Mwongozo wa majukumu ya mawaziri umekamilika.soma zaid
SERIKALI imekamilisha mwongozo wa majukumu
ya mawaziri (instrument) na kwamba muda
wowote itatangaza katika gazeti lake, Bunge
limeelezwa.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, wakati akijibu hoja za wabunge
waliochangia hotuba ya bajeti ya ofisi yake ya
makadirio ya fedha kwa mwaka 2016/17.
Majaliwa alisema kwa mamlaka aliyonayo Rais
alianza kuunda Baraza la Mawaziri na baadaye
makatibu wakuu ambao ndio watendaji wakuu wa
Serikali.
“Ili kuwe na uwezo wa kutengeneza hiyo
instrument, ikikamilishwa lazima itangazwe
kwenye gazeti la Serikali, nataka niwape faraja
kwamba tayari instrument hizi zimeshakamilika
na zimesainiwa Aprili 20, mwaka huu, muda
wowote Rais atakapoamua atatangaza.
“Mawaziri walioko wanafanya kazi kwa mujibu
wa maelekezo ya rais na watendaji wanafanya
kazi kwa mujibu wa instrument hii,” alisema.
Kauli hiyo ya Serikali imekuja siku chache baada
ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni,
Freeman Mbowe, kugoma kuwasilisha maoni ya
kambi hiyo akitoa hoja tatu zilizosababisha
kuchukua uamuzi huo.
Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na kupinga
hatua ya Serikali ya Rais Dk. John Magufuli
kufanya kazi bila ya kuwa na mwogozo wowote
wenye msingi halali wa kisheria katika wizara
zake.
Hoja nyingine ni uvunjaji wa Katiba na sheria za
nchi kuhusu bajeti na Serikali kupoka madaraka
na uhuru wa mhimili wa Bunge.
Mbowe alilieleza Bunge kuwa kambi yake
haitakuwa tayari kuendelea kushiriki uvunjaji wa
Katiba, sheria na haki za msingi za wananchi na
kwamba wanatafakari kwa kina hatua za kufuata.
Alisema kutokana na kukosekana kwa mwongozo
halali wa kisheria katika wizara mbalimbali,
inaonyesha Rais Magufuli hajaiunda kihalali
serikali yake.
Akifafanua hilo Mbowe alisema kiongozi huyo wa
nchi ameshindwa kutekeleza sheria ya
utekelezaji wa majukumu ya mawaziri ya mwaka
1980, ambayo inaweka masharti ya kutengeneza
mwongozo wa muundo na utekelezaji wa
majukumu ya Serikali yake.
Alisema sheria hiyo inamtaka Rais kila
anapounda Baraza la Mawaziri kuchapisha katika
gazeti la Serikali kueleza jinsi Serikali yake
itakavyotekeleza majukumu yake, jambo ambalo
halijafanyika na badala yake Serikali imekuwa
ikifanya kazi kwa kauli za Rais na mawaziri bila
kufuata mwongozo wowote.
“Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mawaziri
ya mwaka 1980, kifungu cha 5(1) kinaweka
masharti kwa Rais kutengeneza mwongozo wa
muundo na utekelezaji wa majukumu ya Serikali
yake.
“Mpaka sasa mwongozo wa utendaji wa Serikali
kwa kila wizara (Instrument) unaotumika ni ule
uliochapishwa kwenye gazeti la Serikali namba
494A la tarehe 17/12/2010,” alisema Mbowe.
0 comments :
Post a Comment