Rais Kabila amuhakikishia Rais magufuli kuwa hali ya kisiasa na usalama nchini Congo ni nzuri.soma zai
Magufuli ataka Wakongo warudi nchini kwao
RAIS John Magufuli ameagiza wakimbizi kutoka
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)
waliopo nchini, warudishwe nchini mwao baada
ya Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila
kumhakikishia kuwa hali ya kisiasa na usalama
nchini mwake sasa ni nzuri.
Magufuli aliyasema hayo Ikulu jijini Dar es
Saalam jana wakati alipokutana na Kabila
ambaye yupo ziarani nchini kwa siku tatu kuanzia
juzi.
Magufuli alisema wakimbizi wa Kongo hawana
tena sababu ya kung’ang’ania kukaa Tanzania
wakati hali ya amani nchini mwao
imeshatengemaa.
Alisema wakimbizi hao wanapaswa kujipanga
kurudi nchini mwao ili wakajiandae katika kazi ya
kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao na kisha
kushiriki katika kujenga uchumi wa nchi yao.
“Wakimbizi walioko Tanzania kutoka Kongo
wajipange kurudi kwao ili wakajiandae kupiga
kura… wakajenge nchi yao kuliko kukaa hapa,”
alisema Magufuli.
Magufuli alitoa kauli hiyo baada ya Kabila
kueleza katika hotuba yake ya awali kuwa hali ya
amani nchini Kongo ni nzuri kwa asilimia 97.
KABILA ALIA NA VYOMBO VYA HABARI
Katika hotuba yake, Kabila alilalamikia baadhi ya
vyombo vya habari alivyodai vimekuwa
vikipotosha ukweli kuhusiana na hali ya amani
nchini mwake kwa kujaribu kuonyesha kuwa kuna
vurugu zitokanazo na vita vya waasi.
Alisema hivi sasa, ni maeneo machache tu
ambayo bado si salama nchini mwake na hayo
yapo mashariki mwa Kongo, yakikaliwa na vikundi
vya waasi vinavyoendesha vurugu.
"Hivi karibuni tutaanza mazungumzo ya kutafuta
amani ya kudumu nchini Kongo na lengo letu ni
kuhakikisha nchi nzima inakuwa na amani kabla,
wakati na baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika
Desemba ama baada ya mwezi Desemba,"
alisema Kabila.
MADEREVA WALIOTEKWA
Katika hatua nyingine, Magufuli alimshukuru
Kabila kwa hatua ya majeshi ya nchi yake kuokoa
uhai wa madereva nane kati ya 10 wa Tanzania
waliotekwa hivi karibuni na kikosi kimojawapo
cha waasi wa Mai Mai.
Katika tukio hilo, madereva wawili walifanikiwa
kuwatoroka waasi hao wakati wakipokuwa
wakipelekwa msituni kwa lengo la kuwashinikiza
waajiri wao walipe dola za Marekani 5,000 (zaidi
ya Sh. milini 10) kwa kila dereva ili waachiwe.
WALICHOZUNGUMZA
Magufuli alisema katika mazungumzo yake na
Kabila, walijikita zaidi katika kuangalia namna
nzuri ya kuboresha ushirikiano kati ya nchi zao
kwenye nyanja za biashara, miundombinu,
uchimbaji wa mafuta na hali ya ulinzi wa mipaka.
Katika mazungumzo hayo, Kabila alimwomba
Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati za
Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya
Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Troika)
kuimarisha ulinzi upande wa Mashariki mwa
Kongo dhidi ya vikundi vya waasi vinavyowatesa
na kuwanyanyasa wananchi wasio na hatia.
Aidha, wakuu hao walizungumzia pia hali ya
kisiasa nchini Kongo huku Kabila akizihakikishia
nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini
mwa Africa (SADC) na Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) kuwa hali ya usalama nchini
mwake ni salama.
“Hali ya amani Kongo ni salama. Ila katika nchi
zote duniani, kipindi cha uchaguzi kinapokaribia
huwa kunakuwa na tensions (mivutano) ya
vyama vya siasa na tumepanga kufanya
mazungumzo ili kumaliza mvutano huo,” alisema
Kabila.
Viongozi hao pia walizungumza na kukubalina
kuingia mkataba wa pamoja wa utafutaji na
uendelezaji wa mafuta eneo la Ziwa Tanganyika,
na kwamba Kongo itakuwa na fursa ya
kusafirisha mafuta kupitia bomba la mafuta la
Uganda hadi Tanzania.
Kabila pia alimwomba Magufuli ambaye ni
Mwenyekiti wa EAC kusaidia kuiingiza Kongo
katika jumuiya hiyo, jambo ambalo liliungwa
mkono na mwenyeji wake, lakini akamweleza
kuwa wafuate masharti pamoja na kuandika
barua ya maombi ya kujiunga.
Magufuli pia alimweleza mgeni wake kuhusu
mpango wa Tanzania wa miaka mitano wa kuwa
nchi ya viwanda na kumwomba kuwahamasisha
wafanyabiashara wa Kongo kuja kuwekeza katika
sekta ya viwanda nchini.
“Pia nimemwomba Rais Kabila ahamasishe
wafanyabiashara wa Kongo kuja kuwekeza
nchini… ni vizuri kufanya biashara na jirani kuliko
kumkaribisha mtu wa mbali, naye amekubali,”
alisema Magufuli.
Aliongeza kuwa atatuma mawaziri kutoka nchi za
Angola, Msumbiji na Tanzania kwenda Kongo
kuangalia mchakato wa maandalizi ya
uandikishaji wa wananchi katika daftari la wapiga
kura, pamoja na hali ya demokrasia nchini humo.
Kuhusu hali ya biashara kati ya Tanzania na
Kongo, Magufuli alisema imeongezeka na
kwamba kwa mwaka 2009 ilikuwa Sh. bilioni 23.1
na mwaka huu imeongezeka hadi Sh. bilioni
393.6.
“Ni kweli kulikuwa na matatizo madogo madogo
pale bandarini, wafanyabishara walikuwa
wanabughudhiwa, lakini TRA wameshayamaliza
na usafirishaji wa mizigo umeongezeka kwa
asilimia 10.6,” alisema Magufuli.
Alisema katika kuimarisha ushirikiano baina ya
Tanzania na Kongo, uongozi wa Bandari ya Dar
es Salaam umetoa upendeleo maalumu kwa
mizigo ya wafanyabishara wa Kongo kuhifadhiwa
bandarini kutoka siku 14 hadi 30.
0 comments :
Post a Comment