako na nafasi yako kwa jamii,”
alisema Profesa Mkumbo.
Alisema hatua hiyo imesaidia Rais kuondokana
na lawama ya Sakata la Kampuni ya Lugumi na
inaashiria kwamba taasisi nyingine za Serikali
zitafanya kazi zake mapema badala ya kumsubiri
Rais afanye kila kitu.
Profesa Mkumbo alitoa mfano kwenye utenguzi
huo na kusema Bunge lilikuwa na uwezo wa
kumzuia asiingie ndani ya ukumbi ule kwa hali
yake ya ulevi, ili asiiaibishe Serikali kama
ambavyo imeonekana, lakini hawakuchukua hatua
hadi Rais alipochukua.
“Sasa ni wazi kwamba Sheria za Kazi na Vileo
maeneo ya kazi zitaanza kufanya kazi, ili kila
mtumishi ajitambue na kufahamu wajibu aliopewa
ni dhamana na anatakiwa kutekeleza kwa
kuzingatia maadili,” alisema Profesa Mkumbo.
Jimboni nako watengue
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema
Kitwanga ameachishwa kazi kwa fedheha na
hata wapigakura wake kama sheria ingeruhusu
wangemwajibisha.
Alisema cheo ni dhamana na kwamba katika
nafasi aliyokuwa nayo ndani ya Baraza la
Mawaziri tena kwenye wizara nyeti, alipaswa
kuwa mfano wa kiongozi mwenye uadilifu na
haiba yake ifanane na hicho chombo.
“Rais katuma salamu nzito kwa wengine na
taasisi za umma, imetufundisha kuwa Rais
akikupa wadhifa, usimuangushe, huyu
kamuangusha Rais na Serikali, alipaswa
kuwajibishwa na amewajibishwa kwa wakati, bila
kushinikizwa,” alisema Dk Bana.
Alisema wananchi wanapaswa kumuelewa Rais
na kuacha kuzungumza maneno yasiyo na maana
kwani Kitwanga alipaswa kuwajibishwa kwa kosa
alilotenda kwa wakati huo la ulevi na Rais
amechukua hatua.
Dk Bana alisema kwa hatua hiyo ya Rais, ni wazi
kwamba wale wote wenye wadhifa katika
utumishi wa umma, wanapaswa kuheshimu na
kuzingatia misingi ya Maadili ya Utumishi wa
Umma na kama misingi hiyo huwezi kuitekeleza,
ni bora waache kazi mwenyewe.
Misingi ya Nyerere
Kwa upande wake Mhadhiri mwingine wa Chuo
hicho, Dk Bashiru Ally, alizungumzia suala hilo
kwa kurejea misingi ya Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere kuwa katika mambo muhimu
aliyoyajenga ni misingi ya utaifa na maadili ya
utaifa.
Alisema kiongozi ni hadhi na ni nafasi ya
heshima na kila kiongozi awe wa ngazi yoyote
kuanzia Serikali za Mitaa hadi urais, anapaswa
kutambua kuwa cheo ni dhamana na kina
masharti na maadili yake.
“Ni mara ya kwanza kwa rais kuonesha ukali,
ulevi ni jambo baya, linatakiwa kukemewa kwa
nguvu zote, ujumbe huu uende kwa taasisi zote
serikalini na kwa umma, pia walevi popote walipo
hizi salamu ziwafikie,” alisema Dk Bushiru.
Alisema kosa alilofanya Kitwanga lipo kwa
watumishi wengi wa umma na kwamba kwa
hatua hizo za Rais, Katibu Mkuu Kiongozi
anapaswa kupeleka salamu kwa taasisi zilizo
chini yake kuwakumbusha kwamba utumishi wa
umma unakwenda sambamba na maadili.
Swali kurudiwa
Kutoka bungeni, kitendo cha Kitwanga kujibu
swali akiwa mlevi, kimesababisha Serikali
kutakiwa kujibu upya swali hilo bungeni, huku
akimkasirisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Aidha, imefahamika kuwa watu wengi
‘walishitukia’ kuwa mbunge huyo wa Misungwi
mkoani Mwanza hakuwa ‘sawasawa’ wakati
akijibu swali bungeni Ijumaa asubuhi mjini hapa.
Uteuzi wa Kitwanga kwa wadhifa wa Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi umetenguliwa na Rais
John Magufuli juzi baada ya kubainika kuwa
waziri huyo aliingia bungeni na kujibu swali
linalohusu wizara yake akiwa amelewa.
Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano,
Ikulu, Gerson Msigwa juzi kuhusu kutenguliwa
uteuzi huo wa Kitwanga ilikuwa na aya mbili tu.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk
John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa
Charles Kitwanga kuanzia leo tarehe 20, Mei,
2016. “Rais Magufuli ametengua uteuzi huo
kufuatia kitendo cha Mheshimiwa Charles
Kitwanga kuingia bungeni na kujibu swali
linaloihusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
akiwa amelewa,” ilisema taarifa ya Kurugenzi ya
Mawasiliano, Ikulu.
Hali ilivyokuwa
Awali asubuhi, Kitwanga akijibu swali la Mbunge
wa Viti Maalumu, Devotha Minja (Chadema)
ambalo liliulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa
Mlimba, Suzan Kiwanga (Chadema). Katika swali
la nyongeza, Kiwanga alihoji Wilaya ya Kilombero
ina miaka 55 lakini polisi hawana nyumba
wamepanga na Jimbo la Mlimba wanaishi
kwenye nyumba za Tazara, hivyo serikali ipewe
miaka mingapi kujenga nyumba na vituo vya
polisi.
Kitwanga alijibu: “Kwani wewe una miaka
mingapi? Usiulize miaka ya kujenga nyumba za
Polisi na vituo. Amini tutajenga tu. Halafu wewe
ni rafiki yangu lazima nikujibu hivyo.” Hata hivyo,
majibu hayo na jinsi alivyokuwa akijibu,
yaliwashitua wengi wakiwamo waandishi wa
habari ambao hawakumwelewa vizuri Kitwanga.
“Hivi mbona Kitwanga leo yuko hivi? Yuko sawa
sawa kweli,” alihoji mwandishi mmoja wa habari.
Hata wakati wa jioni kabla ya baadaye
kutangazwa taarifa za kutenguliwa kwa wadhifa
wa Kitwanga, mwandishi mwingine ambaye
hakuwamo ndani ya ukumbi wakati Kitwanga
anajibu maswali, aliuza: “Jamani hivi asubuhi
wakati Kitwanga anajibu maswali alikuwaje.”
Alijibiwa na wenzake kwamba hakuonekana kuwa
sawasawa, na mwingine akaenda mbali zaidi na
kueleza kwa alionekana amelewa. Waziri huyo
alitembelewa na wapigakura wake kutoka jimboni
na walitambulishwa miongoni mwa wageni
waliofika bungeni juzi.
Kuitwa na Waziri Mkuu
Lakini baada ya hali hiyo kutokea, inaelezwa
kuwa baada ya kipindi cha Maswali na Majibu
Bungeni, Kitwanga aliitwa ofisini kwa Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye awali alikuwamo
bungeni.
Inaelezwa Waziri Mkuu alikuwa amekasirika sana
kutokana na kilichofanywa na waziri huyo na
hakuwa yule aliyezoeleka miongoni mwa watu
wake.
Kilichoendelea kati yao hakikufahamika, lakini
kuna kila dalili alizungumza na Dk Magufuli
kutokana na kitendo cha uvunjifu wa maadili ya
utumishi kilichofanywa na Kitwanga, na
kusababisha rais kutengua uteuzi wake.
Katika taarifa yake juzi usiku saa chache baada
ya kutimuliwa Kitwanga, Waziri Mkuu Majaliwa
alisema uamuzi uliofanywa na Dk Magufuli
umefuata kanuni za utumishi wa umma ambao
unakataza mtumishi kulewa akiwa kazini.
“Zipo sheria za utumishi ambazo mtumishi
hatakiwi kunywa pombe na wala hapaswi kulewa
akiwa kazini… mtumishi anapaswa kuwa na akili
timamu inamwezesha kufanya kazi za Serikali,”
alisema Majaliwa akijibu swali la mwandishi wa
TBC1 aliyetaka kujua ukweli wa taarifa za
kutimuliwa Kitwanga. “Ni kweli Mheshimiwa Rais,
Dk John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Charles
Kitwanga kuanzia leo tarehe 20 Mei, 2016 baada
ya kuonekana amelewa wakati wa kazi. Na hili
lilibainika pale alipokuwa akijibu maswali ya
wizara yake leo asubuhi,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, kutokana na majibu ya Kitwanga
kutoridhisha, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini
(Chadema) aliomba mwongozo wa Spika kwamba
swali la Minja halikujibiwa kwa ukamilifu.
Kwa kawaida, maswali bungeni hujibiwa na naibu
mawaziri kwa kila wizara, na endapo wizara
haina naibu, hujibiwa na waziri husika. Na
endapo wote hawapo, huteuliwa naibu waziri
mwingine kujibu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Hamad Yussuf Masauni hakuwapo bungeni juzi
na imefahamika kuwa yuko safarini kikazi katika
moja ya mikoa nchini. Kwa mujibu wa Naibu
Spika Dk Tulia Ackson, swali la Minja lilikuwa:
“Askari wa Jeshi la Polisi na Magereza wanaishi
katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi,
ikilinganishwa na kazi zao wanazozifanya kwa
jamii? Je, serikali ina mpango gani wa
kuwaboreshe askari makazi.”
Akitoa majibu ya mwongozo huo juzi usiku kabla
ya kuahirisha Bunge, Dk Ackson alisema
ilibainika kuwa si kwamba swali la Minja
halikujibiwa kikamilifu na Waziri, ila majibu yake
hayakutoa mchanganuo wa nyumba ngapi
zitajengwa kwa upande wa askari wa Jeshi la
Magereza.
“Kwa kuzingatia Mwongozo ulioombwa na
Mheshimiwa Mbunge, na uzito wa swali
lililoulizwa kiti kimeamua kuelekeza swali hilo
lirudiwe kuulizwa katika kikao cha tarehe 23 Mei,
2016. “Ili serikali iweze kutoa majibu kwa
ufasaha zaidi ikiwa ni pamoja na kutoa
mchanganuo wa nyumba ngapi za Askari
Magereza zitajengwa, na katika maeneo gani,”
alisema Naibu Spika.
Kitwanga aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na
Nishati na Madini anakuwa waziri wa kwanza
kutimuliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Mapema wiki hii, akifanya majumuisho ya hotuba
yake ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/17,
alisema yeye anatambulika kwa jina la ‘Bwana
STK.’ “Niko serikalini kwa miaka 35 sasa.
Natambulika kama Mr STK, Mzee wa STK –
Sheria, Taratibu na Kanuni.
Nimewasilisha fomu yangu Sekretarieti ya Maadili
kwa mara ya kwanza mwaka 1998. “Hivyo
vinatosha kuwapa taarifa mimi ni mtu wa aina
gani, sipendi kusema, napenda kutenda,” alisema
Kitwanga ambaye amekuwa akitajwa kuwa
mmoja wa marafiki wa karibu wa Dk Magufuli.chanzo habar leo.
0 comments :
Post a Comment