Waliopora mali za chama cha ushirika cha Nyanza (NCU) wasakwa.soma zaid
RAIS John Magufuli ameutaka uongozi wa Mkoa
wa Mwanza, kuhakikisha kuwa watu waliopora
mali za Chama cha Ushirika cha Nyanza (NCU),
wanapatikana na kuzirudisha mali hizo mara
moja, huku akiitaja Kampuni ya Simon Group
yenye umiliki katika kampuni za UDA na mabasi
ya haraka Dar es Salaam (UDA-RT).
Amesema NCU kwa sasa inashindwa
kujiendesha kutokana na watu wachache
kujitwalia mali za NCU kwa kuzinunua kwa bei
ya hasara, kiasi cha kuifanya NCU kutokuwa na
uwezo wa kununua mazao ya wakulima.
“RC (mkuu wa mkoa) umezungumza kwamba
katika miaka yote aliyepewa alikuwa anunue
kwa bilioni moja pointi amelipa milioni 30 tu na
nasikia ni Simon Group. Mimi ni msemakweli na
wala sitaki kuzunguka sijui nikasemee wapi,”
alisema Rais Magufuli akiitaja kampuni hiyo
inayomilikiwa na mfanyabiashara Simon Kisena.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana jijini hapa
wakati akiwahutubia maelfu ya wakazi wa
Mwanza kwenye Viwanja vya Furahisha vilivyopo
Manispaa ya Ilemela.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John
Mongella alimshukuru Rais Magufuli licha ya
kuwa na ratiba ngumu ya kikazi, lakini
ameonesha mapenzi makubwa kwa wakazi wa
Mkoa wa Mwanza na kufanya ziara ya kikazi ya
siku mbili.
Alisema mkoa umeanza na juhudi ya kufufua
zao la pamba sanjari na kuanza kurudisha mali
za NCU, ambazo ziliporwa na baadhi ya watu,
alimuomba Rais Magufuli kuisaidia Serikali ya
Mkoa ili kuhakikisha watu wote waliopora mali
za NCU wanazirudisha kwa wakulima na
wafikishwe mahakamani.
Lakini Rais Magufuli katika hotuba yake, alisema
NCU kwa sasa inashindwa kujiendesha kutokana
na watu wachache kujitwalia mali zake kwa
kuzinunua kwa bei ya hasara, kiasi cha kuifanya
kutokuwa na uwezo wa kununua mazao ya
wakulima.
“Hata kama walichukua miaka 20 iliyopita,
vyombo vya dola vichukue hatua na mali hizo
zirudishwe kwa umma. Waziri wa Ushirika, ni
heri ukose kula, mimi nitakuchagua kwenye viti
maalumu, lakini mali za Nyanza zirudi,” alisema
Rais Magufuli.
Aliwataka mafisadi wakae chonjo kuwa tayari
kufikishwa mahakamani kwa sababu Bunge
tayari limeishaipitisha sheria hiyo, ambayo
itaanza utekelezaji wake mara moja.
Alisema sheria hiyo itakuwa ni mkombozi wa
Watanzania ambao hivi sasa wamechoka na
rushwa, ambapo alikiri kuwa kwa sasa rushwa
ipo kila mahali nchini.
“Nawashukuru sana wabunge (hasa wa CCM)
kwa kupitisha sheria hiyo ya mafisadi,” alisema
Rais Magufuli.
Kuhusu uvuvi haramu kwa kutumia zana
zisizokubalika kisheria, Rais Magufuli alishangaa
kuona vyombo vilivyopewa jukumu la kudhibiti
hali hiyo vikizembea wakati uharamia huo
ukiendelea.
“Kama kuna mtu alichoma makokoro ni mimi na
samaki waliongezeka. Wanapita kuna Polisi,
Uhamiaji, TRA, lazima tulinde rasilimali yetu ili
Watanzania waweze kufaidika. Hizo zana
zinapitishwa kwenye mipaka, shikeni na hilo gari
mtaifishe moja kwa moja kwa sababu hayapiti
angani,” alieleza.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisisitiza
kuwa uchaguzi umekwisha na kwamba hakuna
aliyeshinda wala kushindwa, bali Watanzania
wote wameshinda. Alisisitiza kuwa atatekeleza
ahadi zote alizoahidi wakati wa Uchaguzi Mkuu
ikiwamo kulifanya Jiji la Mwanza kuwa jiji la
biashara.
Akizungumzia hatua ambazo
amekwishazichukua hadi sasa katika uongozi
wake, alisema amebana matumizi ya serikali
kwa kufuta safari zisizo za lazima nje ya nchi,
kutumbua watumishi hewa, kutoa elimu bure, na
mwezi ujao ndege mbili mpya zitatua nchini
kutoka Canada zinaponunuliwa.
Akizungumzia upanuzi wa barabara ya Airport,
Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe, Janet,
alimtaka Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Edwin
Ngonyani, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick
Mfugale kuhakikisha kuwa ujenzi wa barabara
hiyo hadi Airport, badala ya kuishia Pasiansi,
inajengwa haraka iwezekanavyo.
“Upanuzi wa barabara hii usiishie Pasiansi,
uende hadi Airport na iwe ni barabara yenye njia
nne ili kusudi watalii wanapofika hapa
watambue kuwa wameingia jijini Mwanza,”
alisema na kuongeza kuwa serikali itatoa fedha
za upanuzi wa barabara hiyo hadi Airport na
kuahidi kutoa kiasi cha fedha kitakachohitajika
ukamilishaji ujenzi wake.
Aidha, alikerwa na ukusanyaji duni wa mapato
yanayokusanywa kutoka kwenye vitega uchumi
vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwataka
viongozi wote wa chama kuhakikisha kuwa
wanakusanya mapato halali yanayolingana na
vitega uchumi walivyo navyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ngonyani
aliwashukuru wakazi wa Mwanza kwa kazi
kubwa waliyofanya ya kumchagua Dk Magufuli
kuwa Rais wa Tanzania.
0 comments :
Post a Comment