Waziri awataka watanzania kujifunza kuwatia moyo wanamichezo wa watanzania wanaposhiriki mashindano ya michecho ndani na nje ya nchi.soma zaid
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mhe. Nape Nnauye amewataka
Watanzania kujifunza kuwatia moyo
Wanamichezo wanaposhiriki katika
michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Wito huo ameutoa jana Jijini Dar es
Salaam wakati wa Hafla ya kuwapongeza
na kupokea bendera ya Taifa toka kwa
Wanamichezo ambao walishiriki katika
Mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika
hivi karibuni mjini Rio, nchini Brazil. Mhe.
Nnauye alisema kwamba, Watanzania ni
vizuri wakajifunza kusema maneno
mazuri kwa wanamichezo pindi
wanaporejea toka katika Mashindano
mbalimbali ili kuwapa moyo wa kuendelea
kufanya vizuri wanamichezo hao huku
akisisitiza kuwa, ni vema ukosoaji
ukaendana na ushauri mzuri wenye
kujenga badala ya kulaumu.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mhe. Nape Nnauye (Mb) (kulia)
akimkabidhi cheti Mwanariadha
Alphonce Simbu baada ya kuibuka
mshindi wa nafasi ya tano katika
Mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika
hivi karibuni mjini Rio, Brazil.
Aliongeza kuwa, Wanahabari nchini
wanapaswa kuandika mazuri
yanayofanywa na wanamichezo kwani
yana manufaa kwa Taifa badala ya
kutafuta maneno yasiyo na tija ya kukosoa
mara kwa mara kwani kuna wavunja
moyo wanamichezo. “Tukijifunza kuandika
na kusema mabaya tu ya kuvunja moyo
kwa wanamichezo wetu hii sio sawa sawa,
tujifunze kuwatia moyo, na hii ni hatua ya
kwanza na wito wangu kwa Watanzania
wote”, alisema Mhe. Nnauye
Alisisitiza kwamba, Watanzania
wanapaswa kujifunza kujivunia vitu vya
kwao kwa njia hiyo itakuwa ikiongeza
hamasa kwa wanamichezo katika
kujituma kwa manufaa yao na ya Taifa.
Aidha, alisisitiza kuwepo na maandalizi
ya mapema kwa Wanamichezo nchini ili
waweze kufanya vizuri zaidi huku
akishauri uwekezaji wa kutosha katika
sekta hiyo na kuyataka Makampuni kuwa
na tabia ya kuwatumia Wanamichezo
nchini katika kutangaza utalii wa nchi.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mhe. Nape Nnauye (Mb) (kulia)
akimkabidhi King'amuzi cha Kampuni ya
DSTV Mwanariadha Alphonce Simbu
baada ya kuibuka mshindi wa nafasi ya
tano katika Mashindano ya Olimpiki
yaliyomalizika hivi karibuni mjini Rio,
Brazil.
Ametoa wito kwa Viongozi wazembe
ambao watashindwa kufikia malengo
mazuri katika tasnia hiyo ni bora
wakaachia ngazi zao ili kuwapa nafasi
watu wengine wenye uwezo kutekeleza
kazi hiyo.
“Nadhani sasa tuanze kukabana kwenye
Vyama, ukichaguliwa na kukawa na
mashindano kama haya, ukashindwa
kupeleka hata mchezaji mmoja, kazi yako
ya kwanza nadhani ni kijiuzulu”, alisema
Mhe. Nnauye.
Awali akitoa taarifa ya Wanamichezo
walioshiriki katika Mashindano hayo, Rais
wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC)
Bw. Gulam Rashid alisema kwamba,
Tanzania ilishiriki mashindano hayo ikiwa
na Wanamichezo saba, walimu wa tatu wa
michezO ya kuogelea, Judo na riadha
ambapo kati yao wachezaji wa nne
walipata nafasi ya upendeleo
(Universality).
Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania
(RT) Bw. Anthony Mataka akiongea na
baadhi ya Viongozi, wageni waalikwa
pamoja na Wanamichezo (hawapo
pichani) walioshiriki katika Mashindano
ya Michezo ya Olimpiki yaliyomalizika
hivi karibuni mjini Rio, Brazil.
Alifafanua kuwa, wachezaji wa nne
waliofanikiwa kupata nafasi ya upendeleo
ni wale ambao walishiriki katika michezo
mbalimbali katika kusaka viwango, lakini
kwa bahati mbaya hawakuweza kufikia
viwango vinavyowaruhusu wao kushiriki
katika mashindano hayo, hivyo kulingana
na Sera na itikadi za Olimpiki zilitaka kila
nchi Duniani ambayo ni Mwanachama wa
Mashindano hayo kutoa watu wake, hivyo
walitoa nafasi hiyo kwa wale waliokosa
kufikia viwango kuweza kushiriki.
“Nchi ambayo haikuwa na wachezaji
waliofikia viwango vya Olimpiki walipewa
nafasi ya upendeleo kwa wanamichezo
kuweza kushiriki na kwa Tanzania
tulikuwa na Waogeleaji wa tatu, mchezaji
wa Judo na mchezaji wa kike wa mbio
(Marathon) kwa hiyo, huo ndiyo upendeleo
ambao wengi hawauelewi ni upendeleo
upi”, alisema Bw. Gulam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki (TOC)
Bw. Filbert Bayi akiongea na baadhi ya
Viongozi, wageni waalikwa pamoja na
Wanamichezo (hawapo pichani)
walioshiriki katika Mashindano ya
Michezo ya Olimpiki yaliyomalizika hivi
karibuni mjini Rio, Brazil. PICHA ZOTE
NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.
Aidha, katika hafla hiyo, mbali na
kukabidhiwa Bendera ya Taifa toka kwa
kikosi hicho cha Wanamichezo walioshiriki
katika Olimpiki 2016mjini Rio-Brazil, Mhe.
Nnauye kwa niaba ya Makampuni ya TTCL
na DSTV-Multi Choice aliwapatia zawadi
mbalimbali washiriki hao zikiwemo fedha
taslimu ambapo kwa nafasi ya kipekee
Mwanariadha Alphonce Simbu ambaye
aliibuka katika nafasi ya tano katika
Mashindano hayo amepatiwa Mkataba wa
mwaka mmoja wa kuwa Balozi wa DSTV
ambapo kila mwezi atakuwa akilipwa kiasi
cha Shilingi milioni moja pamoja na
king’amuzi maalum, huku washiriki
wengine wakipewa ving’amuzi na fedha.
0 comments :
Post a Comment