Mohammed Dewji ameahidi kumuunga mkono Rais magufuli.soma zaid.
LICHA ya kuongoza kwa kutoa ajira katika sekta
binafsi nchini, bilionea kijana zaidi Afrika,
Mohammed `Mo’ Dewji ameahidi kumwaga ajira
zaidi na kufikia 100,000 ili kumuunga mkono Rais
John Magufuli la kukabili tatizo la ajira.
Kwa sasa, Dewji anayemiliki mtandao wa
kampuni zilizopo chini ya Kampuni ya
Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL)
, ameajiri Watanzania 28,000 katika kampuni zake
zaidi ya 31. Ni mwajiri mkubwa wa pili nchini
baada ya Serikali.
Alikaririwa na jarida maarufu la uchumi duniani,
Forbes la Marekani toleo la wiki hii akisema
ameguswa na uchapakazi wa Rais Magufuli,
hivyo anajiona ana jukumu la kufanya katika
kuisaidia Serikali ya Awamu ya Tano baada ya
Rais kuonesha dhamira ya dhati ya kuinua
uchumi wa nchi.
Alisema anakusudia kuajiri Watanzania 100,000
ndani ya miaka minne, ili aweze kutimiza ndoto
yake ya kurudisha kwa wananchi sehemu kubwa
ya faida katika biashara zake, lakini pia
kuwakwamua vijana na Watanzania waweze
kujitegemea na kupiga hatua kimaendeleo, hali
itakayosaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja
mmoja na taifa kwa ujumla.
Aliyasema hayo ikiwa ni takribani wiki moja tangu
kampuni tanzu ya MeTL Group ilipong’ara katika
Tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa Mwaka 2015
na kutwaa tuzo tatu katika hafla iliyofanyika Dar
es Salaam.
Katika tuzo hizo zilizoandaliwa na Shirikisho la
Wenye Viwanda Nchini (CTI) na kuhudhuriwa na
Rais Magufuli, kampuni zilizo chini ya MeTL, Star
Oils (T) Ltd inayohusisha na bidhaa za petroli,
East Coast Foods & Fats inayozalisha bidhaa za
mafuta na sabuni na kiwanda cha nguo cha 21st
Century cha Morogoro zilitwaa tuzo.
“Ninakusudia kuongeza dola milioni 500 zaidi
(shilingi trilioni moja) katika biashara zangu ndani
ya miaka minne niweze kuajiri zaidi ya watu
100,000, wengi wakiwa Watanzania,” alisema
bilionea huyo mwenye umri wa miaka 41 ambaye
yumo katika orodha ya mabilionea 24 wakubwa
zaidi Afrika, lakini akiwa namba moja kwa
upande wa vijana.
Alisema miongoni mwa maeneo yatakayozalisha
ajira mpya ni pamoja na kiwanda kipya cha
sukari anachokusudia kukianzisha, akisema si
kwamba kitazalisha sukari pekee, bali pia
uzalishaji wa nishati ya umeme.
Rais Magufuli, akizungumza wakati wa Tuzo za
Rais za Mzalishaji Bora wa mwaka 2015, alisema
serikali yake imejipanga kuwasaidia na kuwaunga
mkono wawekezaji wote wa ndani,
watakaoanzisha viwanda nchini ikiwa ni pamoja
na kuwahakikishia ulinzi wa viwanda vyao.
MeTL Group yenye utajiri wa zaidi ya dola bilioni
1 (sh trilioni 2.2) ilianzishwa mwanzoni mwa
miaka ya 1970 na imejikita katika sekta za
biashara, kilimo, uzalishaji, nishati na petroli,
huduma za fedha, huduma za simu, usafirishaji,
usambazaji, majengo na miundombinu.
0 comments :
Post a Comment