Freemana Mbowe na NHC ngoma nzito kuhusu Bilicanas.soma zaid
Zimebaki wiki tatu kabla Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) kuchukua jengo la Bilicanas
lililokodiwa na Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe, kuendesha biashara ya ukumbi wa
starehe.
Jengo hilo lipo eneo la Posta jijini Dar es
Salaam.Awali, NHC ilikuwa imetoa notisi ya siku
60 kwa wadaiwa sugu ambao wamepanga
katika majengo yake akiwamo Mbowe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu,
alisema pamoja na Bilicanas, shirika linazidai
taasisi za umma, binafsi na watu binafsi jumla
ya Sh. bilioni 15.
Notisi ya siku 60 ya kuondoka Bilicanas pamoja
na majengo ya wadaiwa wengine ilishatolewa,
Mchechu alisema na kwamba sasa zimesalia
wiki tatu.
Alisema baada ya muda huo kumalizika,
utekelezaji wa kuondolewa katika majengo hayo
utaanza ukiambatana na uchukuaji wa hatua za
kisheria.
Mchechu alisema mbali ya Bilicanas, wadaiwa
wengine ni Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi
inayodaiwa Sh. bilioni mbili, Benki ya Azania
(Sh. milioni 161) na Wizara ya Mambo ya Nje,
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa (Sh. milioni 631).
Wadaiwa wengine walitajwa kuwa ni Wizara ya
Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto (Sh. bilioni 1.3), Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sh. bilioni mbili),
Tume ya Utumishi (Sh. milioni 109) na Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh.
bilioni moja.
Mchechu alisema ukusanyaji wa madeni hayo
kwa nguvu ni mkakati wa shirika hilo kukusanya
fedha ili kusaidia ujenzi wa nyumba za
watumishi wanaohamia Dodoma.
Alipoulizwa iwapo mkakati huo una uhusiano
wowote na masuala ya kisiasa kutokana na
kumtaja Mbowe kuwa ni kati ya wadaiwa sugu,
Mchechu alisisitiza hakuna uhusiano wa siasa
na zoezi hilo kwani wateja wote wanachukuliwa
sawa.
“Mwaka huu ujenzi unaanza Dodoma," alisema
Mchechu, hivyo fedha tunazodai zitatusaidia
kukamilisha uwekezaji mjini humo."
“Ndiyo maana tumetoa kwa tunaowadai notisi
ya miezi miwili, vinginevyo wataondolewa katika
majengo ya shirika kama kanuni zinavyotaka.
“Hakuna uhusiano wowote kati ya shirika
kukusanya fedha linazodai na watu binafsi
akiwamo Mbowe, taasisi za umma na binafsi.
“Lengo ni kukusanya madeni ambayo baadhi
yake yalisimama kutokana na mengine kuwa na
kesi mahakamani.”
Alisema kuwa fedha hizo zitatumika kwa ujenzi
wa nyumba za watumishi 300 hadi 500 mkoani
Dodoma.
Alisema ujenzi huo unatarajia kuanza mara moja
na utachukua miezi 12.
Kwa mujibu wa Mchechu, Sh. bilioni 60 za
ujenzi wa nyumba hizo zitatokana na fedha za
ndani.
Alisema shirika hilo limenunua ekari 240 eneo la
Iyumbu, ekari saba Chamwino, nne Bahi na
Chemba ekari nne pia ikiwa ni kuunga mkono
azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhamia
Dodoma.
Alisema fedha nyingine zitapatikana baada ya
nyumba 97 za shirika hilo zilizopo Medeli mjini
Dodoma kuuzwa.
Aidha, Mchechu alisema kitendo cha Serikali
kuhamia Dodoma kitatoa fursa kwa Jiji la Dar
es Salaam kujiimarisha kibiashara tofauti na
ilivyo sasa ambapo linakwamishwa na foleni
kubwa za magari kutokana na shughuli nyingi
za serikali kufanyika.
“Dar es Salaam kuna bandari, uwanja wa
ndege," alisema na kuongeza: “Hivyo suala la
kiuchumi litaimarika zaidi kutokana na shughuli
nyingi za Serikali kuhamia Dodoma. Hii itasaidia
uchumi wa nchi kusambaa katika maeneo
tofauti nchini.”
Uwekezaji wa NHC jijini Dar es Salaam upo kwa
asilimia 70, alisema na kwamba ufanisi wa Jiji
utaongezeka hususani katika usafiri na sekta
nyingine kiuchumi.
0 comments :
Post a Comment