Breaking News
Loading...

Advert

Saturday, March 19, 2016

Wachina wahukumiwa miaka 30 jela au kulipa faini billion 108.


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu
imewahukumu Wachina wawili kulipa faini ya Sh
bilioni 108 au kifungo cha miaka 30 jela baada ya
kukutwa na vipande 728 vya meno ya tembo bila
kibali.
Pia mahakama hiyo imeamuru kutaifishwa kwa
magari matatu ya washtakiwa hao mawili yakiwa
aina ya Noah yaliyodaiwa kutumika kubeba meno
hayo.
Akitoa hukumu hiyo mahakamani hapo jana,
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyporiani Mkeha,
alisema washtakiwa hao wametiwa hatiani katika
mashtaka mawili kati ya matatu yaliyowakabili
ambayo ni kukutwa na meno hayo bila kibali na
kujaribu kutoa rushwa ya Sh 30,250,000 kwa
askari walioenda kuwakamata.
“Katika shtaka la kukutwa na meno hayo bila
kibali, kila mshtakiwa atatakiwa kutumikia
adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela au kulipa
faini ya shilingi 54,358,650,000,” alisema Hakimu
Mkeha.
Alisema kwa shtaka la kujaribu kuhonga askari,
kila mshtakiwa ametakiwa kulipa faini ya Sh
milioni moja au kwenda jela miaka mitano na
adhabu hiyo itakwenda pamoja.
Alisema amezingatia hoja za pande zote mbili
lakini kulingana na ushahidi uliotolewa
mahakamani hapo hasa jinsi nchi inavyopoteza
idadi ya tembo na hasara iliyopatikana.
“Hii ni kesi inayostahili kutolewa adhabu ya
kiwango cha juu kulingana na ushahidi uliotolewa,
mahakama imeridhika kwamba upande wa
mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi
ya washtakiwa na washtakiwa hawakuweza
kuwajibika ipasavyo kuutia matundu ushahidi wa
upande wa mashtaka,” alisema Hakimu Mkeha.
Alisema kutokana na hali hiyo ndiyo maana
washtakiwa hao wanatiwa hatiani kwa makosa
hayo mawili.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa
Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, aliiomba
mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa washtakiwa
hao kwa sababu kitendo chao kimesababisha
kuuawa kwa takribani tembo 226.
Nchimbi alisema inaonekana washtakiwa hao
walikuwa vinara wa vitendo hivyo vya ujangili
kwa kuwa tangu wakamatwe hakujatokea
watuhumiwa wengine kukamatwa na idadi kubwa
ya meno ya tembo kama wao tangu kuanzia
mwaka 2010 hadi 2014.
“Watuhumiwa hawa hawahitaji huruma ya
mahakama kwa kuzingatia ukubwa wa kosa
walilotenda, tembo waliouawa ni sawa na robo ya
idadi ya tembo 892 wanaodaiwa kuuawa nchini
kuanzia mwaka 2012 hadi 2013 na kwa mujibu
wa takwimu za taifa wanyama hawa kama
wangekuwepo taifa lingeingiza pato lake katika
sekta ya utalii,” alisema Nchimbi.
Kwa upande wake wakili wa utetezi, Nehemia
Nkono, aliiomba mahakama hiyo iwahurumie
washtakiwa hao kwa kuwa ni wakosaji kwa mara
ya kwanza huku akikanusha kuwa wao ndio
vinara wa vitendo vya ujangili.
Washtakiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 2,
2013 katika Mtaa wa Kifaru uliopo Mikocheni
wilayani Kinondoni, Dar es Salaam. Ilidaiwa kuwa
washtakiwa hao walikutwa na vipande vya meno
hayo vyenye uzito wa kilo 1,880 ambavyo vina
thamani ya Sh 5,435,865,000 na walivimiliki bila
kibali cha Serikali.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top