Mohammed Dewji kuwekeza katika viwanda .soma zaid
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema
wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi
wanaiathiri Serikali katika juhudi zake za
kuboresha maisha ya Watanzania.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifanya
mazungumzo na Mohamed Dewji, Ofisini
Kwake Dar es Salaam leo.
Amesema Serikali haina mgogoro na
wafanyabiashara bali inawataka walipe kodi na
kama kuna wanaoonewa na watendaji wa chini
kwa kubambikiziwa kodi watoe taarifa juu ya
jambo hilo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, 30
Agost, 2016) wakati akizungumza na Mkurugenzi
Mtendaji wa Makampuni ya Mohamed Enterprises
Tanzania Limited (MeTL), Mohamed Dewji, ofisini
kwake jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali imedhamiria kuwaunga mkono
wafanyabiashara katika shughuli zao ili waweze
kulipa kodi itakayoifanya imudu kuwahudumia
wananchi katika huduma mbalimbali za jamii.
“Sisi msisitizo wetu ni ulipaji kodi, wakwepa kodi
wanatuathiri. Sekta nyingine zinashindwa
kuendelea kwa sababu hazina mtaji na kodi
hazipatikani vizuri,” amesema.
Amesema “Ninyi timizeni wajibu wenu kwa kulipa
kodi stahiki, tutawasaidia katika kufanya biashara
zenu. Tutawasaidia katika kusimamia mambo
yenu ila mjue kwamba nchi hii bila viwanda
hatuwezi kwenda,”.
Pia amewataka wafanyabiashara kwenda kujenga
viwanda katika maeneo ambayo malighafi
zinazalishwa ili kuwahamasisha wakulima
kuzalisha zaidi na kuwapunguzia mzigo wa
kusafirisha malighali hizo.
Kwa upande wake Dewji amemuhakikishia Waziri
Mkuu kwamba wafanyabiashara wanaiunga
mkono Serikali ya Awamu ya Tano na hawana
mpango wowote wa kuhamishia mitaji yao nje ya
nchi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
“Huu ni uongo na uzushi tu ambao watu
wameamua kuusambaza, mfano mimi mwenyewe
nimeanza kuongeza mitaji katika biashara zangu.
Nimefufua kiwanda cha kuchambua pamba cha
Chato. Nafungua biashara zingine mpya kubwa
ikiwemo ya kufufua kiwanda cha nguo cha
Musoma ambacho kitakuwa kinatengeneza jeans
za kuuza nje ya nchi,” amesema.
Amesema yuko tayari kuwekeza kwenye ujenzi
wa kiwanda cha sukari katika wilaya ya Rufiji
mkoani Pwani. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo
wa kununua miwa tani milioni 1.2 zitakazozalisha
tani 120,000 za sukari kwa mwaka.
Mkurugenzi huyo amesema amepanga kuwekeza
sh. bilioni 40 kwa ajili ya kukuza uzalishaji katika
mashamba yake ya mkonge kwenye mikoa ya
Pwani, Tanga na Morogoro.
Pia amewekeza sh. bilioni 70 katika viwanda vya
kusaga unga wa ngano na sembe na anatarajia
kununua tani laki moja za mahindi katika msimu
wa mwaka huu.
Mbali na kuwekeza katika viwanda hivyo Dewji
amesema anatarajia kujenga kiwanda kikubwa
cha kutengeneza sabuni ya unga ambacho
kitakuwa ni kikubwa kuliko vyote katika nchi za
Afrika Mashariki na Kati.
“Tumeamua kuongeza uwekezaji katika viwanda
ili kuunga mkono mkakati wa Serikali wa
kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Vile
vile nimefanikiwa kuishawishi kampuni kubwa na
maarufu ya kutengeneza sigara duniani ya
Marlboro kuingia nayo ubia na sasa tunajenga
kiwanda cha sigara hizo mjini Morogoro,”
amesema.
0 comments :
Post a Comment