Necta ichunguzwe vyeti feti.soma zaid
Sakata la watumishi waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi sasa limegeukia kwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) na wataalamu wa Wizara ya Elimu wakituhumiwa kufanya vibaya uhakika na kusababisha wasiohusika kuwemo katika orodha iliyokabidhiwa kwa Rais John Magufuli. Pia waajiri ambao wafanyakazi wao wamekutwa na vyeti vya kughushi wametakiwa waadhibiwe kwa kutokuwa makini wakati wa uajiri. Watumishi 9,932 wa Serikali na taasisi za umma walibainika kuwa na vyeti vya kughushi au kutumia vyeti vya watu wengine vya elimu ya sekondari kupata nafasi ya kuendelea na masomo. Wote waliobainika katika uhakiki huo wametakiwa kuwa wameshaachia ofisi ifikapo leo, lakini Kambi ya Upinzani Bungeni juzi iliinyooshea kidole Necta na wataalamu wa wizara hiyo kuwa walihusika katika kufanikisha kutolewa kwa vyeti feki na kutaka wachunguzwe. Msemaji wa kambi hiyoanayeshughulikia elimu, Suzan Lyimo alisema wakati akitoa maoni yao kuwa uhakiki uliofanywa na Serikali ulikuwa na upungufu mwingi ambao unaweza kusababisha baadhi ya watu kutotendewa haki. “Mathalan, baadhi ya taarifa ambazo kambi rasmi ya upinzani bungeni inazo ni kuwa zoezi hilo halikuzingatia watumishi ambao wakati uhakiki unafanyika walikuwa likizo, wagonjwa, walimu walioajiriwa katika mpango wa Upe waliokuwa masomoni au waliokuwa nje ya vituo vya kazi,” alisema Suzan. “Hivyo kitendo cha mtumishi kutokuwapo katika kituo cha kazi na kuwasilisha nakala halisi ya cheti kulihesabiwa kuwa mtumishi huyo ana cheti cha kughushi jambo ambalo limewaathiri watumishi wengi ambao wana vyeti halisi.” Msemaji huyo alisema kambi hiyo inaitaka Serikali kufanya uamuzi haraka dhidi ya rufaa zilizowasilishwa na watumishi ambao kwa namna moja ama nyingine wameona kuwa hawajatendewa haki. “Ni dhahiri kuwa Serikali ina vyombo vya ulinzi na usalama na kimsingi walikuwa wanafahamu kuwepo kwa vyeti vya kughushi katika utumishi wa umma, lakini hatua zilichelewa kuchukuliwa kutokana na uzembe ndani ya Serikali,” alisema. Suzan, ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu (Chadema), alisema pamoja na utambuzi wa matakwa ya kisheria ya watumishi walioghushi vyeti, kambi hiyo inaishauri Serikali kuwa na jicho la huruma kwa waliokumbwa na kashfa hiyo kwa kuwalipa angalau michango waliyokuwa wanachangia katika mifuko ya jamii ili waweze kuendelea kuishi wakati wakijipanga kwa maisha mengine. Alisema kambi hiyo inatambua kuwa kabla ya usajili, waombaji wa ajira hutakiwa kupeleka vyeti vyao vya taaluma kwa mwajiri kama kigezo mojawapo cha kukidhi masharti ya usaili. “Zaidi ya hapo mwajiriwa mpya hutakiwi tena kupeleka nakala ya vyeti vyake halisi kwa mwajiri kwa ajili ya uhakiki na hatimaye mwajiriwa huyo kuthibitishwa kazini,” alisema. Alisema haiwezekani katika hatua zote hizo mwajiri asitambue mapungufu ya vyeti vya taaluma ya mwajiriwa wake kwa muda wote halafu mapungufu haya yaje kutambuliwa na uhakiki huu uliofanyika hivi karibuni. “Lazima kuna tatizo, ama la uzembe wa waajiri au rushwa katika zoezi la uajiri. Kwa sababu hiyo kambi rasmi ya upinzani bungeni inataka Serikali kuwawajibisha waajiri wote ambao wafanyakazi wao wamekutwa na vyeti vya kughushi,” alisema. Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako alisema Necta ilifanya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma wa serikali za mitaa, taasisi, mashirika ya umma, wakala wa serikali.
0 comments :
Post a Comment