Breaking News
Loading...

Advert

Wednesday, November 16, 2016

Wanafunzi wa secondari mkoani kilimanjaro waongoza kwa mimba.

WANAFUNZI wa shule za sekondari mkoani
Kilimanjaro wanaongoza kukatishwa masomo
kwa kupata ujauzito, baada ya takwimu
kuonesha kuwa kuanzia Januari hadi Oktoba
mwaka huu, jumla ya wanafunzi 216 wamepewa
ujauzito.
Wakati hiyo ikitishia mustakabali wa maisha yao
ya baadaye, kwa wenzao wa shule za msingi ni
tisa tu waliopewa ujauzito katika kipindi hicho
kufanya jumla iwe 225.
Mkuu wa mkoa huo, Saidi Mecky Sadiki alisema
hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Kamati
ya Ushauri cha Mkoa (RCC) ambacho kimelenga
kujadili masuala ya maendeleo ya mkoa katika
sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya,
miundombinu, uchumi na kilimo.
“Nimelileta kwenu hili suala la ubakaji na ulawiti
hususani kwa wanafunzi wetu wanaopewa
mimba za utotoni ili tujadiliane na tuweke
azimio madhubuti...hali ni mbaya na tukikaa
kimya tutasababisha balaa kubwa na kuathiri
hali ya taaluma,” alisema mkuu wa mkoa.
Pamoja na tatizo la mimba, lakini pia mkoa una
upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa
1,875 ambavyo kwa shule za msingi ni vyumba
1,531 na vyumba 344 kwa sekondari.
Mkuu wa Mkoa alisema takwimu zinaonesha
kuwa Wilaya ya Hai inaongoza kwa upungufu wa
vyumba 493, ikifuatiwa na Same vyumba 378,
Mwanga vyumba 337, Moshi vyumba 275, Siha
216, Manispaa 119 na Rombo ni vyumba 57.
Kuhusu tatizo la uharibifu wa mazingira, Sadiki
alisema mwezi uliopita kumekuwepo na tatizo la
wananchi kuwasha moto katika misitu ambapo
jumla ya hekta 3,500 ziliungua katika Msitu wa
Hifadhi ya mlima Kilimanjaro eneo la Shira,
Msitu wa Chome/Shengena na Msitu wa
Kindoroko.
Akizungumzia mpango wa matumizi bora ya
ardhi, mkuu wa mkoa alitaka halmashauri zote
kupunguza migogoro isiyo ya lazima baina ya
wafugaji na wakulima huku akitaka watendaji
kutoegemea upande mmoja. Alisema baadhi ya
migogoro inachochewa na tabia ya watendaji
kuegemea upande mmoja na hivyo kuchochea
migogoro.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top