Kilichotokea UDOM kwa kufukuzwa wanafunzi mapya yaibuka.soma zaid.
JUMUIYA ya Wanataaluma ya Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOMASA) imesema kilichotokea si
walimu kugoma kufundisha programu ya
Stashahada Maalumu ya Elimu, Sayansi, Hisabati
na Tehama, bali tatizo ni kutoelewana na
Menejimenti ya chuo kutokana na mazingira
mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo chuoni
hapo.
Aidha, imelaani kitendo cha wanafunzi 7,802 wa
Programu Maalumu ya Ualimu wa Msingi na
Sekondari, waliorudishwa nyumbani bila kupewa
muda wa kutosha kujiandaa kwa kuzingatia umri
wao na mazingira waliyokuwa wanaishi, hali
inayofanya wazagae mitaani huku wakiwa
hawana pa kwenda.
Hayo yako kwenye tamko lililotolewa jana na
Katibu wa jumuiya hiyo, Lameck Thomas, ambalo
lilieleza kuwa lawama zimekuwa zikitupwa kwa
walimu kutokana na taarifa hizo kutolewa na
upande mmoja, ambao ni Menejimenti ya chuo
kwenda serikalini bila kuwepo na taarifa yoyote
kutoka kwa walimu kupitia jumuiya yao.
Thomas alisema si kweli kama walimu waligoma
kufundisha lakini tatizo kubwa ni kutoelewana
kati ya walimu na Menejimenti ya chuo kutokana
na mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu
hiyo chuoni hapo.
Hatuzungumzii fedha zaidi tunazungumzia suala
la kuboresha elimu ili taifa lipate walimu wa
baadaye katika kufundisha Sayansi, Hisabati na
Tehama, vifaa vya kufundishia navyo ni
changamoto kubwa,” alisema.
Katibu huyo alisema kama Jumuiya ya
Wanataaluma wanapata hisia kwamba Wizara ya
Elimu, imeamua kwa makusudi kushirikiana na
uongozi wa chuo kupotosha uhalisia wa jambo
hilo kwani hakuna hata wakati moja ambao
wamefanya mawasiliano na walimu wenyewe
kupata ukweli kutoka upande wao.
“Alichosema waziri bungeni juzi ni taarifa ya
upande moja ambayo haitatupeleka kwenye
utatuzi wa kudumu wa suala hili kutokana na
ukweli kwamba walimu nao wana mengi ya
kuzungumza,” alisema katibu huyo.
Alisema serikali imejenga desturi ya kuonana na
menejimenti za vyuo pindi yanapotokea matatizo
bila kupata taarifa kutoka vyanzo vingine hali
ambayo imekuwa inasababisha vyanzo sahihi vya
matatizo kutojulikana kwa uwazi.
Alisema changamoto za ufundishaji kutokana na
uhaba na walimu kulingana na idadi ya wanafunzi
waliopo. Akitoa mfano alisema kwa sasa Chuo
cha Sayansi Asilia na Hesabu, kina upungufu wa
walimu 128 waliokuwa wanahitajika kufundisha
programu hiyo kwa ufanisi; na kwa muhula
uliopita walimu 72 tu ndio walibeba mzigo wa
upungufu huo na muhula huu hali ilikuwa
inaelekea kuwa mbaya zaidi.
“Wingi wa wanafunzi na uhaba huu wa walimu
ulisababisha upangaji wa ratiba na kufundisha
kutokana na ukweli kwamba kozi ziligawanywa
katika mikondo mingi ambayo walimu
walilazimishwa kuifundisha huku wakiwa na
majukumu ya kufundisha kozi za shahada na
majukumu mengine,” alifafanua.
Alisema chuo kimekuwa na desturi ya kupokea
wanafunzi wengi bila kuzingatia idadi ya walimu
waliopo na miundombinu ya kufundishia na
kujifunzia na hiyo si mara ya kwanza kwa chuo
kufanya hivyo, kwani mwaka 2008 walileta
wanafunzi wengi ambao matokeo yake walimu
kufundisha masomo mengi kuliko uwezo wao wa
kazi.
Alisema taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Naibu
Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma ilipotoshwa,
kwani haijaeleza ukweli wa madai uliowasilishwa
na chuo husika. Alisema katika Chuo cha Sayansi
Asilia na Hesabu taarifa inasema
yaliyowasilishwa ni madai ya Sh milioni 367.8 na
kupungua mpaka Sh milioni 90 wakati uhalisia ni
kwamba madai hayo hata yangebanwa namna
gani yasingepungua mpaka chini ya Sh milioni
223.7.
Alisema mfano mwingine ni Chuo cha Elimu
Masafa na Sayansi za Kompyuta ambao taarifa
inasema waliwasilisha madai yanayozidi Sh
milioni 100 wakati taarifa ya chuo inasema ni
madai ya Sh milioni 53.7 tu.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Edson Baradyana
alisikitishwa na yaliyotokea na kuitaka serikali
kufanya jitihada za makusudi ili kumaliza
mgogoro huo na hilo litawezekana kama walimu,
wanafunzi na Menejimenti kukaa pamoja.
Baradyana alisema wanafunzi hawakutendewa
haki kwani ilitolewa notisi ya ghafla ya kuondoka
chuoni huku wengine wakiwa hawana nauli na
hawakujua pa kwenda hali inayofanya waendelee
kuzurura mitaani.
Alisema wanaamini kama Menejimenti ya chuo
ingeonesha ushirikiano wa karibu kwa walimu
wanaofundisha programu hiyo na kushirikiana,
hayo yasingetokea au yasingekuwa makubwa
kiasi hicho.
“Lazima kuangaliwa na kutatuliwa kwa
changamoto nyingine zilizoibuliwa na
wanataaluma na wanafunzi katika uendeshaji wa
programu hiyo badala ya kujikita kwenye suala la
malipo tu, serikali iwe na utaratibu wa
kuwasiliana na walimu na wanafunzi mara
kunapotokea matatizo vyuoni ili kupata taarifa
toshelezi kutoka pande zote,” alisema Mwenyekiti
wa Udomasa.
Aidha, wakati wa kurejeshwa nyumbani kwa
wanafunzi hao wa Udom kukibebwa kisiasa na
vyama vya upinzani, taarifa ya serikali imeeleza
kuwa wahadhiri waliogoma, walitaka kulipwa
posho ya zaidi ya Sh milioni 900.
Akitoa taarifa ya pili bungeni juzi usiku, Waziri
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako (pichani)
alisema wanafunzi hao si sehemu ya kazi zilizoko
katika mikataba ya ajira ya wahadhiri hao, ila ni
sehemu ya kazi ya ziada.
Kwa kuwa kazi hiyo ni ya ziada, Profesa
Ndalichako alisema walikubaliana walipwe posho
ya kazi ya nyongeza ambayo uongozi wa Chuo
Kikuu cha Dodoma ulikuwa tayari kutoa zaidi ya
Sh milioni 200.
Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, wahadhiri
hao walisisitiza kuwa wanataka posho hiyo iwe
zaidi ya Sh milioni 900, jambo lililokataliwa na
Mkaguzi wa Ndani wa Mahesabu wa Udom
aliyesema kuwa kiwango hicho ni kikubwa kuliko
uhalisia wa kazi yenyewe.
Kutokana na kutokubaliana kati ya wahadhiri hao
na uongozi wa Udom, wahadhiri hao ndio
wakaitisha mgomo wa kufundisha wanafunzi hao
huku wakiendelea na kazi za kufundisha walio
katika programu za shahada ya kwanza na
kuendelea.
Profesa Ndalichako alisema kwa uamuzi huo wa
wahadhiri, serikali isingeweza kuwachukulia
hatua kwa kuwa wamegomea kazi ya ziada na si
kazi waliyoajiriwa na kuingia mkataba na chuo.
Kwa hali hiyo, Profesa Ndalichako alisema
serikali ililazimika kuingilia kati ambapo Mei 10,
mwaka huu Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella
Manyanya alikwenda chuoni hapo kutafuta
suluhu.
Mbali na Naibu Waziri, alisema hata makatibu
wakuu wa wizara hiyo nao walikwenda
kuzungumza na wahadhiri hao bila mafanikio,
huku wanafunzi hao wakikaa chuoni bila kuingia
darasani kwa wiki ya tatu.
Profesa Ndalichako alisema mbali na madai ya
wahadhiri hao, pia wakati wa kutafuta suluhu ya
jambo hilo, walitazama suala la tija kwa
wanafunzi hao wa diploma maalumu ambao ni
zaidi ya 7,800 na pia kwa wanafunzi wa shahada
ya kwanza ambao pia wanapaswa kufundishwa
na wahadhiri hao.
Kutokana na kukosa masomo kwa wiki tatu
mfululizo na kuwepo kwa uwezekano wa
kukosekana tija katika ufundishaji, Profesa
Ndalichako alisema ndio uamuzi wa kuwarudisha
nyumbani wanafunzi hao ukafanyika ili serikali
iangalie upya utaratibu wenye tija zaidi wa
kuwaendeleza wanafunzi hao.
Aidha, Profesa Ndalichako alisema wakati
wanafunzi hao wakitakiwa kurudi nyumbani,
walizingatia hali yao ya kipato, kwa kuwa tayari
walikuwa wameshapewa fedha za kujikimu za
siku 60 tangu Aprili 21, mwaka huu. Profesa
Ndalichako aliwataka wanafunzi hao kuvuta
subira wakati serikali inatafuta namna bora ya
kuwapatia elimu hiyo kwa kuzingatia tija kwao.chanzo habar leo.
0 comments :
Post a Comment