Tbs yaendelea kuongeza ufanisi wa huduma bora kwa kufungua ofsi katika mikoa hii.
Katika jitihada zake za kuongeza ufanisi
na huduma bora, Shirika la Viwango
Tanzania (TBS) limefungua ofisi za kanda
katika mikoa ya Arusha, Mwanza na
Mbeya.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo,
Dkt. Egid Mubofu (pichani) amewaambia
waandishi wa habari jana jijini hapa kuwa
hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa
bidhaa zinazozalishwa au kuuzwa kwa
watanzania zinakuwa na ubora na
viwango vinavyotakiwa.
“Ofisi hizi zitafanya kazi kwa karibu na
wazalishaji viwandani ili wananchi
wapate bidhaa bora,” alisema na
kuongeza kuwa watendaji katika ofisi hizo
watakuwa wanafanya ukaguzi viwandani
na kushughulika na maombi ya
wazalishaji wapya.
Alisema ofisi ya mkoa wa Arusha
itahudumia mikoa ya kanda ya kaskazini
ikiwemo Manyara, Kilimanjaro, Tanga na
Arusha yenyewe; Ofisi ya Mwanza
itahudumia Kanda ya ziwa mikoa ya
Mara, Kagera, Shinyanga, Simiyu, Geita
na Mwanza yenyewe.
Ofisi ya Mbeya itahudumia mikoa ya
nyanda za juu Kusini ya Iringa, Songwe,
Ruvuma, Njombe na Mbeya yenyewe.
Dkt. Mubofu alisema kwa muda mrefu
wazalishaji wa bidhaa viwandani
walikuwa wakipata huduma makao makuu
ya shirika Dar es Salaam na hivyo
kusababisha ucheleweshaji wa huduma.
Alisema ofisi hizo zitafichua viwanda bubu
vinavyo zalisha bila kufuata utaratibu.
“Ilikuwa ni vigumu kwa shirika kugundua
uwepo wa viwanda bubu katika maeneo ya
mikoani na wilayani kwa urahisi kutokana
na umbali lakini sasa kazi itafanyika bila
kikwazo,”alisema.
Pia shirika limefungua ofisi mipakani
katika mipaka ya Mutukula, Kasumulo na
Tunduma. Awali ilisha fungua ofisi Holili,
Horohoro, Sirari, Namanga na Rusumo.
Alisema kwa upande wa bandari
wamefungua ofisi katika bandari ya
Mwanza na Mombasa na pia wamefungua
ofisi katika uwanja wa ndege wa kimataifa
wa Kilimanjaro (KIA).
“Ufunguzi wa ofisi za mipakani unalengo
la kupunguza miaya ya uingizaji holela wa
bidhaa hafifu katika soko la Tanzania
unaofanywa na wafanyabiashara wasio
waaminifu,” alisisitiza Dkt. Mabofu.
Akitoa mfano alisema ufunguzi wa ofisi
katika bandari ya Mwanza na Mombasa
utapunguza uingizaji bidhaa hafifu toka
nchi jirani za Kenya na Uganda.
Alisema shirika limejipanga vyema na
kuwataka wananchi kushirikiana na ofisi
za mamlaka nchini kufichua viwanda
vinavyozalisha na wafanyabiashara
wanaokiuka utaratibu.
0 comments :
Post a Comment