Mkaguzi wa vyeti feki naye atajwa katika waliogushi vyeti.soma zaid
Dar es Salaam. Muosha huoshwa. Ndivyo ilivyo
kwa mmoja wa wahakiki wa vyeti vya elimu
katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
Mkaguzi huyo naye ametajwa katika orodha ya
watumishi wanaotuhumiwa kuwa na vyeti vya
kughushi.
Hatua hiyo imekuja baada ya kumaliza kwa
mafanikio kazi ya kuhakiki wafanyakazi wengine
iliyomsababishia lawama na sasa ni mmoja wa
wanaotakiwa kuondoka kazini kabla ya Mei 15.
Mkaguzi huyo aliyetajwa kwa jina la Adolph
Shayo, jina lake ni namba 1,023 katika orodha ya
watumishi 9,932 iliyokabidhiwa kwa Rais John
Magufuli Aprili 28.
Baada ya kupokea majina hayo kutoka kwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi wa
Umma na Utawala Bora), Rais Magufuli aliagiza
wote waliotajwa waondoke vituo vyao vya kazi
kabla ya Mei 15 na watakaokaidi wafikishwe
mahakamani, ambako wanaweza kukumbana na
kifungo cha miaka saba.
Pengine sio ajabu kutajwa kwenye orodha hiyo
kwa kuwa ukaguzi wa vyeti haukuacha mtu au
cheo, lakini kugundulika kwake kunaibua maswali
zaidi katika uhakiki huo ambao tayari
umeshaonyesha dosari kama ya kutaja baadhi
kuwa wana vyeti vya kughushi vya elimu ya
sekondari wakati hawakuviwasilisha kwenye
uhakiki uliofanyika.
Kutajwa kwa Shayo kunaweza kuibua utata
mwingine wa usafi wa uhakiki kutokana na
ukweli kuwa utakuwa umefanywa na mtu ambaye
hakustahili kuhakiki wengine.
Shayo alijipatia sifa ya kuwa mkali na msumbufu
wakati wa uhakiki, akidaiwa kuwataka mara kwa
mara watumishi wenzake kumpelekea vyeti.
Mmoja wa waliokaguliwa na Shayo, ambaye
aliomba jina lake lihifadhiwe alisema walimu
walipata shida wakati wa uhakiki kwa sababu
walikuwa chini ya mhakiki huyo.
Alisema alishangazwa kusikia amekuwa mmoja
wa watu waliotajwa kuwa na vyeti vya kughushi
wakati yeye pia alihusika kuhakiki.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Nassib
Mmbaga alisema baada ya ukaguzi kufanyika
ilibainika kuwa vyeti vyake vilikuwa na matatizo
(ambayo hakuyataja) na wakamtaka kuthibitisha,
lakini hakufanya hivyo.
“Ni kweli alikuwa mtumishi katika idara ya elimu
na msaidizi katika kitengo cha bohari ya
manispaa, lakini lilipokuja suala la ukaguzi wa
vyeti ilibidi afanye kazi kama msaidizi,” alisema.
“Hata kama ni mkaguzi ni lazima akaguliwe. Hata
mimi (mkurugenzi) nilikaguliwa. Lakini
tulivyokagua vyeti vyake (Shayo) tuligundua vina
shida,” alisema.
Alisema pamoja na kupewa nafasi ya kuthibitisha
uhalali wa vyeti vyake, alishindwa kufanya hivyo
hadi majina yalipotangazwa.
Mkurugenzi huyo alisema hadi sasa amepokea
zaidi ya barua 60 za rufaa, lakini hajaona jina la
Shayo.
Sakata la vyeti feki limezidi kuchukua sura mpya
baada ya baadhi ya waliotajwa kuamua kwenda
vyama vya wafanyakazi kudai wameonewa.
Mmoja wa waliochukua hatua hiyo ni mratibu wa
elimu wa Wilaya ya Chamwino, ambaye pia ni
mwenyekiti wa CCM, Charles Ulanga ambaye
hajawahi kusoma elimu ya sekondari.
Ulanga anadai kuwa hakuwahi kuwasilisha vyeti
vya sekondari wakati wa ukaguzi na hivyo
anataka kujua wahakiki walivitoa wapi.
Katika Manispaa ya Temeke, jumla ya watumishi
walioghushi vyeti ni 270, kati yao 120 wakitoka
idara ya afya huku Hospitali ya Rufaa ya Temeke
ikiongoza kwa kuwa na watumishi 53.
Pia, Shule ya Msingi ya Mbagala imetoa walimu
saba.
Kuhusu athari za matokeo ya uhakiki huo,
Mmbaga alisema zinazidi kujitokeza kutokana na
kupunguza idadi ya watumishi katika hospitali na
shule. “Tunajaribu kujaza nafasi za watoa
huduma kutoka katika zahanati ambazo
hazihudumii watu wengi ili huduma zisisimame,”
alisema.
0 comments :
Post a Comment