Tingatinga imesababisha taharuki jijini Arusha baada ya kufukua fedha ardhini
AMA wewe unadhani huna fedha, basi kuna
wengine ambao wamezichimbia ardhini, tena kwa
mamilioni. Benki ya chini ya ardhi iliyosheheni
mamilioni ya fedha, zilizoswekwa ndani ya
mifuko myeusi ya plastiki na kufukiwa
mchangani, imechimbuliwa na matrekta ya
kutengeneza barabara jijini Arusha huku noti
nyekundu zikitawanywa kila kona na kufanyika
kuwa 'Sadakalawe - Amina,' kwa kila mpita njia
ambaye angeweza kujitwalia fungu.
Ilikuwa ni mshikemshike katika eneo la Mianzini
mjini hapa, ambako kuna mradi mkubwa wa
upanuzi wa barabara ya kutoka Mianzini Mataa
hadi Ilkiding'a unaoendelea.
Watu walipigana vikumbo katika harakati za
kujineemesha na fedha zilizokuwa zimetapakaa
eneo hilo. Ikiwa imesheheni noti tupu, tena
nyekundu na mpya, kufumuliwa kwa akaunti hiyo
ya benki ya chini ya ardhi pamoja na kuwa
neema kwa wapita njia na wakazi wa eneo hilo,
kuligeuka pia kuwa kilio kwa mmiliki wa hazina
hiyo, Christopher Akoonay maarufu kama
'Mmbulu' ambaye sasa amejipatia jina jingine la
'Mabulungutu.'
Akonaay ni mkulima, lakini hasa akijishughulisha
na ufugaji wa ng'ombe wa maziwa. Yeye
hudamka asubuhi kukamua mifugo hao na kisha
kusambaza bidhaa hiyo ya maziwa katika
maeneo mengi ya jiji katika kuwauzia wakazi wa
Arusha.
Na katika siku ya tukio, Akonaay alikuwa yuko
kwenye shughuli zake za kuwapelekea maziwa
wateja wake, ndipo watengeneza barabara
walipofika eneo hilo la Mianzini na tingatinga zao
na kuanza kuichimba njia hiyo ya kutoka Mianzini
hadi Ilkiding'a katika kata ya Ilboru,
inayotenganisha Jiji la Arusha na wilaya ya
Arumeru.
Ikiwa imejengwa kwa fito na matope, nyumba ya
'Mmbulu' ilikuwa miongoni mwa zile
zilizobomolewa na ni baada ya wamiliki wake,
kugoma kuzibomoa wenyewe ili kupisha upanuzi
wa barabara hiyo.
“Shauri letu tulilipeleka mahakamani kudai fidia
kabla ya mradi wa barabara haujapita hapa,”
alisema Akonaay na kuongeza kuwa mara baada
ya kesi yao kutupiliwa mbali na chombo hicho
cha sheria, wajenzi hawakusubiri hata saa moja
ipite, bali walikwenda moja kwa moja eneo hilo
na kuanza kazi.
Baadhi ya wakazi wa Mianzini, wakizungumzia
suala hilo kwa masharti ya kutotajwa majina,
walisema ni ajabu kwa Mzee Akonaay kuwa na
kiasi kikubwa cha fedha na kuzifukia ardhini huku
mwenyewe akiishi kwenye nyumba duni ya
matope.
Lakini Akonaay ambaye kwa sasa anaitwa
'Mabulungutu,' anasema kuwa alikosa imani na
benki maana wakati akifanya kazi serikalini miaka
ya 1980, alifungua akaunti na akawa anaweka
fedha zake zote benki.
Baada ya kustaafu mwaka 1994 na kuamua
kushughulika na ufugaji, hakuzifuatilia tena fedha
zake benki hadi mwaka 2000, ambako
alipokwenda kuangalia fedha zake aliambiwa
kuwa kwa sababu akaunti yake haikuguswa kwa
zaidi ya miaka 10, alitakiwa aende Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) kujieleza. Hata hivyo, aliona huo
ni usumbufu na kuamua kuanza kuweka fedha
zake nyumbani.
Lakini hii pia ilimtokea puani baada ya mmoja wa
ndugu zake kuzikwapua zote mara baada ya
kuzifuma katika vitita vyenye thamani ya Sh
milioni 20 na zaidi. Sasa Akonaay akaja na
mkakati mpya wa kuhifadhi fedha kwa kuchimba
shimo katikati ya chumba chake cha kulala,
kilichokuwa upande wa barabara ya Mianzini na
kuanza kuweka hazina yake humo.
Lakini tena, bahati mbaya ikiendelea
kumuandama, makatapila ya wachonga barabara,
yakaifukua benki yake hiyo ya ardhini na
kutawanya fedha zaidi ya Sh milioni 35 zilizoishia
kuokotwa na wapita njia pamoja na majirani,
ambao kwa hofu hawakupenda hata
kulizungumzia sakata hilo.
0 comments :
Post a Comment