Wananchi wazidi kulilia Bunge 'live 'soma zaid
MAHITAJI ya wananchi kutaka matangazo ya
Bunge la Muungano kuonyeshwa moja kwa moja
katika vituo vya televisheni na redio yamezidi
kushika kasi, imebainika.
Utafiti uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania
(MCT) umeonyesha asilimia 92 ya wananchi
wanaona kuna umuhimu wa matangazo hayo ya
Bunge kurushwa moja kwa moja huku asilimia
79 wakipinga uamuzi wa Serikali kuyafuta
matangazo hayo.
Akizindua ripoti kuhusu kusimamishwa kwa
matangazo ya moja kwa moja ya Bunge,
Mkurugenzi wa MCT, Pili Mtambalike, alisema
hatua hiyo inakandamiza uhuru wa habari na
haki ya kupata taarifa.
Katika ripoti hiyo ambayo pia imenukuu utafiti
uliowahi kufanywa na Taasisi ya Twaweza ya
Dar es Salaam, Mtambalike alisema utafiti huo
uligundua kuwa wananchi wengi walioulizwa
walilalamika na kusema kuwa baada ya
kufungiwa matangazo hayo hawajui kitu gani
kinaendelea ndani ya Bunge.
Alisema katika utafiti huo, watu wanane kati ya
10 hawajakubaliana na kufungwa matangazo
hayo huku tisa kati ya 10 wanaona kuna
umuhimu matangazo hayo yakarudishwa.
“Ripoti hii inapendekeza matangazo hayo
yarudishwe yaweze kuwasaidia wananchi wa
kawaida kufuatilia mijadala mbalimbali ya
bunge.
“Waandishi wa habari za bunge pia wajengewe
uwezo waweze kuandika habari hizo kwa weledi
mkubwa.
“Ripoti hii inapendekeza pia kuwa kanuni za
Bunge zitumike katika kukomesha tabia
zisizotakiwa bungeni badala ya kuvilaumu
vyombo vya habari vinapokuwa vikitoa habari
na kuonyesha kinachoendelea bungeni,”alisema
Mtambalike.
Ripoti hiyo imetoa mapendekezo kwa uongozi
wa Bunge hilo kutaja hadharani gharama halisi
za kurusha matangazo hayo ya moja kwa moja
ili wananchi waelewe.
“Tunapendekeza kuwapo mfuko maalum
utakaojulikana kama Fedha za Matangazo ya
Bunge (BBF) unaojitegemea, ambao utapata
fedha kutoka nje na ndani ya Bunge,” alisema
Mtambalike.
Ripoti hiyo pia imesema kuwa si kweli kwamba
utaratibu wa kurusha matangazo hayo
haufanywi na Nchi za Jumuiya ya Madola kama
ilivyoelezwa na Waziri wa Habari Utamaduni na
Michezo, Nape Nnauye wakati akielezea sababu
za kufunga matangazo hayo.
“Katika utafiti huu tumegundua kuna nchi sita
duniani ambazo zinaruhusu urushwaji wa moja
kwa moja wa redio na runinga kama Australia,
Uingereza, Canada, New Zeland na Samoa
ambako redio ya taifa inalazimishwa na sheria
kutangaza kila siku au kwa wiki, jinsi Bunge
linavyofanya kazi yake zake,” ilisema sehemu ya
ripoti hiyo.
0 comments :
Post a Comment