Selikari imewatumbua wakurugenzi wake idara ya misitu.soma zaid.
SERIKALI imemuondoa katika nafasi yake
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania
(TFS), Gerald Kamwenda na wakurugenzi
wenzake, katika jitihada za kufumua na kusuka
upya shirika hilo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne
Maghembe, ametangaza hatua hiyo ya serikali
jana alipokutana na vyombo vya habari na
kuongeza kuwa, watumishi wengine 41
wamehamishwa vituo vya kazi.
Alifafanua kuwa hatua hizo ni sehemu ya
utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, lililotaka kufumuliwa na kusukwa upya
kwa TFS ili kuongeza ufanisi.
Kutokana na hatua hiyo, Waziri Maghembe
alisema Profesa Dos Santos Silayo ameteuliwa
kuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa TFS, wakati
Kamwenda anahamishiwa Chuo cha Viwanda vya
Misitu kilichopo Moshi.
Aidha, Mwanaidi Kijazi aliyekuwa Mkurugenzi wa
Usimamizi wa Raslimali za Misitu na Nyuki, yeye
amekwenda kuwa Mhifadhi Mkuu Amani Nature
Reserve na nafasi yake inachukuliwa na Zawadi
Mbwambo.
Waziri Maghembe alisema Mohamed Kilongo
aliyesimamishwa kazi Januari 5, mwaka huu
uchunguzi umeonekana hana hatia na hivyo
anaendelea kuwa Mkurugenzi Mipango na
Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu.
Alisema Wizara imeamua Mkurugenzi wa Idara ya
Misitu na Nyuki, Gladnes Mkamba ahamishiwe
Idara ya Mipango makao makuu na nafasi hiyo
kuteuliwa Dk Ezekiel Mwakalukwa, kuwa Kaimu
Mkurugenzi.
Aidha Monica Kagya aliyekuwa Kaimu
Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Ufugaji
Nyuki, anakuwa Mtafiti Mwandamizi Idara ya
Nyuki (Tawiri). Alisema Kagya ni mtaalamu wa
masuala ya nyuki, hivyo atahamishiwa Taasisi ya
Utafiti wa Wanyamapori, ili ashughulikie utafiti
wa masuala ya nyuki.
Pia alisema katika Idara ya Wanyamapori,
Profesa Alexander Songorwa anakuwa Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, nafasi
ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Herman Kerayo
ambaye anahamishiwa Idara ya Mipango Makao
Makuu.
Profesa Ramadhan Kideghesho, yeye anakwenda
kuwa Mkuu wa Chuo cha Mweka wakati Mabula
Misungwi aliyekuwa Meneja Mradi Selous,
anakwenda Chuo cha Wanyamapori Pasiansi na
nafasi yake inachukuliwa na Jaffary Lyimo, huku
Robert Mande akipelekwa kuwa Kaimu
Mkurugenzi msaidizi Uzuiaji Ujangili.
Waziri Maghembe alisema Majjid Ally ameteuliwa
kuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Leseni, nafasi
iliyokuwa ikishikiliwa na Haji Mpya ambaye
amehamishiwa Shamba Jipya Songea kuwa Ofisa
Misitu Alisema Julai 18, mwaka huu Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa alikutana na viongozi na
watumishi wa Wizara hiyo na watendaji wakuu
na watumishi wa TFS na kuagiza kufumuliwa na
kusukwa upya kwa wakala huo.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu alitaka
kuondolewa kwa utitiri wa vituo vya ukaguzi na
kuwekwa vituo vichache na kuondolewa kwa ofisi
za makontena yanayotumiwa na ofisi ya TFS,
badala yake watumishi wanaofanya ukaguzi
wasimame mahali pa wazi ili kuondoa mianya ya
rushwa na kuweka uwazi katika utendaji.
0 comments :
Post a Comment