Breaking News
Loading...

Advert

Sunday, May 15, 2016

Baada ya MCC kusitisha msaada kwa tanzania serikali ya uingereza yaahidi kuisaidia tanzania sekita ya umeme vijijini.soma zaid.


Uingereza Kusaidia Usambazaji wa
Umeme Vijijini.
Miezi michache baada ya Shirika la
Marekani la Changamoto za Milenia
(MCC) kujitoa kusaidia Tanzania katika
usambazaji wa umeme vijijini, Serikali ya
Uingereza kupitia taasisi yake ya Energy
Africa Initiative, imetangaza utayari wa
kutoa msaada huo.
Waziri wa Uingereza wa Maendeleo ya
Kimataifa, Justine Greening, ameeleza
utayari huo mwishoni mwa wiki, katika
mazungumzo yake na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, aliye nchini humo
kumwakilisha Rais John Magufuli, katika
mkutano wa kimataifa wa kupambana na
rushwa duniani. Katika mazungumzo
hayo, Greening alimhakikishia Waziri
Mkuu Majaliwa, kwamba nchi yake iko
tayari kuisaidia Tanzania kwenye mpango
wake wa kupeleka umeme vijijini.
“Tuko tayari kuwasaidia kutekeleza
mpango huu kupitia taasisi ya Energy
Africa Initiative ambayo inapata ufadhili
kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo
la Uingereza (DFID),” alisema.
Pia Waziri huyo wa Uingereza, alipongeza
hatua zinazochukuliwa na Serikali ya
Awamu ya Tano katika kupambana na
rushwa na kwamba ndiyo maana
Tanzania ilipewa mwaliko maalumu wa
kushiriki mkutano huo, kwa vile baadhi
ya mataifa yanaziona juhudi
zinazofanywa na Serikali ya Rais
Magufuli.
Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza
Waziri Mkuu kwa nia ambayo Serikali ya
Awamu ya Tano imeionesha katika kuwa
na mpango wa kuendeleza viwanda.
Nguvu mpya Rea
Hatua hiyo ya Uingereza, imekuja wiki
moja kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti ya
Wizara ya Nishati na Madini Alhamisi wiki
ijayo, ambayo mjadala wake utafanyika
kwa siku mbili za Alhamisi na Ijumaa,
unatarajiwa kuibua hoja ya kufutwa kwa
msaada huo wa MCC wa Dola za Marekani
milioni 472, uliokuwa utumike kusambaza
umeme vijijini.
Mbali na mjadala huo ambao unatarajiwa
kung’ang’aniwa na Kambi ya Upinzani
Bungeni, hatua hiyo ya Uingereza
itaongeza nguvu katika jitihada za
Serikali zilizokwishaanza kwa mafanikio
za kuwapatia Watanzania umeme wa
uhakika.
Taarifa za Wakala wa Umeme Vijijini
(Rea) zinaonesha kuwa, pamoja na MCC
kujitoa Machi mwaka huu katika
usambazaji umeme, Serikali katika Bajeti
ya 2015/ 2016 inayoisha Juni mwaka
huu, ilikuwa imeshatenga Sh bilioni 950
kwa ajili ya mradi wa Rea Awamu ya Pili.
Mradi huo wenye lengo la kufikisha
umeme kwa vijiji 2,500 na kuunganishia
nishati hiyo wateja 250,000 nchi nzima,
unatarajiwa kukamilika Juni 30, mwaka
huu na kupisha kuanza kwa Rea Awamu
ya Tatu, ambayo itaanza Julai mosi na
kumalizika baada ya miaka miwili.
Jitihada zote hizo, lengo lake ni
kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ya 2015-2020, ambayo inataka
hadi ifikapo mwaka 2020, wananchi
waliounganishwa na umeme wafikie
asilimia 60 na kiwango cha uzalishaji
kifike megawati 4,915.
Mbali na malengo ya Ilani hiyo, jitihada
hizo pia zitachangia katika kutekeleza
Dira ya Maendeleo ya Taifa inayotaka
Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2025, ambayo imeweka
lengo la usambazaji umeme liwe asilimia
50 mwaka huo mwaka 2025 na asilimia
70 mwaka 2033.
Tayari Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo,
ameshaelezea nia ya Serikali kutaka
sekta ya nishati itoe mchango mkubwa
kufikia uchumi huo wa kati, kwa kuwa
rasilimali za kufikia lengo hilo kupitia
nishati zipo na kinachotakiwa ni dhamira
na kasi ya kutekeleza.
Katika kusisitiza kasi na dhamira hiyo ya
Serikali, Waziri huyo amekuwa akielezea
mafanikio yaliyopatikana katika
utekelezaji wa dira hiyo, iliyotaka ifikapo
mwaka 2015 uunganishaji umeme uwe
umefikia asilimia 30. Lakini, kutokana na
utekelezaji madhubuti wa dira hiyo,
kiwango hicho kilivukwa lengo na kufikia
asilimia 40 mwaka 2015.
JPM na Marekani
Mbali na msaada huo wa Uingereza
katika kusambaza umeme vijijini, Serikali
ya Marekani pia imeelezea kuvutiwa na
utendaji wa Rais Magufuli katika
kupambana na rushwa, hatua iliyoanza
kuvutia wawekezaji wa nchi hiyo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa
Marekani anayeshughulikia Masuala ya
Kimataifa, Sarah Sewall, katika
mazungumzo yake na Waziri Mkuu
Majaliwa nchini Uingereza katika mkutano
huo wa kimataifa, ameipongeza Tanzania
kwa kupiga hatua katika mapambano
dhidi ya rushwa.
Alisisitiza kuwa kampuni nyingi za
Marekani, zimeonesha nia ya kuja
kuwekeza Tanzania. “Ninaamini uwekezaji
huu utasaidia kuleta maendeleo ya
kiuchumi na kijamii kwa watu.
Tunampongeza Rais Dk Magufuli kwa
juhudi anazofanya na nipende kusisitiza
kwamba ushirikiano baina ya Tanzania na
Marekani utaendelezwa katika maeneo
yetu ya siku zote,” alisema.
Majaliwa ashukuru
Akizungumza katika kikao chake na
Waziri Sewall, Waziri Mkuu Majaliwa
alimsisitiza asiache kusaidia kuwahimiza
Wamarekani wengi waje kutalii Tanzania
na wawekezaji zaidi waje kuwekeza
nchini katika nyanja mbalimbali, ikiwemo
uanzishaji wa viwanda, uongezaji thamani
kwenye mazao yanayozalishwa nchini.
Alimhakikishia kuwa Watanzania
wamekuwa wakijifunza teknolojia mpya
na za kisasa.
Kuhusu mafanikio katika mapambano na
rushwa, Majaliwa alisema mkutano huo
wa kimataifa, uliojadili jinsi ya
kupambana na rushwa duniani, ni
kiashiria tosha kwamba tatizo la rushwa
ni kubwa na linataka juhudi za pamoja
katika kukabiliana nalo.
Akizungumza na mawaziri hao, Waziri
Mkuu Majaliwa alisema kwamba viongozi
wa Serikali wa Awamu ya Tano,
wameamua kwa dhati kupambana na kila
ovu, linalotokana na janga la rushwa na
wameamua kuwajibika na kuachana na
tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
“Sasa hivi nchi yetu ina utamaduni mpya
wa kufanya kazi na tumeamua kufanya
kazi kwelikweli na siyo tena kwa mazoea,
tumeamua kuweka utamaduni mpya wa
kupiga vita rushwa, ili kuleta uwajibikaji
na uwazi miongoni mwa watu wetu,”
alisema.
Alipoulizwa nini kimechangia kufanya
Tanzania ing’are kimataifa katika vita
hiyo, Waziri Mkuu alijibu kwamba
Tanzania imetumia mambo manne
ambayo ni kuzuia rushwa isitolewe ama
kupokelewa, kampeni za kuelimisha jamii,
kufanya mapitio ya sheria na kuwepo
kwa utashi wa kisiasa.
“Serikali inachukua hatua za kiutawala na
kisheria, kama vile kuanzisha Mahakama
Maalumu ya Mafisadi ambayo inatarajiwa
kuanza kazi Julai mwaka huu,” alisema
Waziri Mkuu.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top