Breaking News
Loading...

Advert

Friday, May 13, 2016

Mapato hospitalini yanuka ufisadi.soma zaid.

UFUNGAJI wa vifaa vya kielektroniki katika
hospitali za Serikali katika mikoa mbalimbali,
umeibua fukuto la ufisadi mkubwa, uliokuwa
ukifanywa katika makusanyo ya fedha wanazolipa
wagonjwa kwa ajili ya huduma.
Akizungumza bungeni mjini hapa jana katika
kipindi cha maswali na majibu, Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema
tangu mfumo huo wa kielektroniki uanze
kutumika katika hospitali nyingi nchini, mapato
yameongezeka.
Jafo alisema mafanikio hayo ya ukusanyaji wa
mapato kwa mfumo wa elektroniki,
yamesababisha katika sekta ya afya kwa sasa
ajenda kuu iwe kuongezea mapato ya hospitali
zote nchini, kuendane na utoaji wa huduma bora.
Hospitali ya Rufaa Mbeya Akitoa mfano wa
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Jafo alisema kabla
ya kufungwa kwa vifaa hivyo, ilikuwa ikikusanya
Sh milioni 70 kwa mwezi, lakini baada ya
kufungwa vifaa hivyo, mapato yameongezeka
zaidi ya mara saba na kufikia Sh milioni 500 kwa
mwezi.
Taarifa zinaonesha pamoja na ongezeko hilo la
mapato, bado hospitali hiyo iliendelea kukosa
vifaa muhimu vya tiba, ikiwemo mashine ya CT-
Scan, kiasi cha kusababisha mwanzoni mwa
mwaka huu Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis
Kigwangalla kuwajia juu watendaji wake.
Dk Kigwangalla alielezea kushangazwa kuona
hospitali hiyo ikikusanya Sh milioni 500 kwa
mwezi, huku ikidai kukosa CT-Scan na kutoa siku
60 kifaa hicho kifungwe. Katika maelezo
aliyopewa, Dk Kigwangalla alielezwa kuwa
ingawa ni kweli hospitali hiyo inakusanya Sh
milioni 500 kwa mwezi, lakini mahitaji ya dawa
pekee yanachukua zaidi ya Sh milioni 300, kabla
ya gharama nyingine ikiwemo za usafiri wa
magari.
Alielezwa kuwa hospitali hiyo imejipanga
kuchukua mkopo kutoka Mfuko wa Bima ya Afya
ya Taifa (NHIF), kwa kuwa ili kupata mashine
hiyo, wanapaswa kuwa na kuanzia Sh milioni 800
mpaka Sh bilioni 1.2.
Sekou Toure Mbali na Mbeya, katika Hospitali ya
Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure kwa mujibu
wa Jafo, kabla ya kufungwa kwa vifaa hivyo,
ilikuwa ikikusanya kati ya Sh 150,000 mpaka
200,000 tu kwa siku.
Jafo alisema baada ya kufungwa vifaa hivyo,
mapato hayo yaliongezeka mpaka karibu mara 21
na kufikia Sh milioni 3.2 kwa kila siku. Hospitali
ya Tumbi Mbali na Mwanza, Naibu Waziri huyo
wa Tamisemi, alisema mkoani Pwani katika
Hospitali ya Tumbi, nako kabla kufungwa vifaa
hivyo, makusanyo yalikuwa Sh 200,000 kwa siku
lakini baada ya kufungwa, mapato yakaongezeka
mara 20 na kufikia Sh milioni nne kwa siku.
Kutokana na mafanikio ya hospitali hizo, Jafo
aliwataka wabunge wote kufuatilia kwa makini
hospitali katika halmashauri zao za wilaya, ili kila
moja iweke mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya
kukusanya mapato katika huduma ya afya.
Aliwataka wabunge hao kuweka kipaumbele
katika kuhakikisha hospitali zote katika maeneo
yao, zinafungwa mifumo hiyo ya kielektroniki, ili
fedha zikusanywe kusaidia katika kuboresha
huduma za afya katika maeneo hayo.
“Tusipozingatia haya, hata tukipeleka fedha bado
tutakuwa na matatizo, ndio maana ajenda yetu
kuu ni kutumia mifumo ya kielektroniki, ili
kuongeza mapato katika sekta ya afya,”
alisisitiza.
Awali Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi
(CCM), alitaka kufahamu kama Serikali haioni
umuhimu wa kuiongezea fedha Hospitali ya Mji
wa Mafinga, ili ihudumie kwa ufanisi idadi kubwa
ya wagonjwa wanaohudhuria hospitali hiyo.
Pia Mbunge huyo alitaka kufahamu kama Serikali
iko tayari kuiongezea hospitali hiyo watumishi
mara mbili zaidi ya kiwango inachopata, ili iwe
na uwezo wa kutosha kukabiliana na mzigo wa
kazi.
Akijibu maswali ya mbunge huyo, Jafo alisema
Serikali imekuwa ikiipatia Hospitali ya Mji wa
Mafinga Sh milioni 90 kwa ajili ya maendeleo na
Sh milioni 90 kwa matumizi mengineyo ; na
kwamba inaweza kuongezewa fedha hizo
kulingana na wigo wa upatikanaji wa fedha.
Kuhusu watumishi, alisema hospitali hiyo ina
watumishi 209 na upungufu uliopo ni wa
watumishi 95, sawa na asilimia 31.3 na kwa
mwaka wa fedha 2016/17 imeidhinishiwa kuajiri
watumishi 18.chanzo habar leo.

0 comments :

Post a Comment

Back To Top