Rais magufuli aagiza wafukuzwe kazi walio mdanganya uwanja wa ndege mwl.nyerere.soma zaid
RAIS John Magufuli amefanya ukaguzi wa
kushitukiza katika sehemu ya kukagulia mizigo
na abiria ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam upande wa
Terminal One na kuagiza maofisa wawili,
waliotoa taarifa za uongo kwake Mei mwaka huu,
wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Mei mwaka huu, Rais Magufuli alifanya ziara ya
kushtukiza mara baada ya kuwasili kwenye
uwanja huo akitokea jijini Kampala nchini
Uganda, ambako alihudhuria sherehe ya
kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda,
Yoweri Museveni. Alitembelea kwa kushitukiza na
kubaini kuwa mashine za ukaguzi (scanners)
zilikuwa hazifanyi kazi.
Lakini jana baada ya kumsindikiza Rais Joseph
Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
ambaye alikuwa akiondoka nchini baada ya ziara
ya siku tatu, aliamua kufanya tena ukaguzi wa
kushitukiza, na mara hii amebaini kuwa mashine
hizo zinafanya kazi, baada ya kujionea yeye
mwenyewe uhalisia wa namna mizigo
inavyokaguliwa.
Hata hivyo, amemuagiza Mkurugenzi wa Uwanja
wa Ndege wa Julius Nyerere, Paul Rwegasha
kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa wawili
waliotoa taarifa za uongo alipofanya ukaguzi wa
kushitukiza mara ya kwanza.
“Leo kweli mashine zinafanya kazi na mimi
nimeona, lakini wale walionidanganya mara ya
kwanza nilipokuja, mkurugenzi hakikisha
unawachukulia hatua,” alisisitiza Dk Magufuli,
kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya
habari jana.
Rais Magufuli aliagiza maofisa hao, ambao kwa
mujibu wa mkurugenzi huyo, ni Lilian Minja na
Novia Maduka ambao ni maofisa oparesheni wa
JNIA, washushwe vyeo.
Alipofanya ziara ya kushitukiza kwa mara ya
kwanza Mei 13, mwaka huu, Rais Magufuli
aliiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola
kuchukua hatua mara moja dhidi ya dosari za
ukaguzi zilizopo katika kitengo cha ukaguzi wa
mizigo na abiria Terminal One.
Aliitoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa mashine
za ukaguzi za sehemu ya kuwasili abiria na
mizigo hazifanyi kazi kwa muda mrefu.
Maofisa wa uwanja huo waliokuwa wakitoa
maelezo juu ya hali ya kitengo cha ukaguzi wa
mizigo na abiria kwenye uwanja huo, walikuwa
wakitoa taarifa zinazotofautiana kuhusu utendaji
kazi wa mashine za ukaguzi, hali iliyosababisha
Rais Magufuli aamue kuiagiza wizara husika kwa
kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua
mara moja.
“Unajua mimi sipendi kudanganywa, ni vizuri
uzungumze ukweli tu, kwa nini nimeanzia hapa
huwezi ukajiuliza?
Eeeh sasa sipendi kudanganywa, ukinidanganya
nitachukia sasa hivi, wewe umenidanganya
kwamba hiyo ndio mbovu na hii ndio nzima,
nikawaambia muiwashe hiyo nzima, akaja huyu
mwenzako amezungumza ukweli kabisa, akasema
hii ni mbovu kwa miezi miwili,” Rais Magufuli
aliwahoji maofisa wa uwanja wa JNIA wakati
huo.
0 comments :
Post a Comment