Breaking News
Loading...

Advert

Saturday, October 8, 2016

Vita dhidi ya meno ya Tembo ni tishio.


NI wazi kwamba vita dhidi ya biashara ya meno
ya tembo ni tishio kutokana na uchunguzi wa
gazeti hili kubaini kuwa ni biashara inayohusisha
mataifa makubwa, wafanyabiashara maarufu
duniani na wanasiasa kutoka pande zote tawala
na upinzani.
Uchunguzi huo uliofanyika kwa wiki kadhaa sasa
kwa kulihusisha Pori la Akiba la Selous pamoja
na mambo mengine umebaini hali ya ujangili
kuendelea kuwa tishio pamoja na jitihada
mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na serikali
ili kukomesha hali hiyo.
Imeelezwa kuwa pori hilo lililopo kusini mwa
Tanzania limepoteza asilimia 90 ya tembo
waliopo katika hifadhi hiyo kutokana na ujangili
uliokithiri.
Katika kuthibitisha hilo ripoti ya Mfuko wa Hifadhi
ya Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) ya
hivi karibuni, imesema kufikia mwaka 2022 kama
hakutakuwa na hatua zozote kali
zitakazochukuliwa kuwalinda tembo kutokana na
ujangili katika Pori la Selous basi watatoweka
kabisa.
Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa kwa miaka
ya nyuma Pori la Selous lilikuwa mojawapo ya
mbuga kubwa kabisa katika Bara la Afrika lenye
tembo wengi ambapo kulikuwa na tembo zaidi ya
110,000 lakini kutokana na ujangili uliokithiri
katika miaka 40 iliyopita tembo hao wamepungua
na kubaki 13,000.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa inachangiwa na
mahitaji makubwa ya pembe za ndovu katika
nchi kubwa duniani hatua inayoelezwa kuwa
kichocheo kikubwa cha ujangili na mauaji ya
idadi kubwa ya tembo hao.
Aidha ripoti hiyo inaonesha athari kubwa
kiuchumi itakayotokea kutokana na kwamba
Tanzania kupitia Pori la Selous inaingiza dola
milioni 6 kwa mwaka ikilinganishwa na sekta ya
viwanda inayochangia dola milioni 5 katika Pato
la Taifa.
Kupungua kwa tembo Pori la Akiba la Selous
linafahamika kwa kuwa na tembo wengi, kwa
bahati mbaya kutokana na mfululizo wa hali ya
ujangili wa biashara ya meno ya tembo hesabu
ya tembo ilipungua kutoka 110,000, ilivyokuwa
mwaka 1976 na kufikia tembo 13,000 sasa.
Si mara nyingi tembo kuonekana wakiwa katika
makundi makubwa bali huonekana wakitembea
kwa vikundi vidogo vinavyoongozwa na kiongozi.
Madume ya tembo hupendelea kukaa kwenye
vichaka mara kwa mara lakini wakati fulani
hujitokeza kujiunga na makundi ya tembo wa
kike.
Inadaiwa kuwa kukithiri kwa ujangili
umesababisha kuwepo kwa tembo wachache
wenye meno makubwa, huku pia tembo wa umri
wa miaka 30 wakiwa wachache. Tembo kiongozi
anapochezesha masikio au kuinua mkonga na
kusonga mbele ni dalili ya kuwepo kwa adui.
Kiutaalamu inaelezwa kuwa ni hatari sana
kukutana na tembo anayetishia adui, askari wa
wanyamapori wenye uzoefu ndio wanaoweza
kutambua kama tembo anatishia tu au
amekasirika.
Juhudi za serikali Pamoja na hayo Serikali ya
Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maliasili na
Utalii imeweka mikakati madhubuti ikiwemo
kuunda kitengo chake cha intelijensia na kuunda
kanda nane za doria za ushirikiano katika mifumo
ya ikolojia ya mbuga ya Selous ambayo imeanza
kuwa na mafanikio.
Mwaka 2014 Shirika la Kimataifa la Sayansi,
Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa
(UNESCO) liliweka Pori la Selous katika urithi wa
asili ulio hatarini duniani.
Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Hanock
Msocha akitoa maoni yake kufuatia maswali
yaliyojitokeza wakati wa uchunguzi wa gazeti hili
kuhusu hali ya ujangili katika mbuga hiyo, pamoja
na kukiri kuwa ni tishio anasisitiza kuwa kiama
cha watu wanaojishughulisha na biashara hiyo
kimefika kutokana na nia ya dhati ya Rais John
Magufuli kukabiliana na masuala mbalimbali ya
kitaifa kwa nguvu zake zote.
Msocha anasema pamoja na kwamba askari wa
Wanyamapori wanaendelea na mapambano ya
kukabiliana na majangili wanaovamia mara kwa
mara katika Pori la Selous na kuua tembo, lakini
vita hiyo ni ngumu kwa vile wanaojihusisha ni
wafanyabiashara wakubwa na mataifa makubwa
duniani, huku wakitumia teknolojia ya kisasa kila
mara.
“Ni mapambano magumu, kwanza askari wetu
wanapambana na watu na mataifa yenye fedha
na teknolojia za hali ya juu. Zipo jitihada
zinafanyika za kuwajengea uwezo askari wetu na
kuwapatia vifaa mbalimbali lakini bado ni vita
hatari na tishio.
“Kwangu mimi naona tatizo kubwa limekuwa ni
utashi wa kisiasa. Wanasiasa hawapigani kwa
dhati katika vita hii na wapo ambao wamegeuka
mawakala na kazi yao ni kuhakikisha kuwa nchi
haifanikiwi katika mapambano haya,” alisema
Msocha.
Muelekeo wa mapambano
Akizungumzia namna anavyoona muelekeo wa
vita hiyo baada ya kuingia madarakani kwa
Serikali ya Awamu ya Tano, Meneja huyo wa Pori
la Selous alisema;
“Rais Magufuli ameonesha utashi wa kisiasa,
nimeingiwa na matumaini yeye kushinda vita hii.”
Alisema ingawa haiwekwi wazi, lakini ni ukweli
kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili
iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne ili
kukabiliana na ujangili pamoja na kuwa na kasoro
za hapa na pale ilikuwa ni sahihi katika kukabili
vita hiyo.
“Ni kweli unapohusisha wanajeshi wa Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) haiwezi
kuwa sawa na kuwatumia askari wa
Wanyamapori, wao nguvu yao ni kubwa zaidi, na
naamini wangekomesha kabisa.
“Kilichotokea ndiyo hicho ninachosema ni
ukosefu wa utashi wa kisiasa maana wanasiasa
ndio waliotumika kuipiga vita hadi ikasimamishwa
kwa kuwalaghai wananchi kudhani kuwa haikuwa
operesheni sahihi na badala yake ilitesa na
kuwaumiza watu,” alisema.
Alisema askari wa Wanyamapori wanajitahidi
pamoja na hatari iliyo mbele yao ya kuuawa ama
na tembo wenyewe au majangili akitolea mfano
wa askari mmoja (bila kupenda kumtaja jina)
aliyesema aliuawa na tembo hao wiki mbili
zilizopita akiwa katika eneo la ofisi Matambwe na
kusafirishwa mkoani Mbeya kwa maziko.
Operesheni Tokomeza Taarifa ya Kamati ya
Bunge ya Maliasili na Mazingira chini ya
aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli
wakati huo akiwa CCM, iliyotolewa kuhusiana na
kasoro za utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Ujangili ilipandisha hasira za wabunge na
hatimaye kulazimisha mawaziri wanne kujiuzulu.
Operesheni hiyo ilianza Oktoba mwaka 2013, na
kusitishwa na Bunge Novemba 4, mwaka 2014,
kwa maelezo kuwa ilikiuka haki za binadamu.
Mawaziri waliojiuzulu ni pamoja na aliyekuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Shamsio
Vuai Nahodha na aliyekuwa Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Dk Mathayo David.
Hata hivyo licha ya kuwepo kwa madhara
yaliyojitokeza katika operesheni tokomeza
Ujangili, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya
Kikwete alisema kuwa operesheni hiyo
ingeendelea, hatua ambayo Meneja wa Selous
alisema ana imani kubwa na Rais Magufuli
ataiendeleza na kutokomeza kabisa ujangili.
Kasoro katika operesheni hiyo zilitajwa na Tume
ya Uchunguzi iliyoundwa na Kikwete ikiongozwa
na Jaji mstaafu Balozi Hamisi Msumi ikiwa na
makamishna Jaji mstaafu Stephen Ihema na Jaji
mstaafu Vincent Lyimo, huku Wakili wa Serikali,
Frederick Manyanda akiwa Katibu wa Tume,
kueleza kubaini ukiukaji wa haki za binadamu
katika utekelezaji wake.
Tume hiyo ilitumia siku 265 kwa kutembelea
wilaya 38 na mikoa 20 ambapo walipokea
malalamiko mbalimbali yakiwemo unyang’anyaji
wa silaha wanazomiliki kihalali na kuhoji
mashahidi 259 katika mikoa ya Ruvuma, Iringa,
Morogoro, Pwani, Rukwa, Mbeya, Geita, Singida,
Tanga, Arusha, Manyara, Shinyanga, Kigoma,
Katavi, Kagera, Simiyu, Mara, Lindi na Tabora.
Mwigulu azungumza Katika hatua nyingine,
alipotakiwa na HabariLeo Jumapili kuelezea
hatma ya silaha za wanannchi zilizochukuliwa na
serikali wakati wa Operesheni Tokomeza, Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba
alisema serikali ipo tayari kuzirejesha silaha hizo.
Waziri huyo alitumia mwanya huo kutoa mwito
kwa wananchi wanaomiliki kihalali silaha ambazo
zilichukuliwa wakati wa operesheni hiyo na
hawajarudishiwa hadi leo, kufika kwenye vituo
vya Polisi katika maeneo yao, wakiwa na nyaraka
za umiliki silaha hizo.
Nchemba alisema wakati wa operesheni hiyo
iliyoanza Oktoba mwaka 2013, silaha mbalimbali
zilizokuwa zikitumika isivyo halali zilikamatwa na
kwamba wale waliokuwa wanamiliki silaha hizo
kihalali na wana nyaraka, wanapaswa kufika
kwenye vituo vya Polisi vya maeneo yao kuulizia
silaha zao.
“Ni kweli katika Operesheni Tokomeza ambayo
ililenga kutokomeza ujangili dhidi ya tembo,
silaha mbalimbali zilikamatwa na nyingine
zilikuwa zikimilikiwa isivyo halali. “Sasa kwa
yeyote anayemiliki silaha kihalali, alichukuliwa
silaha yake na hakurudishiwa ni vyema akaenda
kituo cha Polisi kwenye eneo lake akiwa na
nyaraka halali za umiliki,” alisema Mwigulu. Kauli
hiyo imekuja kutokana na malalamiko ya
wananchi kwenye maeneo tofauti kuwa wengi
hawajarejeshewa silaha zao
wanazozimiliki kihalali na kuzitumia kwa shughuli
mbalimbali ikiwemo kujikinga na wanyama
wakali.
Lijue Pori la Akiba la Selous
Pori la Akiba linatofautiana kwa kiwango kikubwa
na Hifadhi za Taifa, tofauti kubwa ikiwa ni wakati
Hifadhi za Taifa ni kwa ajili ya utalii, Pori la
Akiba ni kwa ajili ya uhifadhi wa ikolojia
unaokwenda sambamba na utalii mdogo na
uwindaji katika vitalu.
Aidha wakati Hifadhi za Taifa zipo chini ya
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na
nyinginezo, Mapori ya Akiba yapo mbioni kuwa na
Mamlaka yao kutokana na kuundwa kwa
Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) hivi
karibuni.
Likiwa na eneo la kilometa za mraba kati ya
50,000, au asilimia tano ya sehemu ya nchi kavu
ya Tanzania, Pori la Akiba la Selous ni moja ya
maeneo makubwa yaliyohifadhiwa duniani.
Namna ya kufika Pori hilo linaweza kufikika kwa
njia mbalimbali ikiwemo usafiri wa anga kutokana
na kuwepo kwa kiwanja kidogo cha ndege eneo
la Matambwe, usafiri wa Reli ya Tazara hadi
Matambwe ambako ndiko liliko lango kuu la
kuingilia. Unaweza kufika pia kwa barabara
kilometa 300 kutoka Dar es Salaam kupitia
Morogoro au kilometa 310 kutoka Dar es Salaam
kupitia Kibiti mkoani Pwani. Njia nyingine ni
usafiri wa maji katika ukanda wa mkoa wa
Pwani.
Ni pori kubwa kuliko yote Afrika na lenye maji ya
kutosha kiasi kwamba uwezekano wa kuwepo
kwa binadamu kwa ajili ya makazi ungekuwepo,
na hivyo ukweli huo unalifanya pori hilo
kutofautiana na mapori mengine makubwa
yaliyohifadhiwa Afrika.
Mapori kama hayo ni Pori la Namib-Naukluft la
Namibia ambalo sehemu kubwa ni jangwa.
Wageni wanaolitembelea Pori la Akiba la Selous
hujikuta wakiwa katika nyika za asili mbali na
maeneo yaliyozoea mapito ya kitalii.
Wanyamapori waliopo katika pori hilo ni wa
kushangaza, makundi ya wanyama wakiwemo
nyati, tembo, viboko, mbwa mwitu na mamba ni
wakubwa kuliko kote Afrika, lakini pia mfumo wa
mito na maziwa ni wa kipekee katika Afrika
Mashariki.
Pori hilo lina maeneo aina kwa aina yakiwemo
maeneo wazi yenye nyasi fupi, misitu ya miombo,
na misitu kando kando ya mito, lakini pia
mabwawa ambayo ni tegemeo kubwa kwa
wanyama na mimea. Sababu ya kuwa urithi wa
dunia Ni kutokana na sifa hizo Umoja wa Mataifa
ulilipa hadhi Pori la Selous kuwa eneo la Urithi
wa Dunia kutokana na kuwa na ikolojia ya
kipekee, ikidaiwa kuwa ndio pori pekee lililosalia
Afrika likiwa na hali halisi ya kiuhalisia.
Kutokuwepo kwa shughuli nyingi za utalii,
kunachangia kuwepo kwa hali ya nyika na ili
kuhifadhi mazingira hayo na vile vile kuzuia utalii
mkubwa ni utalii mdogo unaodhibitiwa ndio
unaopewa kipaumbele zaidi. Sehemu kubwa ya
Kanda ya Kaskazini ya Selous imetengwa kwa
ajili ya utalii wa picha. Ni moja ya maeneo
mazuri na yenye wanyama wengi.
Kanda hii imepakana na Reli ya Tazara kwa
upande wa Kaskazini. Mashariki ni mpaka wa
pori lenyewe na kwa upande wa Magharibi ni
Stiegler’s Gorge pamoja na barabara iendayo
Matambwe na kwa upande wa Kusini, mpaka ni
Mto Rufiji. Mto mpana wa Rufiji na muelekeo
wake wa kuzunguzunguka, hufanya maeneo
mengi kuwa na ardhi oevu za maziwa na
mabwawa na kufanya ikolojia ya kuvutia.chanzo habar leo.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top