Breaking News
Loading...

Advert

Monday, October 10, 2016

Taarifa kwa umma ya mh.Ummy Mwalimu waziri wa Afya Maendeleo Jinsia,Wazee na Watoto kuhusu hali ya upatikanaji wa Dawa Nchini.soma zaid

TAARIFA KWA UMMA YA MHE. UMMY
MWALIMU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA
JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO.
KUHUSU HALI YA UPATIKANAJI WA DAWA
NCHINI NA UFAFANUZI WA MASUALA KADHAA
YALIYOTOLEWA NA BAADHI YA TAASISI ZA
KIJAMII ZINAZOFATILIA MASUALA YA AFYA.
TAREHE 10/10/2016
Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa katika
baadhi ya vyombo mbalimbali vya habari vya
ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na
mitandao ya kijamii vikizungumzia hali ya dawa
nchini hasa kufuatia taarifa zilizotolewa na
taasisi ya kiraia na baadhi ya viongozi wa
vyama vya siasa.
Taarifa hizo zilidai kwamba katika kipindi hiki
kuna upungufu mkubwa wa dawa katika bohari
kuu ya dawa , Hivyo, kusababisha kukosekana
kwa dawa katika vituo vya kutolea huduma za
Afya.
Taarifa hizi si sahihi na zinalenga kupotosha
umma na kuwatia wananchi wasiwasi. Napenda
kuwathibitishia wananchi kuwa Afya ni suala la
kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Tano.
Hivyo, ningependa kutoa ufafanuzi kwa wananchi
katika masuala yafuatayo; –
Hali ya Upatikanaji wa dawa
Hali ya upatikanaji wa dawa kwa sasa iko vizuri.
Dawa muhimu zinazohitajika sana nchini
zinapatikana kwenye maghala ya Bohari ya
Dawa (MSD). Mfano kwa upande wa dawa za
antibiotics tuna Amoxycillin, Ciprofloxacin,
Cotrimoxazole na Doxycycline. Kwa upande wa
dawa za maumivu – tunazo za kutosha kama
vile paracetamol, asprin na diclofenac.
Pia tuna dawa za kutosha za malaria, Kifua
Kikuu, ukoma na dawa za kufubaza makali ya
UKIMWI (ARVs). Kwa upande wa chanjo za
watoto na wajawazito, ni kweli kulikuwa na
uhaba nchini kwa kipindi cha miezi miwili
iliyopita. Hata hivyo, wiki iliyopita Serikali
imenunua na kupokea dozi milioni 2 za chanjo
ya Kifua Kikuu (BCG), dozi milioni 1.2 za Polio
na dozi milioni za Polio. Chanjo hizi
zinasambazwa katika vituo vya afya nchini.
Dawa nyingine zitaendelea kupatikana katika
Bohari kuu ya Dawa kwa kuwa tumeagiza dawa
za kutosha kutoka kwa wazalishaji wa ndani na
nje ya nchi. Aidha, kiasi kikubwa cha dawa
zinazowasili Bohari kuu ya Dawa zikifika
zinapelekwa kwenye Kanda nane za MSD pamoja
na vituo viwili vya Mauzo kwa ajili ya
kuwasambazia wateja walioagiza. Hivyo, kipimo
cha upatikanaji wa dawa si kuangalia katika
maghala ya Bohari ya Dawa peke yake bali pia
katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Ili kuondoa mlolongo wa manunuzi ya dawa,
tunapenda kuwataarifu kuwa Bohari kuu ya Dawa
imepanua wigo wa upatikanaji wa dawa kwa
sasa kwa kutumia mikataba ya muda mrefu
(miaka miwili) na washitiri wa ziada wa ndani
(Prime Vendors) ili kuhakikisha dawa
zinapokosekana MSD zinapatikana kwa haraka
kwa Washitiri wa ndani waliothibitishwa katika
kila mkoa.
Katika muktadha huo huo, Bohari ya Dawa
imefungua maduka ya ziada kwa ajili ya
kuongeza upatikanaji wa dawa zaidi ya aina 600
kupitia mfumo wa maduka katika mahospitali
kama vile Muhimbili, Mbeya na Arusha.
Bajeti ya dharura kwa ajili ya dawa
Ni muhimu wananchi wakajua kuwa fedha
zilizotengwa kwa ajili ya manunuzi ya dawa
katika mwaka wa fedha 2016/17 zinatosha
kuhudumia mahitaji ya dawa kwa mwaka mzima.
Hivyo hakuna sababu ya kuwa na bajeti ya
dharura.
Niwakumbushe bajeti zilizotengwa kwa ajili ya
kununulia dawa na vifaa tiba katika miaka
michache iliyopita mpaka hivi sasa, kama
ifuatavyo: -.
Mwaka 2011/2012 bajeti iliyotengwa ilikuwa
shilingi Bilioni 23.7
Mwaka 2012/2013 bajeti ilikuwa shilingi Bilioni
34
Mwaka 2013/2014 ilikuwa shilingi Bilioni 34
Mwaka 2014/2015 ilikuwa shilingi Bilioni 60
Mwaka 2015/2016 ni shilingi Bilioni 30
Na mwaka huu 2016/17 ni shilingi Bilioni 251.5
Mkakati wa Wizara kwa sasa ni kuhakikisha
kuwa fedha hizo zinapatikana kwa wakati kutoka
Hazina kulingana na makusanyo ya nchi.Vilevile
ieleweke kwamba tayari serikali imeshatoa kiasi
cha shilingi bilioni 20 katika kipindi cha robo ya
kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17, kwenda
Bohari kuu ya Dawa kwa ajili ya ununuzi wa
dawa na chanjo. Hali hii inathibitisha kuwa
suala la upatikanaji wa dawa ni la kipaumbele
kwa Serikali ya Awamu ya tano.
Kulipa Deni la Bohari ya Dawa (MSD)
Napenda kuwafahamisha kuwa Serikali
imedhamiria kulipa deni lote la Bohari ya Dawa
(MSD) ambapo katika mwaka huu wa fedha
2016/17 tayari Bilioni 85 imekwishatenga kwa
ajili ya kulipa deni hilo. Jambo ambalo
halijawahi kutokea huko nyuma. Kulipwa kwa
deni hilo kutasaidia kuhuisha mtaji wa MSD
(revolving fund) na hivyo kuiwezesha MSD kuwa
na dawa na vifaa tiba kwa kiwango kikubwa.
Aidha serikali imekwisha kuviagiza vituo vyote
vinavyotoa huduma za Afya kupitia Halmashauri
zao, kuhakikisha zinakuwa na fedha ya
mzunguko kwa ajili ya kununulia dawa (revolving
fund) na hivyo kupata dawa kwa kulipa fedha
taslimu kutoka Bohari ya Dawa badala ya
kukopa.
Fedha hizo zitapatika kutoka kwenye vyanzo
vyao vingine vya mapato kama vile Bima ya
Afya (NHIF, CHF) na gharama wanazochangia
wananchi katika kupata huduma. Hii itawezesha
kutoendelea kukuza deni kutoka Bohari ya Dawa
na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati
wote.
MSD Kupata Mshindani
Katika mwaka 2015, Serikali ilimpa kazi mshauri
mwelekezi wa kampuni ya ushauri iliyobobea
kimataifa ya Deloitte ya kulitazama jambo hili
kwa ajili ya kuifanyia tathmini MSD pamoja na
mambo mengine ikiwemo kuangalia suala ya
kutafutiwa mshindani katika manunuzi na
usambazaji wa dawa.
Napenda kuwajulisha kuwa tathmini hiyo
ilionyesha kuwa MSD kutafutiwa mshindani
itakuwa ni kuongeza gharama kubwa kwa
serikali kutokana na kurudufisha (duplication)
majukumu. Pia ilibainika kuwa suala la dawa ni
muhimu, hivyo Serikali haiwezi kuliacha kwenye
mikono ya watu binafsi.Jambo ambalo
lilipendekezwa ni kuifanyia maboresha makubwa
MSD ili iweze kutekeleza majukumu yake
ipasavyo. Utekelezaji wa mapendekezo hayo
tayari umeshaanza.
Nchi ambazo zinaiuzia dawa na vifaa tiba MSD
MSD inaagiza dawa na vifaa tiba nje ya nchi
zaidi ya asilimia 80 kwa sababu viwanda
vilivyoko ndani ya nchi havikidhi mahitaji ya
nchi kwa ubora na kiasi. Hivyo, MSD hununua
dawa na vifaa tiba kutoka nchi za India, China,
Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Ujerumani,
Marekani, Ufaransa na sehemu nyingine duniani.
Kwa mfano, tuna dawa zaidi ya aina nne ambazo
zinanunuliwa kutoka Kenya (Dawa ya kutibu
malaria kwa akina mama wajawazito ijulikanayo
kama Sulfadoxine Pyrimethamine (SP), dawa ya
kutibu magonjwa ya maambukizi ya
Cotrimoxazole ya watu wazima na watoto
pamoja, Amoxicilline na Paracetamol ya maji
kwa ajili ya watoto.
Ikumbukwe kuwa MSD hununua dawa hizi
kupitia mchakato wa zabuni, ikiwa baadhi ya
vigezo ni kuangalia usajili wa dawa nchini
pamoja na ushindani wa bei. Hata hivyo, ili
kukuza viwanda vya ndani, watengenezaji wa
dawa wa ndani hupewa hadi 15% ya upendeleo
katika mchakato wa tathmini ya zabuni dhidi ya
dawa zinazotoka nje ya nchi (Domestic
preference).
Kwa upande mwingine mkakati wa serikali sio
kuendelea kutegemea dawa kutoka nje ya nchi,
kwani kwa kufanya hivi uchumi wa nchi
hautakuwa. hivyo basi serikali iko katika hatua
za mwisho za utaratibu wa kuwakaribisha
wawekezaji wa viwanda vya kuzalisha dawa
kuwekeza nchini kwa mpango wa kuwashirikisha
wadau wengine katika masuala ya dawa (PPP).
Hitimisho
Wizara ya afya inapenda kuwahakikishia
wananchi kuwa itasimammia ipasavyo
utapatinaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba nchini
kwa wakati na kwa bei nafuu kwa kuwa Sera ya
afya inawataka wananchi kuchangia huduma.
Aidha vituo vya kutolea huduma za Afya
vinahimizwa kupeleka mahitaji na maoteo yao ya
dawa kwa wakati badala ya kusubiri hadi dawa
zote muhimu zimeisha kabisa katika vituo vyao.
Pia wanakumbusha kulipa madeni wanayodai na
bohari ya dawa sambamba na kuhakikisha fedha
inayopatikana katika shughuli za utoaji huduma
inatumika kwa ajili ya dawa, vifaa na vifaa tiba.
Ili kuondoa vikwazo kwa wananchi katika kupata
dawa na huduma za afya kwa ujumla wananchi
wanahimizwa kujiunga na mifuko ya Bima ya
Afya kwani hakuna anayejua leo hama kesho
ataugua na Magonjwa hayapigi hodi na wakati
mwingine yanakukuta hauna
akiba ya fedha, ila ukiwa na bima wakati
wowote unapata matibabu.
Mwisho, Wizara itaendelea kuhakikisha kuwa
kuna dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya
maabara vya kutosha kwenye vituo vya umma
vya kutolea huduma za Afya nchini

0 comments :

Post a Comment

Back To Top