Kichanga aliyeibiwa morogoro mwaka 2013 amepatikana Dar es salaam.soma zaid
POLISI mkoani Morogoro inawashikilia
wanawake wawili, wakazi wa Mbezi jijini Dar es
Salaam, Sarafina Henry (28) na Johari Hussein
(22) kwa tuhuma za wizi wa mtoto wa kike
( jina lake limehifadhiwa) na kuishi naye tangu
mwaka 2013 hadi Agosti 7, mwaka huu.
Mtoto huyo alipoibwa, alikuwa na umri wa
mwaka mmoja na nusu na amepatikana akiwa
ametimiza umri wa miaka minne na nusu, huku
watuhumiwa hao wakimwandaa kumwanzisha
kusoma elimu ya awali (chekechea).
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Morogoro, Leonce Rwegasira alisema jana kuwa
watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 7, mwaka
huu Kawe jijini Dar es Salaam.
Rwegasira alisema wanawake hao walimwiba
mtoto huyo Julai 4, 2013 saa 11 jioni maeneo ya
Karume Manispaa ya Morogoro akiwa na umri
wa mwaka mmoja na nusu.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi,
mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye Ashura
Shabani (33) mkazi wa Karume katika Manispaa
ya Morogoro aliripoti Kituo Kikuu cha Polisi mjini
hapa kuwa mtoto wake huyo ameibwa katika
mazingira ya kutatanisha.
Akielezea tukio hilo kulingana na maelezo ya
mama mzazi wa mtoto huyo, mtoto wake
aliibwa baada ya wanawake wawili waliofika
nyumbani kwake kwa ajili ya kutaka huduma za
kusuka nywele.
Alisema wanawake hao walifanikisha uhalifu huo
baada ya ndugu wa mama wa mtoto huyo
kwenda dukani kufuata rasta na ndipo
walipomrubuni awape mtoto wambebe na
mmoja wao kumbeba na kisha kutokomea
kusikojulikana kwa kipindi chote tangu 2013 hadi
Agosti 7, mwaka huu.
Akizungumzia mazingira ya kukamatwa kwa
watuhumiwa hao, alisema mdogo wa mama
mwenye mtoto aliyeibwa akiwa anaishi eneo la
Kawe jijini Dar es Salaam, alimwona mwanamke
mmoja akiwa amembeba mtoto anayefanana na
wa dada yake, ambaye aliibwa kipindi kirefu siku
siku za nyuma.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi,
mdogo huyo baada ya kumwona mwanamke
huyo akiwa na mtoto huyo, alikwenda kutoa
ripoti Kituo cha Polisi Kawe, ambako Askari
Polisi walifanya uchunguzi na kufanikiwa
kumkamata Johari Hussein ambaye alikutwa na
mtoto huyo.
Baada ya kuhojiwa kama mtoto huyo ni wake,
Johari alikataa na kusema kuwa hajawahi kuwa
na mtoto isipokuwa mtoto aliyekuwa naye ni wa
dada yake, ambaye ni Sarafina na alimpeleka ili
amwezesha kwenda kuandikishwa shule ya
watoto iliyopo eneo la Kawe.
Kaimu Kamanda alisema baada ya kufika
nyumbani kwa dada yake huyo, aliyekuwa
amemwachia mtoto na alipohojiwa, alidai mtoto
huyo alimzaa akiwa Mwanza alipokuwa akiishi
kabla ya kuhamia Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa baada ya kuhojiwa kwa kina,
mwanamke huyo alidai hakuwa na mtoto
isipokuwa mtoto huyo alitelekezwa na mama
yake na yeye aliamua kumchukua na kukaa
naye kipindi chote hicho. Alisema uchunguzi
unaendelea kufanyika na kwamba watuhumiwa
hao watafikishwa kwenye vyombo vya sheria
kujibu tuhuma za makosa yao.
Kwa upande wao, watuhumiwa hao walijitetea
kwa nyakati tofauti, mmoja akisema mtoto huyo
aliletewa na dada yake ili amsaidie
kumwandikisha shule, wakati mtuhumiwa wa
wizi wa mtoto huyo akidai alimchukua mtoto
huyo akiwa mdogo baada ya kutelekezwa na
mama yake huyo na kuamua kuishi naye kama
mwanawe wa kumzaa.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Ashura alilaani
vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wanawake
wenzao kuiba watoto, kwa kuwa ni dhambi
kubwa na matukio hayo yanawaletea majonzi na
uchungu zaidi wanawake wanaotendewa
matukio hayo.
0 comments :
Post a Comment