Breaking News
Loading...

Advert

Wednesday, September 7, 2016

Watumishi 34 wa mahakama wakiwemo mahakimu 11 wamefukuzwa kazi.soma zaid

WATUMISHI 34 wa mahakama wakiwemo
mahakimu 11, wamefukuzwa kazi kutokana na
makosa mbalimbali ya kinidhamu.
Aidha, Tume ya Utumishi wa Mahakama
inaendelea kujadili hatma ya mahakimu 30,
waliokuwa wanatuhumiwa kuhusika na rushwa
na kushinda zao mahakamani ili kuangalia kama
walifanya makosa ya kinidhamu.
Jaji Mkuu, Mohammed Chande Othman alisema
hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza
na waandishi wa habari baada ya kupokea
taarifa za ukaguzi wa mahakama pamoja na
uendeshwaji wa mashauri.
Othman alisema watumishi hao, wamefukuzwa
kutokana na uamuzi wa kikao cha Tume ya
Mahakama, kilichofanyika Agosti 18, mwaka huu
baada ya kushughulikia masuala mbalimbali ya
kinidhamu.
“Tumewafukuza mahakimu wakazi wafawidhi,
mahakimu wa mahakama za Mwanzo za
Rombo, Temeke, Bahi na Chamwino na
watumishi wengine 23. Hii ni idadi ndogo
ambayo ni sawa na asilimia 0.005 ya
wafanyakazi wote lakini kwa mahakama ni doa
kubwa,” alisema Jaji Mkuu.
Alisema mahakimu hao wamefukuzwa kwa
makosa mbalimbali ya kinidhamu, ikiwemo
kutumia muhuri wa mahakama kinyume cha
taratibu, kuathiri utendaji wa haki kwa
kumsaidia mtu kufungua kesi moja katika
mahakama mbili pamoja na kufungua kesi ya
mirathi bila kuwa na hati ya kifo.
Aliongeza kuwa kuna makosa ya kisheria
ambayo jaji au hakimu akikosea kutumia kifungu
cha sheria hawajibishwi, lakini kuna makosa ya
kinidhamu ambayo yanaondoa sifa ya kuwa
hakimu au jaji.
Kuhusu mahakimu walioshinda kesi za rushwa
mahakamani, Jaji Chande alisema mahakama
inaweza isiwakute na hatia, lakini Tume
itaangalia kama walifanya vitendo vya ukosefu
wa nidhamu na kuwawajibisha.
Aidha, alisema mahakimu wengine 32 waliokuwa
wanakabiliwa na kesi za jinai na kushinda kesi
mahakamani, wanafunguliwa mashitaka ya
kinidhamu katika Kamati ya Maadili ya Maofisa
wa Mahakama kwa sababu inawezekana
hawajapatikana na hatia ya kosa la jinai, lakini
kama kuna vitendo vya ukosefu wa maadili
watawawajibisha kimaadili.
Mahakama Maalumu ya Ufisadi na Uhujumu
Katika hatua nyingine, Mahakama Maalumu ya
Ufisadi na Uhujumu Uchumi imeanza rasmi na
wiki ijayo Kanuni za Uendeshaji wa mahakama
hiyo, zinatarajiwa kuchapishwa. Jaji Mkuu
Othman alisema mahakama hiyo, imeanza rasmi
Julai 18 mwaka huu baada ya Rais John
Magufuli kusaini sheria ya uanzishwaji wa
mahakama hiyo.
“Wiki ijayo tutachapisha kanuni mbalimbali za
uendeshwaji wa mahakama hiyo, ikiwemo jinsi
ya kulinda mashahidi pamoja na taratibu za
ufunguaji wa kesi,” alisema Othman.
Alisema mahakama hiyo itakuwa na majaji wa
kutosha ili kufanya kazi kwa uadilifu na
kumaliza kesi kwa wakati, pia haitakuwa
ikiahirisha kesi mara kwa mara.
Kuhusu utendaji kazi wa mahakama, Jaji Mkuu
alisema mahakama haiwezi kutoa haki kama
itakuwa inajificha au kuendeshwa kwa siri, ndiyo
maana kwenye maboresho ya mahakama,
wameamua kuwapa fursa wananchi kutoa
mapendekezo au kero zao kupitia namba za
simu pamoja na barua pepe.
Kesi za uchaguzi Awali akiwasilisha taarifa za
utendaji wa Mahakama Kuu, Mahakama za
Hakimu Mkazi, Wilaya na za Mwanzo, Msajili wa
Mahakama Kuu, Ilvin Mugeta alisema baada ya
uchaguzi, walipokea kesi 247 za uchaguzi, 53
za kupinga matokeo ya ubunge na 194 za
udiwani.
Mugeta alisema tayari wameshamaliza kesi 234,
zimebaki 13, lakini hadi kufikia Desemba mwaka
huu kesi zote zitakuwa zimemalizika.
Aidha, alisema tathmini waliyoifanya inaonesha
kesi zilizopo zinawiana na mahakimu, na kama
watawezeshwa kwa vifaa vya kutendea kazi
hadi Desemba mwaka huu watamaliza kesi zote
zilizofunguliwa mwaka huu.
Mahakama ya Rufaa Kwa upande wake, Msajili
wa Mahakama ya Rufaa, John Kahyoza alisema
kiwango cha kumaliza mashauri katika
Mahakama ya Rufaa kimeongezeka, pia wana
lengo la kuhakikisha nakala za hukumu
zinapatikana siku hukumu na ndani ya siku tatu
zitapatikana kwenye tovuti ya Mahakama ya
Tanzania.
Aidha, aliwaomba wananchi watoe ushirikiano ili
rufaa zisikilizwe na kuisha mapema, kwa sababu
kuna watu wanashindwa kufika mahakamani bila
sababu za msingi au kutoa visingizio jambo
linalosababisha rufaa zao kuchelewa.
Umuhimu wa mahakama Katika hotuba yake
kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari
4, mwaka huu, Rais Magufuli alisema
anaitegemea sana Mahakama na aliwaambia
majaji na mahakimu nchini kuwa:
“Nawaomba waheshimiwa majaji na
waheshimiwa mahakimu, muitangulize Tanzania
kwanza. Mkiitanguliza Tanzania kwanza
tutaweza kufika mbali na tutaweza kuwasaidia
watanzania wengi. Nimeamua nchi iende, na
itaenda. Anayefikiri ataikwamisha, atakwama
yeye kwa sababu Mungu yuko pamoja na mimi.
Na watu ninaowategemea sana ni Mahakama.
Mahakama unafunga kila mmoja. Hata Rais
nikitaka kufungwa na Mahakama, nafungwa.
Mbunge anafungwa, nani anafungwa, nyinyi ndio
wenyewe”.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top