Breaking News
Loading...

Advert

Saturday, October 8, 2016

Kipigo cha mwanafunzi shule ya kutwa mbeya day mengi yaibuka.soma zaid

WANAFUNZI wanne wa ualimu waliomfanyia
ukatili wa kumchapa fimbo na kumpiga makofi
mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya
Sekondari ya Kutwa ya Mbeya (Mbeya Day),
Sebastian Chinguku (17), wamekamatwa na
Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul
Mtinika, walimu hao waliokuwa katika mafunzo
ya vitendo katika shule hiyo ambao ni Franky
Msigwa, Deo John na Evance Sanga wa Chuo
Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE) na
Sanke Gwamaka wa Chuo Kikuu cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere walikamatwa
wakati tukio hilo lililotokea Septemba 28, mwaka
huu katika ofisi ya walimu shuleni hapo
likiendelea kuchunguzwa.
“Walimu wamekamatwa kwa sababu Serikali ina
mkono mrefu na uchunguzi unaendelea
kufanyika,” alisema.
Mtinika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mbeya alisema
wamebaini kuwa shule hiyo ina tatizo kubwa la
utovu wa nidhamu.
Alisema walibaini tatizo hilo baada ya mgomo
baina ya walimu na wanafunzi kutokea shuleni
hapo jana.
Mtinika alisema mgomo huo ulipotokea Serikali
iliingilia kati na kufanikiwa kuumaliza baada ya
walimu kushindwa kufundisha huku wanafunzi
nao wakishindwa kuingia darasani kuendelea na
masomo.
“Leo (jana) asubuhi tulipata taarifa kwamba
baada ya tukio la mwanafunzi Sebastian
kutokea walimu wamegoma kuingia darasani
huku wanafunzi nao walionekana kutokuwa na
mwamko wa kuendelea na masomo hivyo
ilitulazimu kufika na kulitatua tatizo hili,”
alisema Mtinika na kuongeza:
“Ili kuinusuru hali hiyo Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya ya Mbeya kwa niaba ya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla
ililazimika kuingilia kati kulimaliza.
“Ile shule ni kubwa ina wanafunzi 1,467 na
walimu 70 na baada ya kuongea nao tuligundua
kuna tatizo la utovu wa nidhamu na Sebastian
aliyepigwa naye ni miongoni mwa wanafunzi
wasiokuwa na nidhamu na tumewaambia
wafuate taratibu za shule.”
Alisema kitendo cha tukio hilo kusambaa na
kuzua mjadala juzi katika mitandao ya kijamii
huku Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George
Simbachawene, kuingilia kati na kuagiza hatua
za kuwafukuza walimu hao na kuwakamata
ndicho kilichosababisha walimu na wanafunzi
wa shule hiyo kupatwa na mshtuko kushindwa
kuingia darasani.
“Kwa hiyo tumezungumza na walimu na
kuwakumbusha wajibu wao kwa wanafunzi huku
wanafunzi nao tumewaambia kutambua wajibu
wao pindi wakiwa shuleni likiwamo suala la
nidhamu ambalo ndio silaha ya kila kitu,”
alisema.
Mtinika alisema Serikali inafahamu changamoto
wanazokutana nazo walimu lakini ni vema
wakafuata taratibu za kisheria kwa sababu tukio
hilo lilikuwa wazi na halizuiliki, ushahidi
unajionyesha.
“Kama mwanafunzi ni mtovu wa nidhamu,
taratibu zipo na adhabu za kupewa
zimeorodheshwa hivyo hakukua na sababu ya
kupigwa kama mwizi jambo ambalo halikubaliki
nchini kwa sababu hata Katiba yetu
imeelekeza,” alisema.
Kuhusu utekelezaji wa agizo la Simbachawene
la kuitaka Mamlaka ya Nidhamu ya Walimu
kumvua madaraka Mwalimu Mkuu wa Mbeya
Day, Magreth Haule, kutokana na kushindwa
kutoa taarifa ya tukio hilo, Mtinika, alisema
mwalimu huyo ataendelea na majukumu yake
kwa sababu linaendelea kuchunguzwa.
Kwa upande wake, Mwalimu Haule, aliyejitetea
kuwa hakuwapo shuleni na alimkabidhi
majukumu yote Makamu wake, Adonath Nombo,
wakati tukio hilo linatokea na alisema kwa sasa
hawezi kuzungumza chochote bali anasubiri
kutekeleza maagizo yaliyotolewa hadi
atakapopewa muongozo mwingine.
WALIMU WAFUNGUKA
Wakizungumzia sababu ya wao kushindwa
kuingia darasani, baadhi ya walimu wa shule
hiyo walisema mara kadhaa Serikali imekuwa
mstari wa mbele kutatua matatizo
yanayowapata wanafunzi huku wakiwasahau
wao wanaofanyiwa vitendo viovu na wanafunzi.
“Hapa sitetei tukio la Sebastian, ila ninapenda
kuieleza Serikali hasa viongozi wetu wa juu pale
walimu wanapowasilisha matatizo ya wanafunzi
au uongozi wa shule unapotoa adhabu kwa
wanafunzi kama vile kuwasimamisha shule kwa
muda kutokana na matatizo ya nidhamu basi
wasiingilie,” alisema mwalimu mmoja ambaye
aliomba jina lake lihifadhiwe.
WANAFUNZI NAO WANENA
Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na baadhi ya
wanafunzi wa shule hiyo ambao walisema tukio
hilo liliwashtua kwa sababu hawakutarajia kama
mwenzao angeweza kupatiwa adhabu ya namna
hiyo.
“Ni kweli mwanafunzi ana makosa hatukatai
lakini adhabu ya namna ile hakustahili kupewa
kwa sababu sisi tulijua mwalimu amemalizana
naye darasani kwa kumchapa viboko vitano
kumbe, kipigo kiliendelea” alisema Mwanafunzi.
SEBASTIAN AFUNGUKA
Akizungumzia sakata hilo, Sebastian, alisema
adhabu ya pamoja na wanafunzi wenzake
aliitumikia kwa kuchapwa viboko vitano lakini
alishangaa mwalimu aliyemtaja kwa jina la
Franky kumuita pembeni na kuanza kumuuliza
maswali ambayo yeye binafsi anadai alimjibu.
“Mwalimu Franky aliniita pembeni na kuniuliza
kwamba unanikumbuka ? Mimi nikamjibu
hapana, akaniuliza mara nyingine, tena kwa
msisitizo unikumbuki kweli au ni kiburi?
Nikamjibu sikukumbuki,” alisema.
Sebastina alisema baada ya hapo mwalimu
huyo alimwambia kwamba anakumbuka siku ya
mtihani alimwambia avue sweta lake lakini na
siku hiyo alimdharau na alimwamuru amfuate
ofisini.
“Alinipeleka ofisini, huku akiwa na walimu
wenzake na kuanza kuniadhibu kwa kipigo
ambacho nyinyi wenyewe mmekiona na mbali
na hilo walimu hao walinishinikiza niandike
barua ikiwa na maelezo kwamba mimi ndiye
niliye wapiga walimu jambo nililolifanya kwa
kuogopa kufukuzwa shule,” alisema.
Sebastian alisema wakati walimu wa kawaida
wakilijadili suala hilo alionekana amekosa na
kumlazimu kumtamfuta mwalimu ambaye ni
jirani yake na kumweleza ukweli wa tukio lote.
“Mwalimu huyo alifanya upelelezi wake na
kubaini kwamba mimi sikuwapiga walimu bali
walimu ndio walinipiga mimi hivyo kuwaita na
kunitaka mimi nichague adhabu ya kuwapa
lakini niliwaeleza kwamba shule ina utaratibu
wake juu ya walimu wa namna hiyo lakini mimi
binafsi nimewasamehe,” alisema.
DUCE
Akizungumza na gazeti hili kwa sharti la
kutotajwa jina lake gazetini mmoja wa wahadhili
wa DUCE alisema utekelezwaji wa agizo la
Profesa Ndalichako bado haujafanyika na
hakuna kikao chochote cha kiofisi kilichofanyika
jana kwa sababu kwa sasa chuo hicho
kimefungwa.
“Mimi sio msemaji lakini naweza kusema haya
mambo bado yanaongelewa kwenye korido hapa
chuoni kwamba vijana hawa hawana makosa
lakini bado hayajajadiliwa kiofisi, kwa bahati
mbaya suala hili limetokea chuo kikiwa
kimefungwa,” alisema mhadhiri huyo.
Alisema mbali na kuwa vijana hao kitaaluma
wanaonekana hawajafanya kosa kubwa la
kupatiwa adhabu yenye uzito huo lakini agizo la
Profesa Ndalichako lazima litekelezwe kwa
sababu kwa sasa limekaa kisiasa zaidi.
“Kumfukuza mtu chuo sio rahisi kama
mnavyofikiria kuna taratibu zake, wale ni
wanafunzi wamefanya kosa la kawaida ili
wachukuliwe hatua taratibu zilipaswa kuanzia
shule husika walipaswa waandike barua ije
kwenye uongozi wa chuo,” alisema.
Alisema barua hiyo ilipaswa kuwasilishwa katika
kikao cha Bodi ya Uongozi wa DUCE na badaye
taratibu zingetolewa na adhabu zingefuatwa.
Alisema waziri hana mamlaka ya kumfukuza
mwanafunzi chuo hivyo uamuzi uliotolewa
umekaa kisiasa zaidi na msukumo wa mitandao
ya kijamii.
HAKI ELIMU
Shirika lisilokuwa la kiserikali la Haki Elimu
limesema tukio la Sebastian ni sehemu tu ya
matukio mengi ya ukatili wanayofanyiwa
wanafunzi shuleni.
Pia lilisema kuwa kuwa matukio hayo ya kikatili
yamezifanya shule kutokuwa sehemu rafiki na
salama kwa wanafunzi na hivyo kuwa na athari
kubwa katika juhudi zao za kujifunza.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar
es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Haki
Elimu, John Kalage, alisema kwa mujibu wa
utafiti uliofanywa mwaka 2011 na Shirika la
Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa
(UNICEF) kuhusu ukatili dhidi ya watoto
unaonyesha kuwa kuna viwango vya kutisha vya
kikatili dhidi ya watoto katika shule nyingi
nchini.
Alisema vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa
wanafunzi ni pamoja na vitendo vya kingono na
kihisia katika mazingira ya shule za Tanzania na
kwamba walimu ndio vinara wa ukatili huo.
“Kwa mujibu wa utafiti huo nusu ya wasichana
na wavulana ambao wamewahi kunyanyaswa
kimwili (kufinywa, kuchapwa viboko na kupigwa
mateke) waliwataja walimu kuwa ndio
wanyanyasaji wakuu shuleni nchini Tanzania,”
alisema Kalage.
Alisema wamesikitishwa na kitendo cha ukatili
aliofanyiwa Sebastian.
BODI YA MIKOPO
KUSITISHWA KWA MIKOPO YA WANAFUNZI
WALIOHUSIKA KATIKA TUKIO LA KUMDHURU
MWANAFUNZI HUKO MBEYA
Katika hatua nyingine, Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesitisha
mikopo ya elimu ya juu iliyokuwa ikitolewa kwa
walimu-wanafunzi hao waliosimamishwa
masomo kwa kuhusika katika tukio la
Sebastiani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo
vya habari Dar es Salaam jana walimu hao
wamepoteza sifa za kuendelea kupokea mikopo.
“Mikataba inayosainiwa na wanufaika wa
mikopo inawataka wanufaika kuzingatia
masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kuzingatia
nidhamu na kufuata sheria na taratibu za vyuo
na mamlaka halali,” ilisema taarifa hiyo na
kuongeza:
“Kwa mujibu wa taratibu za kukopeshwa,
wanafunzi hawa watatakiwa kuanza kurejesha
kiasi walichokopeshwa mara moja. Bodi ya
Mikopo inawakumbusha wanufaika
wanaoendelea masomo kuzingatia masharti ya
ukopeshwaji na kuheshimu sheria, kanuni
taratibu na kuwa mfano mwema katika jamii.
“Mikopo na ruzuku zinazotolewa na Serikali ni
kwa ajili ya kuwaandaa kuwa raia wema,
waadilifu, na wachapa kazi ili kujenga uchumi
imara na ustawi kwa wote.”
Habari hii imeandikwa na Upendo Fundisha
(Mbeya), Khadia Hamis na Aziza Masoud (Dar
es Salaam)
Source: Mtanzania

0 comments :

Post a Comment

Back To Top