Chama cha wananchi CUF zanzibar mashakani kufutwa.
CHAMA KIKUU CHA UPINZANI ZANZIBAR CUF
KUCHUNGUZWA KIKIBAINIKA KUHUSIKA NA
KUCHOCHEA UBAGUZI KUFUTWA.
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar
(BLW), wamepitisha hoja binafsi wakitaka Chama
cha Wananchi (CUF), kichunguzwe na kikibainika
kinahusika na vitendo vya ubaguzi ulijitokeza
Zanzibar, kifutwe.
Wajumbe hao hawakuishia hapo pia, wanataka
Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad
achukuliwe hatua za kisheria.
Hoja hiyo imewasilishwa kwa dharura na
Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae Mohamed said
Mohamed (Dimwa) na kuungwa mkono na
wajumbe baada ya kujadiliwa.
Mbele ya Spika wa Baraza la Wawakilishi (BLW),
Zuberi Ali Mouludi hoja ziliibuliwa za kutakiwa
Msajili wa Vyama vya Siasa kuchunguza vitendo
vinavyodaiwa kufanywa na viongozi wa CUF
baada ya kufanyika uchaguzi wa marudio ambao
waliususia.
Hatua ya CUF kususia uchaguzi wa marudio kwa
madai haukuwa halali kwa mujibu wa katiba ya
Zanzibar na sheria ya uchaguzi namba 11 ya
mwaka 1984, imesababisha kukwama kuundwa
kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).
Wajumbe watano waliyochagia hoja hiyo na
kueleza kuwa hali ya kisiasa ya Zanzibar si
shwari kutokana na kasi ya wananchi kubaguana
katika nyumba za ibada, misiba, harusi na
kunyimana huduma za madukani na ndani ya
vyombo vya usafiri kwa sababu ya chuki za
kisiasa.
Chimbuko la ubaguzi huo pamoja na kuhujumiwa
mali za serikali na wananchi kama utekelezaji wa
mpango wa kutomtabua Rais wa Zanzibar Dk Ali
Mohamed Shein na viongozi wote, lilidaiwa ni
agizo la Katibu Mkuu wa CUF kwa wananachama
wa chama hicho.
Wawakilishi hao wanataka Maalim Seif,
achukuliwe hatua za kisheria kwa kuhatarisha
amani na umoja wa Wazanzibari kutokana na
kampeni zake za kuwataka wananchi kugoma
kulipa kodi pamoja na kutoshirikiana na serikali
na wana CCM.
Hoja binafsi imesema waathirika wakubwa ni
wana CCM ambao wanatengwa katika nyumba za
ibada, misiba, harusi pamoja na kupata huduma
nyingine za kijamii kama usafiri wa daladala.
Kuelekea Mwezi wa Ramadhani, waumini
wanahitajika kufanya ibada pamoja lakini, hali
imekuwa tofauti hasa katika kisiwa cha Pemba,
ambako ni ngome kuu ya kisiasa ya CUF.
Madhara ya mpasuko wa kisiasa yameanza pia
kuathiri Watanzania Bara ambao pia wameanza
kutengwa hasa wanaoishi katika nyumba za
kupanga wakionekana kama ni sehemu ya wana
CCM Zanzibar.
Lakini SMZ katika kupambana na tatizo hilo,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Mohamed Aboud Mohamed anasema
watawanyang’anya leseni za biashara
wafanyabiashara watakaopatikana na hatia ya
kutoa huduma kwa ubaguzi au kujaribu kufanya
mgomo kwa sababu za kisiasa.
Aliwambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
kuwa, SMZ imempiga marufuku Maalim Seif
kuzunguka na misafara mirefu ya magari na
kufanya mikusanyiko ya watu katika matawi au
sehemu anazopita bila ya polisi kuwa na taarifa
au kuwa na kibali.
Tayari watu watatu wameripotiwa kujeruhiwa
katika vurugu zilizotokea vijiji vya Kivunge,
Mkwajuni na Bumbwini baada ya askari wa
kutuliza ghasia kutumia mabomu ya kutoa
machozi, kuwatawanya wafuasi wa CUF
waliojitokeza kumpokea Maalim Seif akiwa katika
ziara yake ya kwanza tangu kufanyika uchaguzi
wa marudio.
Mpasuko huo uliibuka baada ya Mwenyekiti wa
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim
Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa
mwaka jana kwa madai ulikuwa na udaganyifu
pamoja na waangalizi wa ndani na nje kudai
ulikuwa uchaguzi huru na wa haki.
Baadhi yao ni Umoja wa Ulaya(EU) Jumuiya ya
Madola (Commonwealth), Marekani na
Uingereza. Uamuzi wa ZEC unapigwa na CUF
ambao walisusia uchaguzi wa marudio wa Machi
20, 2016.
Tunajiuliza kwanini wananchi wateswe kwa
maamuzi yaliyofanywa na Jecha na kufikia
kunyimwa huduma muhimu za kijamii pamoja na
kuhujumiwa mali zao yakiwamo majengo na
mashamba ya mazao?
Lazima tukumbuke kwamba vitendo vya ubaguzi
vinavyoendelea kufanyika Zanzibar hasa kisiwani
Pemba havikubaliki katika misingi ya haki za
binadamu na utawala bora.
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana
hakuharibiwa au kufutwa na wananchi wa
Zanzibar tangazo la kuubatilisha lilitolewa na
Mwenyekiti wa ZEC, kwanini waadhibiwe
Wazanzibari au Wabara (Watanganyika),
wasiokuwa na hatia?
Pamoja na wawakilishi kutaka CUF ichunguzwe
na Katibu Mkuu achukuliwe hatua za kisheria si
ufumbuzi wa kumaliza mpasuko wa uchaguz
mkuu wa Zanzibar.
Unaweza kuifuta CUF lakini watu wanaoiunga
mkono huwezi kuwafuta wataendelea kuwepo na
kubakia na misimamo yao, cha muhimu ni
kutafuta maelewano kwa njia za kidiplomasia na
amani badala ya nguvu za dola.
Maridhiano bado ni jambo muhimu katika
kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi
mkuu wa Zanzibar kwa vyama vya CCM na CUF
pamoja na kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa
marudio na kuundwa kwa serikali ya awamu ya
saba Zanzibar.
Kuwataka wahisani kuongeza vikwazo au
wananchi wasilipe kodi hakusaidii, wanyonge
ndiyo wataumia kwa ugumu wa maisha kwa
kukosa misaada na wala si viongozi wakuu.
Chanzo : Nipashe
0 comments :
Post a Comment