Breaking News
Loading...

Advert

Thursday, August 11, 2016

Waliohodhi viwanja kati 700hadi10,000 bila kuendelezwa kutaifishwa na serikali

SERIKALI imesema kuna watu wanamiliki
viwanja kati ya 700 hadi 10,000 na vimepatiwa
hati, lakini wamevishikilia bila kuviuza, wakisubiri
kupanda thamani kwa ardhi ya maeneo yao na
kuwauzia wananchi, hivyo serikali imewataka
kuviendeleza au kuviuza, la sivyo itavitaifisha.
Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
amewataka watu wote walionunua mashamba
na kupima viwanja na kupatiwa hati kwa lengo
la kuuza viwanja hivyo, wafanye hivyo ndani ya
siku 90 vinginevyo serikali itawafutia hati hizo.
Lukuvi alisema hayo jana jijini Dar es Salaam
wakati akizungumza na wamiliki wa kampuni
binafsi za mipango na upimaji miji, aliokutana
nao kwa lengo la kuwataka waanze kazi ya
kupanga miji na kupima maeneo nchini ambayo
halmashauri zitayatangaza kisheria kuwa miji.
“Wapo watu na ninawafahamu ambao walinunua
viwanja na mashamba na ninyi mkawapimia na
kuja kuchukua hati kwa majina yao halafu
viwanja hivyo hawaviuzi na wamefungua
masijala majumbani mwao kwa lengo la kusubiri
bei zipande wawauzie wananchi… nawapa miezi
mitatu wawe wameuza viwanja hivyo vinginevyo
tutawafutia hati zao,” alisema Lukuvi.
Lukuvi alisema anawajua watu hao na yupo
ambaye kwa siku moja, alichukua hati za
viwanja 700 peke yake wizarani hapo, lakini
hajaviuza hadi leo, hivyo aliwataka wamiliki hao
ambao wengine wana hati hadi 10,000
wanasubiri hadi miaka 10 ndio waviuze.
Alisema wamiliki wa viwanja hivyo, watangaze
kupitia magazeti juu ya kuuza viwanja hivyo,
vinginevyo watapitisha msako na wakibainika
bado wamehifadhi viwanja hivyo moto
utawawakia. Lukuvi alisema kama wamiliki hao,
wanavitaka viwanja hivyo, basi waviendeleze na
wasipofanya hivyo watavitaifisha viwanja hivyo
kwa kushindwa kuviendeleza.
Katika kutafuta maoni ya kisheria juu ya uamuzi
huo wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, gazeti hili lilitafuta baadhi ya
wanasheria na kusema kuwa uamuzi huo wa
serikali ni wawazi, kwani ardhi ni mali ya serikali
na ina mamlaka kisheria kutoa maamuzi yoyote.
“Watanzania wengi tumejisahau sana juu ya nani
hasa mmiliki wa ardhi, ardhi ni mali ya serikali,
ndio maana inakupa hati na wakati wowote
kama imekutaka uiendeleze hati hiyo iliyokupa
na wewe hujafanya hivyo inaweza kuichukua na
kukufidia kama kuna gharama zako,” alisema
Wakili Emmanuel Makene.
Aidha, Lukuvi alisema katika kukabiliana na
wahalifu wa namna hiyo na kuendana na kasi ya
utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano,
wameamua kuzipa idhini kampuni binafsi za
mipango miji na upimaji ardhi kufanya kazi hiyo.
Alisema nchini kwa sasa kuna kampuni za
kupanga 33 na kupima 58, ambazo zimesajiliwa
kisheria hivyo zisambae nchini kote kufanya kazi
ili kutimiza lengo lililokusudiwa la serikali la
kupima na kutoa hati kwa watu wengi zaidi.
Alisema serikali ina uhaba wa watumishi hasa
katika sekta ya ardhi, upande wa mipango na
upimaji, hivyo kuwapa kazi hiyo sekta binafsi
kwani wao watakuwa waaminifu na watafanya
kazi kwa wakati.
Alisema awali kazi ya upangaji na upimaji
ilikuwa inafanywa na idara za ardhi za wilaya na
kampuni binafsi chache, zilizokuwa na watu wao
na kutumia ujanja wao walikuwa wakipenya na
kufanya kazi hizo lakini sasa kazi hiyo
imerasimishwa rasmi kwa sekta binafsi ili kazi
ifanyike kwa ufanisi.
Aidha, amesema licha ya Tanzania kuwa na
ardhi kubwa, lakini hadi sasa ni hati milioni 1.7
tu ndio zimetolewa jambo linalowafanya watu
wengi kuishi katika maeneo ambayo
hayajapimwa na serikali imejipanga kwa mwaka
huu kutoa hati 400,000 za viwanja na
mashamba hivyo ameamua kushirikisha sekta
binafsi katika kufikia lengo hilo.
Katika hatua nyingine, Lukuvi amekabidhi fomu
za kupatiwa hati mbadala kwa wananchi 446
wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, ambao viwanja
vyao viliuzwa mara mbili na maofisa ardhi wa
wizara na halmashauri ambao walikuwa si
waaminifu.
Lukuvi alisema Wizara yake imetenga jumla ya
viwanja 600 kwa ajili ya kuwafidia watu hao na
kuwataka kujitokeza na vielelezo vyao vyote ili
wafidiwe viwanja hivyo.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top